Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia Makadirio ya Bajeti ya Wizara hizi ambazo ziko chini ya Ofisi Rais, TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora. Nianze na jambo la Utawala Bora ambalo Mheshimiwa Prof. Tibaijuka ameligusia kidogo. Naomba nilipanue zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na utamaduni hivi sasa, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kukamata watu. Hatujui kama kesi hizo wanabambikiwa au ni kesi halali, lakini baadaye tunaona kwamba watu wale wanakubaliana na Ofisi ya DPP, wanalipa fedha kesi zinakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nchi yetu ipate ufafanuzi, kwa sababu namna ambavyo jambo hili linafanywa, kwanza inawezekana kuna uonevu mkubwa sana kwamba kuna watu ambao wanabambikiwa kesi, wanapewa money laundering offences, wanawekwa ndani ili wakazungumze na DPP halafu waende Mahakamani wakiri walipe faini ya kile kiwango ambacho wameshtakiwa nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano dhahiri ni wa juzi, ambapo taarifa ambayo VODACOM wameitoa, kwa sababu VODACOM ni listed Company; hawa watu wengine inawezekana negotiations zinafanyika na DPP zinaishia kimya kimya hatujui, lakini kwa VODACOM kwa sababu ni listed Company waliweka taarifa yao ile public kwa sababu wako listed kwenye Dar es Salaam Stock exchange na Johannesburg Stock exchange.

Mheshimiwa Mwenyekiti, VODACOM wanasema, VODACOM Tanzania has reached an agreement with Director of Public Prosecutions (DPP) for five detained employees to be released. The agreement include payment of five point two billion Tanzania Shillings by VODACOM to Tanzania in order to settle charges initiated by DPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nipate uelewa. Nchi yetu haina sheria wala kanuni zinazowezesha pale ambapo mtu anakuwa ametuhumiwa kujadiliana na prosecuter ili ama kupunguza adhabu au kufuta adhabu au kulipa faini. Haya makubaliano ya DPP na watuhumiwa yanaendeshwa kwa sheria ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa revenue book, kila Mbunge amepewa. Ukitazama revenue books hizi, kuna kila senti ambapo kila Idara ya Serikali inaingiza. Nimeangalia Vote 35 - The National Prosecutions Services, kwa miaka mitatu yote ya nyuma na hata mwaka huu, wanatarajiwa kuingiza shilingi milioni 14 tu. Mwaka 2018 peke yake DPP wamefanya transactions za zaidi ya shilingi bilioni 23 kwa watu ambao wanakamatwa na ku-settle kesi kati yao na DPP wanaenda Mahakamani kesi zinafutwa. Naomba kufahamu, kwa sheria ipi? Fedha zinakwenda wapi? Nani anazikagua hizo fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni jambo ambalo tukilikalia kimya tunatengeneza a gangstar republic, kwamba dola inaweza ikaenda ikamkata mtu, ikamzushia, ikamwambia ukitaka utoke, toa hela; watu wanatoa hela, wanatoka. Hatuwezi kuendesha nchi kama gangstars. Naomba tupate maelezo ya jambo hili, ni namna gani ambavyo linakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili…

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti,...

MBUNGE FULANI: Tulia wewe…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella Manyanya.

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kwa mujibu wa kauni ya 64 1(a) na kuendelea, naomba kufuatia maelezo ambayo Mheshimiwa Zitto anayazungumza, badala tu ya kuyaweka kwa ujumla jumla na kwa sababu vyombo anavyovizungumzia ni vizito na vinavyoheshimika katika nchi hii, ni vyema akatoa kwa vielelezo vikaja mbele ya kiti chako ili hata watakapokuja ku-respond wajue ni kitu gani anakizungumzia kwa uhakika. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zitto.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kulizungumzia ni TAKUKURU. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAKUKURU ndiyo Taasisi ambayo tumeipa dhamana ya kupambana na Rushwa. Nimeona kwenye bajeti ya mwaka huu tunawaombea shilingi bilioni 75, lakini taarifa ambazo ninazo za uhakika ni kwamba kwa takribani miaka minane iliyopita TAKUKURU hesabu zake hazijawahi kukaguliwa na auditor yeyote yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu kutoka Ofisi ya Utawala Bora, ni kwa nini TAKUKURU, licha ya kwamba sheria tuliyoitunga mwaka 2007 inataka wafunge mahesabu na wakaguliwe, kwa nini TAKUKURU hawakaguliwi na kila mwaka tunawatengea mabilioni ya fedha, tunawaamini kwamba wanapambana na rushwa, lakini wao wenyewe fedha ambazo tunawapa hazikaguliwi na wala hili Bunge haliwezi kuziona? Ni kwa nini jambo hilo linaendelea kufanyika? Naomba Serikali iweze kutoa maelezo ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, utawala bora pia na hili jambo ni la muhimu sana; kuna watu kwenye nchi ambao ni lazima mhakikishe ya kwamba hawakugusiki na mambo machafu au hata hisia. Nimesoma hotuba ya Ofisi ya Rais hapa ukurasa wa 87 ambapo Bunge linajulishwa kuwa kwa mujibu wa GN Na. 252 ya mwaka 2018, sasa Wakala wa Ndege za Serikali umehamishiwa Ofisi ya Rais kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kwamba mwaka 2017/2018 tulitenga fedha shilingi bilioni 509, mwaka uliofuata shilingi bilioni 497 na mwaka huu zinaombwa shilingi bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa ndege za ATCL. Sisi wote tunajua ATCL hawamiliki ndege zile. Ndege zile zinamilikiwa na Wakala wa Ndege wa Serikali. ATCL inakodishiwa ndege zile. Halafu tumepitisha huko, tunategemea kwamba CAG atakwenda kukagua Wizara ya Ujenzi na kadhalika, ghafla tunaambiwa kwamba Wakala wa Ndege za Serikali hayuko tena Ujenzi, iko Ofisi ya Rais. Serikali inaenda kuficha nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mtu mwingine anafanya procurement, una mtu mwingine anamiliki ndege, una mtu mwingine anaziendesha zile ndege; Serikali inataka kuficha nini? Kwa nini mnafanya mambo bila kutumia maarifa mnajaza jambo kama hili lenye ma-procurement ya hela nyingi, chini ya Ofisi ya Rais? Likitokea doa hata kidogo, mmnamgusa Rais moja kwa moja. Nasi hatulaza damu, tutasema moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hivi vitu huwa vinatenganishwa ili angalau Mkuu wa Nchi anakuwa juu aweze ku-deal na hawa wa chini. Mnalundika procurement yote, zenye utata hatujui zilitangazwa lini, negotiations zilikuwaje, ndege zinadondoka kila siku. Juzi hapa KQ Dreamliner yao imekwama, imetua Dar es Salaam. Ikianguka yetu hapa, twende tukamlaumu Rais? Hivi si ni vitu vya kawaida tu ambavyo wataalam mnapaswa kukaa na muepushe! Hata mwenyewe akitaka, mnamwambia mzee hatuwezi kufanya, tukifanya tutakuletea shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo ya Serikali ni kwa nini maamuzi haya yamefanywa? Maamuzi haya mmefanya wakati Bunge linaendelea, maana yake ilikuwa Bunge linaendelea, ni Juni 2018, tayari tumeshapitisha Bajeti inayokwenda kununua hizo ndege kwa ajili ya kwenda Wizara ya Ujenzi, halafu pia mambo yote hayo yamepelekwa Ofisi ya Rais na tunajua hapa kuna controversies za Vote 20 ambazo naomba nipate maelezo haya ya Serikali... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)