Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Waziri wa Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Capt. Mkuchika; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa; Makatibu wote wawili na Watendaji wa Wizara hii kwa kazi nzuri sana wanayoifanya na pia kwa kuwasilisha hotuba yao hapa ili tuweze kuijadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mkurugenzi wa TASAF kwa kazi nzuri aliyofanya katika Mkoa wetu wa Iringa. TASAF imefanya vizuri sana, imeweza kusababisha hali ya kaya masikini na kuwa na hali zenye unafuu wa maisha japokuwa mwanzoni kulikuwa na ukiritimba katika kuzibaini. Kuna baadhi ya watendaji walitaka kutumia kisiasa kaya za watu masikini na walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Waziri wa Utumishi Mheshimiwa Capt. Mkuchika kwa kuitembelea kaya masikini na yenye watoto walemavu zaidi ya watatu inayoishi katika Kijiji cha Lulami na kujionea jinsi ilivyo na kuiongezea kipato na kuipatia TV. Nilikuwa naomba kujua: Je, kaya masikini na yenye watoto wenye ulemavu kama hiyo, Serikali inawasaidiaje kuwapatia angalau mradi endelevu unaoweza kusaidia watoto wenye ulemavu kama hao ambao hawana hata uwezo wa kutembea kabisa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa sana la upandishwaji wa madaraja kwa Walimu na wanapopandishwa marekebisho ya mishahara hayafanyiki kwa wakati na kusababisha mpaka wakati mwingine Mwalimu anastaafu lakini mshahara wake unakuwa haujarekebishwa. Je, nini mkakati wa Serikali kwa changamoto kama hiyo? Hii inasababisha usumbufu mkubwa sana kwa wastaafu ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa mafao yao wanapostaafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana kwa wafanyakazi wanapokaimu nafasi kuthibitishwa. Je, sheria inasemaje ili kumpatia haki mtu anapokaimu kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.