Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia machache kwenye Wizara hizi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri hasa wa Wizara hizi pamoja na Manaibu, nawapa hongeza sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mambo ya afya; kwa Mkoa wetu wa Morogoro kwa kweli na Tanzania nzima afya imefanya vizuri sana, Nashukuru kuona kwenye bajeti hii ya mwaka 2019/2020 tumeweza kutengewa fedha kwenye vituo vya afya Mkoani Morogoro ikiwepo Mvumi, ambayo imetengewa milioni 200 ambayo na mimi nimeshaichangia matofali 2000. Pia napongeza kwa upande wa kituo cha afya cha Dumila ambao na wenyewe wametengewe milioni 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwa vituo vya afya vingine ambavyo bado havijaweza kutengewa, kikiwepo kituo cha afya cha Mzinga, ambacho tayari wamejenga kwa nguvu za wananchi, lakini hakijakwisha, kikiwepo na Magadu pamoja na Mafisa na vituo vingine ambavyo sikuvitaja kwenye Mkoa wetu wa Morogoro kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia natoa pongezi zangu kwa Serikali kwa upande wa kutenga fedha za hospitali za Halmashauri ya Wilaya. Tunashukuru sana kwa upande wa Gairo, tumeweza kutengewa milioni 500, Kilombero milioni 500, Mvomero milioni 500, pamoja na Morogoro Wilaya milioni 500. Hii kwa kweli nashukuru kwa sababu Hospitali ya Mkoa ilikuwa inapata matatizo sana ya msongamano wa wagonjwa hasa kwa upande wa wazazi ilikuwa ni kazi kweli, kwa sasa hivi naona tatizo hili litakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona hela kwenye upande wa hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Morogoro ambayo inajengwa na inatumika, lakini haijatumika sawasawa kwa sababu bado haijakamilika. Kwa hiyo, naomba Serikali waweze kuangalia na waweze kunijibu kama kweli wamenitengea kwa sababu sijaona hela yoyote ya hospitali ya Manispaa pale mjini. Naomba hospitali hii iweze kuangaliwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa watumishi hasa kada ya afya pamoja na elimu kwa Mkoa wa Morogoro bado tuna matatizo. Kwa upande wa wataalam wa afya na hasa ukikuta kwenye vituo vile ambavyo viko pembezoni kwenye Wilaya za pembezoni kama Malinyi, Ulanga unakuta kuwa kituo cha afya au zahanati inaweza ikawa na Mganga mmoja ambaye hawezi. Halafu mimi mwenyewe nimeshuhudia, unakuta hivi vituo vya afya vingine vinafungwa saa tisa. Jioni havifanyi kazi, usiku havifanyi kazi, hapo kwa kweli sielewi. Naomba Wizara waliangalie kwa sababu ugonjwa hauchagui ni saa ngapi unaumwa, saa yoyote unaumwa, kwa hiyo naomba waliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu, Walimu ni pungufu na hasa kwa upande wa Walimu wa sayansi naomba watupatie hao Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha sana kuipongeza Serikali kwenye miradi ya kimkakati kwa kweli Manispaa ya Morogoro tunaringa na wananchi wanajivuna na Mkoa wa Morogoro wote kwa sababu Manispaa ni kioo. Mpaka sasa hivi tuna soko ambalo tunajenga, soko zuri sana ambalo tumetengewa shilingi bilioni tati na milioni mia tano kwa bajeti hii. Kwa hiyo tunashukuru, pia tuna wale wanaopita pale Stendi, wote mnaiona kuwa Stendi ya Morogoro ni nzuri kwa hiyo tunaishukuru Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya msingi bila malipo, Mkoa wa Morogoro kwa kweli Serikali inafanya vizuri chini ya Mheshimiwa Rais, lazima niipongeze kwa sababu upande wa elimu bila malipo, kwa upande wa shule za msingi tumeweza kutengewa zaidi ya billioni sita na pia kwenye sekondari zaidi ya bilioni sita. Tunaishukuru sana Serikali iendelee kufanya vizuri kama inavyofanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ninaloomba ni kwa upande wa hosteli, hospitali ambazo zitajengwa naomba ziweze zijengwe kwenye shule za wasichana kwa sababu watoto wa kike wanapata matatizo sana na wao wanayajua kwa mimba za utotoni na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuwa kuna magari kama 40 ambayo yatanunuliwa na kutawanywa kwenye halmashauri ambazo zina mazingira magumu. Kwa kweli kwenye Halmashauri ambazo zina mazingira magumu naomba kuomba kupatiwa gari moja kwa Halmashauri ya Malinyi, ambayo iko mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wananchi kiuchumi, asilimia nne kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa walemavu ni jambo zuri sana ambalo limeweza kufanywa na Serikali, lakini kuna wale ambao hawatimizi masharti. Naomba hayo masharti yaangaliwe vizuri kusudi hao vijana waweze kurudisha kwa wakati na hizi hela ziweze kuwasaidia. Kwa upande wa wanawake wanarudisha vizuri, lakini vikundi viko vingi, kwa hiyo naomba Wizara wanisikilize, waweze kuangalia jinsi ya kuwasaidia hawa wanawake ili waweze kupata hela nyingi na za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TARURA, ni kweli wanafanya vizuri lakini wanapata hela kidogo. Kwa upande wa Morogoro kwa barabara za vijijini naona hawajaweza kuendelea vizuri kwa sababu hela hazitoshi. Kwa hiyo, naomba waongezewa hela ili kusudi waweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Manispaa kuna barabara za pembezoni ambazo wanazisahau. Kwa mfano kama barabara za Magadu na SUA kwa wasomi. Naomba na zenyewe waweze kuzitengeneza vizuri kadiri inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwa upande wa lishe. Tanzania yetu ina udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo 34% wamedumaa, kuna utapiamlo lakini Serikali imeweza kuona kuwa ni jambo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Dkt.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja za Wizara zote mbili, ahsante sana na Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)