Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Ofisi ya Makamu wa Rais na nitajikita zaidi kwenye suala zima la mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe masikitiko yangu makubwa sana kuhusiana na bajeti ya Wizara hii. Kama ambavyo hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani imesema imekuwa ni mazoea kwa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kutokutengewa bajeti ya kutosha na hata hiyo kidogo ambayo inawekwa haifiki kama ilivyokusudiwa, hivyo kupelekea ufanyaji kazi katika hii kuwa mgumu kuliko ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tunafahamu suala zima la mazingira ndiyo roho za sisi Watanzania. Tunapodharau mazingira tutegemee tutapata elimu na afya tunajidanganya. Bila mazingira hakuna afya, elimu na miundombinu vinginevyo tunajisumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wakizungumzia kuhusiana na sula zima la ukatazaji wa matumizi ya mifuko ya plastiki. Bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Mazingira, suala hili lilianza muda mrefu na sisi kama Kamati tulijaribu sana kuishauri Serikali na kuangalia ni kwa namna gani wanaweza wakafanya ili kusaidia hawa wenye viwanda ambao wanatengeneza mifuko ya plastiki waweze kutengeneza kwa teknolojia ya kisasa. Teknolojia za kisasa zipo ambapo mifuko hii mingine watu wanatengeneza na inaoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama Serikali imejiandaaje baada kuzuia matumizi haya kwa nchi jirani ambazo zinazalisha kwa wingi kuliko tunavyozalisha Tanzania mifuko ya plastiki kuingia nchini kwetu? Kwa sababu ni ukweli usiopingika Tanzania tunazalisha mifuko ya plastiki kwa asilimia 30 peke yake lakini asilimia 70 ya mifuko ya plastiki inayoingia nchini kwetu ni mifuko inayotoka nje ya nchi. Je, Serikali imejipanga namna gani kuhakikisha kwamba mifuko hii haiwezi kuingia nchini Tanzania na matumizi ya mifuko ya plastiki yakaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati tunakataza mifuko ya plastiki tumejiandaa na vifungashio vya aina gani? Kwa sababu nachokiona hapa ni makatazo tu lakini hatujaambiwa kwamba tunakwenda kutumia mifuko ya aina gani, leo tutakuwa tunabeba mikononi bidhaa ama tutakuwa tunafanyaje? Kwa hiyo, tungeomba sana Waziri anapokuja hapa atuambie ili Watanzania wajue baada ya mifuko ya plastiki kukatazwa tarehe 1 sijui Mei au Julai, nini ambacho kitatumika mbadala badala ya mifuko hii ya plastiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ya mazingira ni mtambuka kama nilivyosema, kwa hiyo lisiishie kwenye masuala ya mifuko ya plastiki peke yake, je, suala la mkaa limefikia wapi mpaka sasa? Kwa sababu ya kupata mkaa watu wanakata sana miti. Leo tunaambiwa nchi inakwenda kuwa jangwa kwa asilimia 61, hii ni asilimia kubwa sana kwa nchi ya Tanzania, tunapoelekea vizazi vyetu vitakuja kukuta nchi imeshakuwa jangwa, hali ni mbaya kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapofikiria zaidi mifuko ya plastiki, mimi huwa nasema vitu vidogo vidogo Mheshimiwa Waziri anajua, tusing’ang’anie na vitu vidogo vidogo kama mifuko ya plastiki tuangalie uhalisia wa mazingira, vitu vingi zaidi vinategemea mazingira yetu. Kama mazingira hayataboreshwa tusije tukategemea hivi vyote ambavyo tunavifanya vitaendelea kuwepo kwa sababu ni lazima vitapotea kutokana na kwamba mazingira siyo rafiki, tunakwenda kuingia kwenye ukame wa hali ya juu. Kama ambavyo mmeshuhudia kuna maeneo ambayo mvua hazijanyesha kabisa, kuna maeneo kama kwenye Mikoa yetu ya Tabora tulikuwa tunapata mvua misimu miwili, leo Tabora ukienda ni msimu mmoja tu ndiyo mnapata mvua na mvua zenyewe siyo za zinatosheleza, hali ni mbaya kweli kweli kila maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali iangalie upya kuhakikisha kwamba bajeti inayotakiwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais inapelekwa kama ilivyokusudiwa kuliko kutegemea bajeti za wafadhili. Hawa wafadhili leo umeomba bajeti ya asilimia 40 unaletewa bajeti asilimia 10, mwisho wa siku mambo yanakuwa hayaendi ama hawaleti kabisa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)