Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. Naomba nianze kwa kuungana na walionitangulia kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wa TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora kwa kazi nzuri wanazofanya chini ya Ofisi ya Rais. Suala la utawala bora ni mtambuka na nyeti na ndiyo maana labda Wizara hizi zipo chini ya Ofisi ya Rais, kwa hiyo, hapa tunazungumzia mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo basi, nianze tu kwa kueleza kwamba mapema mwaka huu nilikuwa na changamoto za kiafya nikaenda kutibiwa Marekani nikapata nafasi kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katika maongozi yetu, alinipongeza sana na alisema maeneo yafuatavyo, namnukuu, alisema: “You know Anna Tanzania is unique”. Ina maana kwamba Tanzania ni nchi ya pekee. Akasema kwa sababu katika katika nchi za Afrika ni nchi ambayo ina utamaduni na inaonyesha kwamba ina uwezo wa kuwa na changamoto zake na ikazitatua yenyewe. Hayo ni maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Kiingereza anaitwa Secretary General of the United Nations, kuna wenzetu hapa walikuwa wanataka kukusikia Kiingereza chake. Tulipofika hapa katika dhana nzima ya utawala bora, sina budi kuwapongeza majemedari wetu Waheshimiwa Mawaziri ambao wana dhamana ya sekta hizi na Mheshimiwa Rais kwamba tulipofika si haba. Hii ndiyo salamu ambayo naileta kutoka kwa marafiki zangu na watu wengine ambao niko nao, juzi juzi nimetoka nchi za Nordic tulipofika si hapa. Ukiangalia Rais alipoanzia katika kuleta utawala bora tulianza na janga la madawa ya kulevya…

MBUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Kwa vyovyote mawazo yako juu ya mtu ni ya kwako lakini huwezi kusema mtu anayekuja kupambana na madawa ya kulevya atapata marafiki, hilo ni la kwanza na dunia inalitambua. Tukaingia katika changamoto ya mikataba mibovu iliyokuwa inatuumiza sana kwenye madini tukalikamilisha na mengine yanakuja. Kwa hiyo, katika dhana ya utawala bora, nafikiria Taifa zima bila kuangalia itikadi ya mtu tunatakiwa tuwe pamoja kuhakikisha kwamba tunaimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe kwa maumbile yangu (by inclination) ni mtu ambaye napenda sana hoja, ushindani na upinzani kama ikiwa lazima. Tunapozungumzia utawala bora lazima pia tuzungumzie upinzani bora maana hatuwezi kuwa na utawala bora kama hatuna upinzani bora, kwa sababu upinzani bora ndiyo utaleta utawala bora. Kwa hiyo, nataka kusema tunapokaa hapa wakati mwingine tunasahau context ya tunachotaka kufanya hapa.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa, kidogo tusikie taarifa, Mheshimiwa Mwakagenda.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuumpa taarifa mzungumzaji anayeongea ambaye ni Profesa Mbobevu katika nchi hii. Nataka kumpa taarifa kwamba alipokuwa anaongea na huyo Kiongozi wa UN angemueleza kwamba upinzani bora unahitaji fairness. Kwa hiyo, nilifikiri kwamba angemsaidia na kumpa uwazi wa kinachofanyika katika Taifa letu. Mheshimiwa Profesa nataka nikukumbushe nawe ulikuwa Waziri wa awamu zilizopita na madawa hayo hayo yalikuwepo wakati wewe ukiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa, taarifa hiyo.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mwakagenda kwa hiyo perspective yake. Nimeshasema mimi ni mtu ambaye nakaribisha mawazo mbadala ila naweza kumhakikishia maongezi yangu na Katibu Mkuu yaligusa mambo yote hayo na zaidi. Cha msingi ni kwamba Tanzania is unique, tulipofika ni pazuri na tujipongeze na Rais wetu anakwenda vizuri Mheshimiwa Mwakagenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde dakika zangu alizozichukua Mheshimiwa Mwakagenda. Baba Mtakatifu Francis katika kazi yake ya kujaribu ku-promote utawala bora na uongozi wa kiroho alikuwa katika nchi za Uarabuni alifika Dubai, alitoa nasaha ambazo kwa ukosefu muda sitaweza kuzisoma hapa lakini naomba nikabidhi nyaraka hii kama sehemu ya Hansard ya hotoba yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba Mtakafitu anasema ni lazima tujue changamoto zipo, tatizo siyo changamoto, tatizo siyo watu wanakusema, tatizo siyo kwamba watu wanakuonea, tatizo ni wewe una-respond namna gani? Kwa hiyo, usikubali mtu yeyote aku-pull down, wewe weka hoja mezani, nyaraka hii naikabidhi ili isaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiona kwenye mitandao Baba Mtakatifu anahakangaika na wenzetu wa South Sudan. South Sudan watu hawaelewani, sasa Baba Mtakatifu ameamua kuwapigia magoti, mtaona kwenye mitandao nadhani ina-trend, utawala bora pia unaamanisha dhamira zetu, kama unataka utawala bora lazima uangalie pia dhamira zetu. Kwa mantiki hiyo basi na kwa sifa tulizonazo tusizipoteze kwa kuokosa nation dialog. Ni kwa mantiki hiyo basi nataka kuchangia ifuatavyo:-

Mhehimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa utawala bora utataka utawala wa sheria na haki. Utawala bora lazima utokane na sheria na haki, sheria peke yake bila haki haiwezi kuleta utawala bora. Kwa mantiki hiyo, nataka kusema kwamba suala la haki Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, naomba liangaliwe kwa umakini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP) ni lazima ijiangalie pia kwa sababu huwezi kuwaweka watu gerezani bila kusikiliza kesi zao ukasema nina utawala bora. Hiyo naiweka kwa perspective niliyosema kwamba hapa tunachangia, hili ni Bunge la Jamhuri, tatizo letu hapa huwa ni ideologies zinatufanya tunashindwa kwenda forward. Kama mtu unatuhumiwa una makosa ni sawa lakini wachunguzi kama hawajawa na ushahidi, kusudi tukae vizuri mbele ya Mataifa na majirani wanaotuangalia na humu ndani, naomba suala hilo tuliangalie na nalisema hili bila kuwa na usabiki wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa, muda wako umeisha.

WABUNGE FULANI: Aaaaaa.

MBUNGE FULANI: Mwongezee.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Dakika tano, bado jamani, sijui kama nimeongea dakika tano. Kama nimemaliza dakika zangu nitaweka…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tibaijuka, kwa sababu Kanuni pia zinatambua watu fulani ambao wametoa mchango mkubwa kwa nchi hii na kwa Bunge hili, kwa hiyo, nakuongezea dakika tano. (Makofi/Kicheko)

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa heshima hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, naomba niende haraka na nitaweka hapa mchango wangu kama ulivyoandikwa, kwa sababu mimi ni Profesa nimeandika uingie wote kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya muhimu ya kusema, niende kwenye suala la kuwezesha watu wetu katika utawala bora, kuna suala la kuwalipa wakandarasi wa ndani. Wakandarasi wa ndani sasa hivi Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa nalileta kwenu ni suala la utawala bora kwa sababu wasipolipwa fedha hawawezi kufanya kazi, hatuwezi kujijengea uwezo, tutabaki na Wachina peke yao. Kwa sababu ya muda umekuwa mfupi nimelifafanua katika hotuba yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nikupe nyaraka nyingine ambapo kuna kitu kinaitwa Ilani ya Usafi. Utawala bora pia ni mkono wa Serikali wa kushoto kujua wa kulia unafanya nini. Sasa hivi kuna tabia mbaya, naomba niseme kwamba Maafisa Afya na Mazingira wanakwenda kwenye shule binafsi na hapa na-declare interest kwa sababu nina shule, wanategemea uwape bahasha kama bahasha haipo imekula kwako, unakuta unaandikiwa Ilani Chafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikukabidhi Ilani moja hapa ambayo imeandikwa kwenye Shule ya Wasichana ya Barbro ambayo huwa naisaidia, inasema tuong’oe vyoo (WCs) kama hivi hapa Bungeni tuweke vyoo vya kuchuchumaa. Hata hivyo, Bwana Afya hajui kwamba kwa wanawake kuchuchumaa inaweza pia ikaeneza UTI, hapa ndipo tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalileta jambo hili hapa mtu atashangaa kuwa ni la kisekta, siyo la kisekta ni la kiutawala bora. Sheria ya Elimu ndiyo inatawala shule, watu wa mazingira na watu wengine wale wakitaka kuingia kwenye shule lazima waende na Mkaguzi wa Shule, vitu kama hivi havifanyiki vinatuletea matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijakaa hili lazima niliseme ni muhumu sana, naomba sana Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa na nadhani na Mheshimiwa Rais pia atatusikia ni kuhusu suala la watumishi walioachishwa kazi kwa sababu walidai kwamba wamemaliza form four wakati hawakumaliza, naomba tena Mheshimiwa Rais atumie huruma na hekima yake kuliangalia upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa nafasi yangu ukiniuliza nasema kuna wengine walijaza form wakisema kwamba wana form four kwa sababu mabosi wao waliwaambia jaza form four. Tuje humu Bungeni, Mheshimiwa Lusinde leo sijui kama yupo au hayupo yeye huwa anapenda kujiita darasa la saba lakini namjua ana-masters ni kwamba hana cheti tu. Unaona ni persepective tu huwezi kusema Mheshimiwa Lusinde ni darasa la saba siyo darasa la saba huyu, kwa elimu yake ana-masters na zaidi lakini kwa sababu ya certification ndiyo tusema darasa la saba, sisi tumekwama kwenye certification tunashindwa kwenda mbele. Kwa hiyo, naomba niseme jamani, jamani suala hili ni muhimu sana kuangaliwa upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kutunza vyeti, siyo kazi ya individual. Ni kazi ya NACTE, BRELA, Wizara ya Ardhi na wengine. Sisi raia hatuna safe ambayo ni fireproof kwa mfano. Kwa hiyo, cheti changu kikiungua nakwenda NACTE kuomba cheti changu. Sasa nina kesi za watu ambao ni Maprofesa, wamesimamishwa kazi katika Vyuo Vikuu kwa sababu walipoteza vyeti vya Form Four. This is not serious. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nitaleta kwa maandishi. (Makofi)