Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kwa kumshukuru tena Mungu kupata nafasi hii kutoa na mimi mchango wangu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara na Mazingira, na ni Mwenyekiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe mchango wangu baada ya kuwa nimekutana na wadau wengi sana pamoja na Kamati yangu, tulikutana na wadau wenye viwanda, wafanyabiashara lakini pia tulikutana na mamlaka za udhibiti, ziko nyingi, tulikutana nazo kama 19 hivi. Tulikutana pia na waagizaji wa bidhaa na wale ambao wanapeleka bidhaa nje. Pia tulikutana na Wizara ya Viwanda na Biashara. Kila tulipokutana swali langu la kwanza kwa Waziri lilikuwa ni kwamba hivi tunafanya muujiza gani ili tuweze kutekeleza hii azma ya Mheshimiwa Rais ya kuwa na viwanda katika miaka 10 ijayo? Waziri ni shahidi na hata Wajumbe wenzangu ni mashahidi, tuliuliza sana swali hili na kwa kweli hatukupata jibu kwa maana kwamba yale yote yaliyowasilishwa kwenye Kamati ni business as usual. Kwa kweli ni vizuri sisi Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani na sisi wa Chama cha Mapinduzi tutoe ushauri ambao utatutoa hapa tulipo utupeleke mbele. (Makofi)
Baada ya kutafakari, naomba niseme mambo kama sita hivi kwa kifupi, nadhani muda utanitosha. Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano una maneno mazuri sana na unasema vizuri sana, naturing industrialization in Tanzania. Maneno haya ni mazuri na Mheshimiwa Rais ameya-reflect wakati anafanya kampeni na sisi sote lazima tufikirie kwenda huko. Tukifanya kazi kama tunavyofanya tunaweza tusifike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ni lazima tuwe na quick wins sasa, vitu ambavyo tutavifanya kwa haraka tuone mabadiliko. Jambo la kwanza katika quick wins, ni viwanda vilivyopo na wafanyabiashara waliopo; tuwaondolee kero zao, tutengeneze mazingira mazuri, waweze kupanuka badala ya kufa. Walituambia wana kero sana na Waheshimiwa Wabunge wamesema, kero ni nyingi. Regulation ya udhibiti, kila mtu anakuja kudhibiti kiwanda kidogo. OSHA anakuja, nani anakuja mpaka unafunga. Kwa hiyo, Regulatory Authorities hizo bado zinachelewesha huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walisema mambo mengi; utitiri wa kodi, tozo na vitu vingi sana. Jambo lingine walilosema hao wenye viwanda vilivyopo, walisema service wanayopewa na hizi institutions, wakati mwingine wanazilipia kwa bei kubwa. Serikali inatakiwa itoe service hii bure kwa hivi viwanda ili viweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, walilosema miundombinu. Umeme unakatika sana. Pamoja na kwamba tuna mipango mizuri, tunaishukuru Serikali, lakini bado umeme uwe stable, reliable. Siyo unakatika! Kwenye kiwanda ukikata dakika tano, umechelewesha production kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia walisema kulinda bidhaa za ndani. Kuna hatua tunaona zinachukuliwa, tunaishukuru Serikali. Tulinde bidhaa za ndani dhidi ya bidhaa za nje. Viwanda na wafanyabiashara waliopo wana mambo mengi sana ambayo siwezi kuyasema, lakini Waheshimiwa Wabunge wamesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali mmeonesha vizuri sana kwenye hotuba, lakini pia kkwenye Mpango, viwanda vya kimkakati. Ukisoma kwenye mpango vimejatwa vizuri; viwanda vya chuma, vimetajwa viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo na viwanda vingine kama vya mazao ya uvuvi na mazao ya mifugo. Ukienda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, unaona ni kiwanda kimoja tu cha chuma ndio cha kimkakati, lakini viwanda vingine; sijui kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua mbu, sio cha kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuangalie hasa viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo. Hivi ni vya kimkakati kweli, sivioni kwenye speech! Kwa hiyo, tunaomba hilo liwe jambo la pili. Tunavyotaka kujenga viwanda vipya, ni hivi vitakavyohamasisha industrialization katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhamasisha wawekezaji. Tuliongea na wawekezaji wengi wa ndani na nje, wote walisema wanaonekana kama wezi. Mtazamo wa Watanzania wengi na mtazamo wa hata viongozi wengine, mwekezaji wa ndani anayepewa eneo kubwa anasumbuliwa, anaonekana mwizi, yule wa nje ndio kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, wawekezaji hawa wanahitaji misamaha. Japokuwa tulipitisha sheria mwaka jana, ile ya VAT ya mwaka 2015 nadhani, na mimi nilisimama hapa nikasema hii VAT ukiweka kwenye vifaa kwa ajili ya kutafuta madini, kwa ajili ya kuanzisha kiwanda, utafukuza wawekezaji. Kwa hiyo, nasema tena, tutazame hii misamaha tusiiogope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni kufufua viwanda vilivyokufa. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, viko viwanda vya mazao ya kilimo kama pamba. Igunga kule tulikuwa na Manonga Ginnery, ilikufa. Hatutazamii kufufua viwanda vya namna hii. Kule Tabora ndugu yangu amesema; viwanda vya nyama Mwanza, Shinyanga na kadhalika tumeviacha; viwanda vya chuma Tanga na kadhalika, tuvifufue hivi. Kuna viwanda vingine kama CAMATECH na Mang‟ula, vitu vya namna hii tuvitazame, tuvifufue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niseme maeneo ya kuwekeza (EPZA), tulipe madeni. Serikali itafute fedha ilipe madeni, Shilingi bilioni 191. Fedha hizi zitafuteni mlipe ili mpate maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani, naomba nimalizie kwa kusema, tulikubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba ili tuweze kupata gist ya mambo haya, tuitishe Mkutono wa wadau na tulikubaliana tuitishe Dodoma kabla ya bajeti. Tulisema wadau ambao tunataka tuwaitishe, tuzungumze tufanye dialogue hii, tujue; tukipata yale maneno ndiyo tuyaingize kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mwaka kesho tutakuwa na mpango mzuri zaidi kwa sababu tutakuwa tumepata mawazo ya wenzetu. Kwa hiyo, wadau ambao tulikubaliana, Mheshimiwa Waziri na hii lazima uitishe labda hata wiki ijayo ili tupate mambo haya kwa ajili ya mwaka kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.