Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbeya Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi, lakini kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza na ni bajeti yangu ya kwanza, nimshukuru sana Jehova, lakini nimshukuru Mheshimiwa Rais pia kwa kuendelea kuniamini na kunipa nafasi hii nimsaidie kwenye eneo hili. Nimshukuru pia Waziri wangu, Mheshimiwa Kapteni Mstaafu George Huruma Mkuchika, kwa kunipa ushirikiano mzuri na vilevile kunipa mwongozo mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajibu kwa ufupi, lakini nichukue fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia kwa mdomo na vilevile wale waliochangia kwa maandishi katika hotuba yetu au bajeti ya ofisi yetu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Vilevile niishukuru Kamati yetu ya Bunge na niombe tu kusema kwamba yale yote ambayo yamechangiwa kwa maandishi, kwa mdomo tumeyapokea tumeyachukua na tutayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi kabisa kama nilivyosema nitayajibu kwa pamoja nikianza na lile la kukaimu. Leo asubuhi nimejibu hapa suala hilohilo la kukaimu kwamba kuna watumishi wengi, kuna viongozi wengi wanakaimu kwa muda mrefu. Ukweli ni kwamba wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu kutokana na kwamba hizi nafasi huwa wanakaimishwa kule na waajiri wao kienyeji tu, unakuta kwamba huyu anampenda basi anaona ni bora akakaimu kwenye hiyo nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba, kuna waraka kabisa umetumwa mwaka jana Septemba, 2018 kwamba nafasi zote zile za kukaimu lazima zipate kibali kutoka Utumishi na kukaimu kwenyewe kusizidi miezi sita. Kukaimu ni nafasi ya muda, sio kwamba maana yake wewe utathibitishwa au tayari umeshateuliwa, hapana. Kwa hiyo niwatake waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba wanafuata sheria, kanuni na taratibu wanapokuwa wanakaimisha wale viongozi kule katika maeneo yao ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa ufupi ni kuhusu watendaji wakuu kuhamahama na watumishi kwenda kwenye ofisi zao nyingine. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba watendaji wakuu kuhama na watumishi hiyo sio sahihi kwa sababu utumishi wa umma ni obedience, utumishi wa umma ni utii, kokote kule unakokwenda, kwanza ukipewa transfer unatakiwa kufanya kazi mahali popote utakapokuwa umepangiwa, lakini vilevile na kule unakokwenda na kwenyewe kuna watumishi wa umma. Kwa hiyo sio vizuri kusema kwamba unahamahama na watumishi, utawakuta kule na wao sana sana unachotakiwa kufanya ni kuwajengea uwezo ili na wenyewe waweze kuwa ni watendaji wazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu muda wa likizo ya uzazi; naomba niseme mimi pia ni mama, tunaelewa adha ya kujifungua. Likizo ya uzazi, naomba niseme, sisi kama Serikali katika zile siku 84 tumeongeza siku 14 zaidi, lakini tunaelewa kama wanawake consequences za kujifungua mtoto zaidi ya mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lililozungumzwa ni idadi ya wanawake ile 50 kwa 50. Katika utumishi wa umma, naomba niseme kinachoangaliwa ni sifa, vigezo, ubunifu na umahiri wako wa kazi na vilevile je, unaendana na ubunifu na kasi ya Serikali tuliyopo, sio tu kwamba eti kigezo chako kitakuwa kwa vile ni wewe ni mwanamke, kuwa mwanamke ni sifa ya ziada endapo kuna maeneo mawili labda umechuana na mwanaume lakini sasa wewe kwa sababu ni mwanamke basi hapo unapewa priority.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndugu zangu wanawake sote tunaelewa sisi ni jeshi kubwa, tuendelee kujiamini, tunaweza tukipewa, kubwa la msingi na sisi tunapobebwa tuoneshe kwamba tunabebeka. Hili sizungumzii masuala ya Madiwani na Wabunge, nazungumzia katika utendaji kazi kwenye utumishi wa umma na wanawake ni jeshi kubwa. Kwa hiyo tukibebwa lazima tuoneshe tunabebeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kutowapandisha watumishi mishahara. Hili suala lilikuwa limesitishwa kutokana na sababu mbalimbali, lakini sisi kama Utumishi, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba vijana wetu wa kizalendo, vijana wetu wa Kitanzania tumekuwa tukitumia ule Mfumo wa Lawson, Version 9, lakini sasa hivi hawa vijana wetu wa Kitanzania wanaleta mfumo mwingine mpya ambao una nguvu zaidi, capacity yake ni kubwa zaidi na gharama zake ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mfumo tutaanza kuutumia kuanzia Juni na naomba niseme katika mfumo huu tutakuwa tumeboresha mambo mengi sana; masuala kwa mfano yale ya OPRAS, utendaji kazi Serikalini, watu wamekuwa wakifanya kazi kimazoea. Kwa hiyo ule Mfumo wa OPRAS ambao tutakuwa tumeuanzisha kutokana na mfumo wetu huu, wenyewe utasaidia kuziba mianya ya upendeleo, lakini vilevile kuziba mianya ya chuki, kwamba mwingine kwa vile anampenda fulani basi anamwongeza cheo au mwingine kwa sababu hujamsalimia asubuhi basi hakupendekezi. Kwa hiyo mfumo huu utakuwa ni wa kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwenye mfumo huu pia tunatarajia kuanzisha One Stop Centre katika maeneo yote ambayo yanatolewa huduma na utumishi wa umma. Tunategemea kuanzisha One Stop Center ili kusiwe na Mtanzania yeyote, mwananchi yeyote wa Kitanzania ambaye yuko katika Serikali ya uadilifu ya Awamu ya Tano kwamba asafiri kutoka Kigoma mpaka kwenda Mwanza, kwa hiyo One Stop Center kupitia mfumo huu itakuwa imeanzishwa katika mkoa mmoja na huduma zote atakuwa anazipata mahali pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie suala la utumishi wa umma; michango mingi imetoka hapa na sote tunaelewa kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma ni chuo nyeti na naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wa umma wote wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza, nitoe rai, hata kwa waajiri, wote nchini kuhakikisha kwamba wanapitia kwenye Chuo chetu cha Utumishi wa Umma, hii ni mandatory wala sio ombi na wale wote ambao watakiuka maagizo haya watachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu unapopita kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma kule kuna mambo mengi ambayo inabidi tufundishwe; jinsi gani ya kutunza siri za Serikali, jinsi gani ya kuwa na uadilifu, jinsi gani ya kuwa na uzalendo na mambo kama hayo. Kwa hiyo naomba nitoe rai kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wale wote wanaoajiriwa wanapita kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma ili kupikwa kama watumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana.