Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii ya Waziri. Hata hivyo, ninayo machache ya kushauri; ni dhahiri bila kutunza mazingira nchi yetu itapata matatizo mengi na makubwa. Mkoa wa Kigoma na hasa Halmashauri ya Mji Kasulu ulibahatika kutembelewa na timu ya wataalam wa mazingira na vyanzo vya maji. Timu hii ilimaliza kazi na kutoa ripoti yake mwaka 2017. Kazi kubwa iliyofanyika ni pamoja na kutembelea vyanzo vya maji vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu. Vyanzo kadhaa vilifanyiwa tathmini na utafiti wa kina baada ya taarifa ile ya kitaalam niliamini kwamba hatua za utekelezaji zimechukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hotuba yako ya Bajeti 2019/2020, ukurasa wa 83 (xi) kwamba moja ya kazi zitakazotekelezwa mwaka huu ni kupitia miradi iliyowasilishwa na wadau ili ipate wafadhili wa Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Je mradi wa ulinzi wa vyanzo vya maji zaidi ya 25 katikaHalimashauri ya Kasulu Mjini ni sehemu ya mkakati huu? Naomba Wizara yako ifahamu kwamba maji yanayotiririka kutoka uwanda wa juu wa Heru Juu, Buhigwe maji hayo hatimaye hutiririka hadi Ziwa Tanganyika. Ulinzi wa vyanzo hivi si tu kwamba ni muhimu ni jambo la lazima, tafadhali hatua sasa zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa ardhi oevu ya Malagarasi; eneo hili maarufu Malagarasi wetland linahitaji kulindwa. Eneo hili kwa kiasi kikubwa linakumbwa na uvamizi wa ng’ombe wengi kutoka baadhi ya maeneo ya nchi yetu na wakati fulani nchi jirani. Eneo hili la Ramsar Site litapotea, urithi wetu utapotea na rasilimali hii itaangamia pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Wizara ya Maliasili na Utalii, TAMISEMI, Mambo ya Ndani na Wizara hii waje na mpango mkakati wa kulinda eneo hili, lisipolindwa ndani ya miaka mitano mpaka saba shida itakuwa haiwezi kurekebishika tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatakie Wizara hii kazi njema katika kulinda mazingira ambayo ni uhai wa Taifa letu.