Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Nitaanza kwa kutafakari kwa pamoja. Ni dhahiri kwamba Taifa letu bado halijatambua thamani ya mazingira na afya ya mazingira na hili lipo linajionesha dhahiri ndani ya Serikali baina yetu sisi hapa Wabunge hata na jamii inayotuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu ukiangalia tu kwa Wizara zilizopita humu ndani Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tunagombania nafasi za kuchangia kama ni TAMISEMI au ni Utawala Bora au ni Ofisi ya Waziri Mkuu na vitengo vyake lakini sasa kama tulikuwa tunakimbilia kutetea shule, barabara, vyakula, afya na kadhalika tulitakiw atujue kwamba kiini kinachotubeba sisi kama Taifa na afya na uchumi wa Taifa, ni mazingira. Mazingira ndiyo kiini cha maendeleo. Tungelitambua hilo tukaisimamia Serikali ipasavyo tungetoka kwenye huu umaskini, kwa sababu hali ya umaskini inajengwa na vitu vikuu vitatu, uchumi duni, utawala bora na uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania mazingira ndiyo yanayotubeba, kwa sababu hata hao wananchi wetu huku vijijini asilimia 96 wanategemea maliasili, zaidi ya asilimia 90 wanategemea nishati kutoka kwenye maliasili. Kama tunaongelea viwanda, maji safi na salama inategemea na hali ya mazingira iliyopo. Kama mazingira yanachechemea hatutakaa tukote katika dimbwi la umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitunga Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 kama Mheshimiwa Waziri husika alivyosema na iliainisha mambo sita makuu ya uharibifu wa mazingira. Tuliainisha changamoto za uharibifu za vyanzo vya maji, hii tunaangalia mito, mabwawa, bahari na kadhalika; tuliainisha uharibifu mkubwa wa maji safi ambayo yanaenda kujenga uchumi kwa sababu kusipokuwa na wananchi wanaopata maji safi inaenda kuharibu afya yao binafsi, mifugo au na chochote kinachotegemea maji safi; tuliainisha uharibifu wa ardhi, ardhi ndiyo iliyobeba miundombinu ambayo tunaitegemea sisi aidha sekta za kilimo na vinavyobebwa na kilimo au ni shughuli za madini na kadhalika; na tuliainisha kwamba kuna upotevu mkubwa wa makazi ya viumbepori na bioanuwai. Hivi vyote kwa ujumla wake ni nguzo hizo sita ambazo zinabeba shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 22 iliyopita Mheshimiwa Waziri umesema haya na sasa hivi tunachanganua hii sera kwa upya wake, ardhi inasemaje, uharibufu wa ardhi upo katika percent ngapi na una-reflect vipi hali ya uchumi? Kwa sababu unapoharibu ardhi ina maana unaharibu na uzalishaji ambao unategemeana na ile ardhi. Kama unaharibu vyanzo vya maji hupati maji safi au maji yanayotakiwa unaenda kuwa reflected kwenye shughuli za kiuchumi. Tunalia kila siku kuhusu bajeti ya maji haitoshi, sasa tungeweza ku-link kuhusu upatikanaji wa maji, budget wise na upatikanaji maji kwenye kutunza vyanzo vya maji na njia za maji basi tungeweza kwenda sambamba na kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera yetu imeainisha mambo sita makubwa ambayo bado hayana ufumbuzi kwa sababu bado tunaharibu mazingira, sasa nayo yanakuwa reflected kwenye uchumi wetu. Uchumi wa mtu mmoja mmoja unategemea na hayo mazingira kwa sababu kila mtu anayategemea mazingira hayo. Mfano tu mfupi, usipokuwa na maji safi kwanza ukinywa maji machafu au maji hayako salama jamii hiyo husika inapata maradhi, kwa hiyo, inaenda ku-reflect bajeti ya afya, bdo tunazidi kuididiza. Kama hupati maji kwa ajili ya kilimo chako cha umwagiliaji unategemea mvua na sasa hivi kuna mabadiliko ya tabianchi ina maana uzalishaji wako utakuwa wa wasiwasi hutakaa utoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuipa nguvu Sheria yetu ya Mazingira ambayo imeainisha mambo makuu manne, kuna utafiti, uelimishaji na kadhalika, hii sekta inaweza ikatutoa hapa kwenye dimbwi la umaskini.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri. (Makofi)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwape bajeti inayotakiwa, ahsante. (Makofi)