Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Juma Kombo Hamad

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nami nafasi hii ya kuchangia mawili, matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametupa afya, bado tupo na tunaendelea na pia nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na msemo wa Kiswahili, watu wa Pwani tunakuwa na msemo tunasema kwamba, “ukipenda boga, basi upende na mti wake.” Siyo sahihi kwamba unapenda boga, lakini mti wake unautia moto. Hii itakuwa siyo sahihi na wala haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia udugu siku zote ni kufaana na siyo kufanana. Kama kufanana, miaka 50 tumefanana vya kutosha, lakini sasa tunatakiwa tuwe na mwelekeo mpya kabisa wa kufaana hususan katika masuala mazima ya kiuchumi. Kama tutajaribu kuimba na kusifu tu masuala ya Muungano lakini bila kusaidiana kiuchumi, bila kupeana fursa zaidi za kiuchumi, kwa kweli Muungano huu utakuwa hauna mwendo mwema na hauna afya kwa Watanzania hususan wale walioko Zanzibar kwa maana ya Wazanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kimsingi ni ukweli usiopingika kwamba Muungano kama Muungano ni muhimu na hakuna anayekataa hata mmoja. Siyo kweli kwamba kuna Wazanzibar fulani hawataki Muungano, siyo kweli kabisa. Wazanzibar wanataka Muungano. Kama alivyosema Kaka yangu Mheshimiwa Jaku tunahitaji Muungano ambao utakuwa na maslahi kwa pande zote mbili. Hatuhitaji Muungano ambao umejikita maslahi ya upande mmoja hii itakuwa siyo muungano. Naomba Mawaziri watakapokuja ku-wind up kwanza waje wanijibu masuala mawili ambayo tumekuwa tukiyazungumza mara kwa mara pale tunapopata fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kuhusiana na vyombo vya moto. Kwa kweli tumekuwa tukipata taabu sana Wazanzibar, hasa sisi Wabunge, tumekuwa tukibughudhiwa sana na TRA na Polisi kwa sababu tu tuna magari yamesajiliwa kwa namba za Zanzibar. Hii siyo halali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kwenye mchezo ule wa Simba na Mazembe ya Congo, tuliwakuta Wakongo wanahojiwa kwenye vyombo vya habari. Walikuja hapa na magari yao na wakafanya shughuli zao Dar es Salaam, Tanzania hii hii na halafu wakaondoka na magari yao. Leo hakuna Mzanzibar anayethubutu kuja Tanzania Bara na gari yake akatumia, hii siyo haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi na-declare kwamba ipo siku nilifukuzwa na TRA na Polisi usiku Dar es Salaam. Nasimama, wananiambia tuna wasiwasi na gari yako. Kwa nini? Unatumia namba za kigeni. Aah, nikashangaa, nikamwuliza wewe nani? Mimi Afisa wa TRA. Hii namba ya wapi? Namba ya Zanzibar. Hivi Zanzibar leo ni nchi ya kigeni na Dar es Salaam? Ananiambia kwani Zanzibar ni Tanzania Bara. Nikataka kujua kumbe hivi kuna nchi inaitwa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni vitu ambavyo vinahitaji majibu. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja anipe jibu sahihi juu ya suala hili kwamba ni lini sasa bughudha hii na adhabu hii itaondoka kwa Wazanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka Mheshimiwa Waziri aje anijibu kwa kina ni suala la uwepo wa Account ya Pamoja ya Fedha ambayo imetajwa wenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 133. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, mwaka juzi 2017 tulizungumza suala hili akaahidi kwamba linakwenda kutatuliwa; mwaka jana 2018, tulizungumza suala hili akaahidi kwamba linakwenda kutatuliwa. Leo tunataka commitment ya Serikali kwamba ni lini sasa suala hili linakwenda kumalizwa na tuone Account ya Pamoja ya Fedha ambayo itashughulika na mgawanyo sahihi wa mapato ya Muungano baina ya Zanzibar na Tanzania Bara au Tanganyika unakwenda sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya yanakuja kwa sababu moja; hakuna siku Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa na nia njema na Muungano huu. Hiyo ndiyo kauli simple kabisa, ndiyo kauli rahisi. Siku Muungano huu unaundwa uliundwa kwa siku mbili baina ya Mwalimu Nyerere na Karume, lakini tunazungumzia kero ya Muungano tena ambayo iko ndani ya Katiba inachukua miaka 50, nia njema iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuimba tu kwamba tuna nia njema, tunataka kutatua kero za Muungano, sijui tunafanyeje, wakati nia njema hakuna. Vijana wetu hao, wote vijana; Mheshimiwa Makamba na Mheshimiwa Mussa, wote wana utashi wa kuona kero za Muungano zinatatuliwa. Tena hata ukizungumza nao unahisi kwamba wanaumia na wako tayari kuona kero za Muungano zinatatuliwa. Ushirikiano wanaopata bila shaka ni tatizo, Serikali haiko tayari kuona kero hizi zinatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Muungano limekuwa na shida na ndiyo maana zipo taarifa zinasema na ni sahihi kabisa, hata mgogoro uliokuwepo katika miaka ya 1970 baina ya Mwalimu Nyerere na Karume sababu ilikuwa ni Muungano. Hata mgogoro uliomwondoa Jumbe kwenye madaraka kama Rais wa Zanzibar akafukuzwa Urais, akafukuzwa nafasi zote sababu ilikuwa ni Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mashehe ambao leo wako jela kwa mwaka wa sita sasa; siyo ugaidi, wala siyo suala la uanaharakati, wala siyo suala lolote, ni kwa sababu walisimama na Wazanzibar kudai maslahi zaidi…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: …ya kiuchumi kwa ajili…

MWENYEKITI: Taarifa. Mheshimiwa Kombo kaa chini kwanza.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji, anaposema kwamba Chama cha Mapinduzi hawana nia njema na Muungano huu na Chama cha Mapinduzi sasa hivi kina umri wa zaidi ya miaka 51 na Chama cha Wananchi CUF walipojaribu kuja na Muungano wa Shirikisho, Chama cha Mapinduzi ndiyo kilisimama imara kupinga Muungano ule wa shirikisho. Kwa hiyo, suala la kusema Chama cha Mapinduzi hakina nia njema na Muungano huu, siyo sawa sawa. (Makofi)

MWENYEMITI: Ahsante. Mheshimiwa Kombo, taarifa hiyo.

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuchauka ndugu yangu wewe umekwenda juzi CCM…

MWENYEKITI: Jibu taarifa yake. Mengine yaache.

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: …hayo mapenzi yako na CCM yamekuja lini? Au kwa sababu Mbunge! Subiri kesho kutwa CCM wakuangushe halafu uanze kuimba imba huko. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba nia njema ndiyo itakayodumisha Muungano. Naomba niseme moja na katika hili naomba Mheshimiwa Jenista anisikilize vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa ya mazungumzo ambayo ipo sasa kwenda kutatua changamoto hizi za Muungano, baada ya muda hazitakuwepo tena na tutakuja kushuhudia mambo mengine ambayo hayastahili. Kwa sababu unapobana fursa za kiuchumi za Zanzibar, vizazi vinavyokuja havitakubali kuona kwamba wao hawa-enjoy fursa za kiuchumi kama zile ambazo wenzao Watanzania Bara wanazipata ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili hawatalikubali. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tutumie fursa ambayo ipo, tutumie nafasi ambayo sasa hivi tunayo ili kutatua changamoto hizi tukiwa na nia njema ya kwenda kwenye Muungano ambao utadumu na utadumisha usawa na haki kwa pande hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie mchango wangu kwa kusema kwamba, suala la mazingira Wizara hii bahati mbaya sana hakuna fedha ya ndani ambayo imetengwa katika kuendeleza suala la mazingira ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Fedha yote inayotegemewa ni ya misaada kutoka nje. Hii inadhihirisha au inaonyesha kwamba ni kiasi gani Serikali haiko serious na kuendeleza suala la mazingira katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wakati wa kupitisha bajeti na Waheshimiwa Mawaziri pamoja na Cabinet iwe serious na suala la mazingira kwa sababu ni muhimu na ni suala ambalo linagusa binadamu na viumbe vyote vilivyomo ndani ya Tanzania yetu. Bila mazingira sahihi na bila kudumisha mazingira, Taifa hili litatupotea na tutakuja kujutia nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)