Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ELIBARIKI E. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi na Bunge lako tukufu kwa kunipa nafasi ya mimi kutoa mchango katika ofisi ya Rais TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mimi binafsi naomba ku-declare kwamba Mheshimiwa Freeman Mbowe namuheshimu sana kama kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa sababu ni mtu makini nina imani. Hata hivyo, kuna vitu ambavyo kaka yangu Mheshimiwa Mbowe amevizungumza naomba nivitolee ufafanuzi kidogo sana hasa katika suala zima la ulinzi wa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ulinzi wa Rais, naomba nieleweke, kwa namna ambavyo Rais wetu amechukua maamuzi katika masuala mazima ya uchumi wa nchi, usalama wa Rais wetu lazima utakuwa kwenye mashaka makubwa kwa sababu ya maamuzi Rais wetu aliyoyachukua. Wewe ni shahidi, Bunge lililopita Mheshimiwa Zitto Kabwe na timu yake walileta hoja hapa kuna watu walipiga fedha katika masuala ya ESCROW, Mheshimiwa Rais Magufuli ameingia madarakani, watuhumiwa wote waliokuwa wamefanya ubadhirifu kwenye mambo ya ESCROW, amewakamata, sasa wako magerezani. Kwa kiwango cha fedha zilizokuwa zimeliwa, Rais amekamata watu hawa mnataka kuniambia hawa ma-Taikun hawana watu wanaoweza wakaleta insecurity kwa usalama wa Rais? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema Serikali inatekeleza miradi ambayo Wazungu wanaipiga vita, Stiegler’s George, tunakwenda kuzalisha MW2400 za umeme, Wazungu wanapiga vita, Rais kwa ujasiri anatekeleza hilo. Hizi ni ahadi zilifanywa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jasiri na jemedari Rais wa Awamu ya Tano anayetokana na Chama cha Mapinduzi ameingia madarakani, hajaangalia Wazungu ameangalia maslahi ya nchi, Stiegler’s George inajengwa, mnafikiri Wazungu wanafurahi? Mnafikiri usalama wa Rais utakuwa sawasawa? Leo tunavyozungumza Rais anajenga Standard Gauge, mnafikiri mataifa ya Ulaya wanapenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe taarifa, ulinzi wa Rais tena uongezwe mara dufu kwa sababu usalama wa Rais wetu kwa mambo anayoyafanya kwa maslahi ya Taifa hili hatuwezi kuacha usalama wa Rais ukawa katika stake kwa sababu tunaogopa kupiga makofi, Wazungu walikuwa wanataka wavae vichupi wakapige picha kwenye Stiegler’s George kule Ruvu, haiwezekani. Tunaomba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na sisi ndiyo majority, ndiyo sauti ya nchi humu Bungeni, ulinzi wa Rais wetu ikiwezekana uongezwe hata mara kumi zaidi kwa sababu usalama wake hauko sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kulizungumza ni suala la utawala bora. Mwaka mmoja baada ya kuingia hapa Bungeni tuliona Taifa letu lilivyojaribiwa na hapa mimi nazungumza kwa sababu toka nimemaliza kusoma chuo kikuu sijawahi kufanya kazi mahali popote zaidi ya kuitumikia Serikali hii. Tumeingia Bungeni hapa kuna mambo mengine Serikali haiwezi kuya-disclose kwa sababu ya siri za nchi, Mataifa ya Ulaya kwa kushirikiana na watu ndani ya nchi mmeona kilichokuwa kinatokea kule Rufiji, watu wameuawa Kibiti, ili Taifa kudhihirisha kwamba lina utawala bora, dola ya Tanzania imekwenda kudhibiti upumbavu uliokuwa unafanyika pale Kibiti na nchi imetulia. Nataka niseme katika suala la utawala bora hakuna mahali ambapo tunaweza tukapigia kelele utawala bora, tunafanya vurugu, tuache Taifa letu liwe torn apart, never shall we allow this. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye michango, moja ya vitu pia ambavyo tunaweza tukavizungumza katika utawala bora ni equal distribution of national cake. Nampongeza sana Mkurugenzi wa TARURA na timu yake na Mheshimiwa Jafo na timu yake na Mzee wetu Mheshimiwa Mkuchika, toka nimeingia madarakani fedha zilizoletwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwasaidia wapigakura wanyonge, walipa kodi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeletewa fedha shilingi bilioni 1.3 na tumejenga madaraja; tumeletewa fedha za vituo vya afya Sepuka, Ihanja na sasa hivi tuna kituo cha afya kule Iyumbu, yote haya ni mambo ya utawala bora. Zaidi ya hapo, hata kwa Jimbo jirani la kaka yangu Mheshimiwa Tundu Lissu ambaye amepata matatizo, hapa napozungumza Serikali ya CCM bila kujali hayupo na anaumwa, zimepelekwa fedha vijiji 19 watu wake wanachimbiwa maji. Leo mnataka kusema nini hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Mheshimiwa Esther Matiko anazungumza hapa, Serikali ya CCM hapa napozungumza imemjengea Kituo cha Afya cha Mkende kwa shilingi milioni 400. Hapa tunapozungumza Serikali imemtengea shilingi bilioni 8 kumjengea soko la kisasa pale kwake Tarime. Hapa tunapozungumza boma lake la Halmashauri amepelekewa shilingi bilioni 2 na shilingi milioni 500 zimeshakwenda. Msije hapa kuwadanganya Watanzania, msije hapa kuudanganya umma, sisi tunachokisema Serikali ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Dkt. John Joseph Magufuli inafanya kazi. Nataka niwaambie, mimi kwenye Jimbo langu Rais alipata asilimia 73 ya kura ya uchaguzi uliopita lakini kwa kazi hizi 2020, Rais anakwenda kuchukua zaidi ya asilimia 95 ya kura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nitoe rai kwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba unilindie muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema sina maana kazi yangu hapa ni kuja kusifu tu lakini upotoshwaji unaofanywa juu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, nikiwa kama Mbunge nayetokana na chama hiki lazima tuje hapa Bungeni tuweze kufafanua ili dunia na Watanzania waweze kujua ni kweli chama chetu na Serikali yetu inatekeleza au haitekelezi. Ndiyo maana nimetoa mfano, Jimboni kwa kaka yangu Mheshimiwa Tundu Lissu aliyepata matatizo, hayupo hapa Bungeni lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi imepeleka miradi ya maji katika vijiji 21 na hapa tunapozungumza miradi ya maji inaendelea kutekelezwa. Nimesema miongoni mwa mambo ambayo yanaweza yakaingia katika components za good governance ni pamoja equal distribution of resources na national cake na ndivyo Serikali ya Chama cha Mapindizi inavyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimalize kwa kusema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umekwisha.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, kidumu Chama cha Mapinduzi. (Makofi)