Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi ni suala mtambuka na siyo tu linaathiri sekta moja. Ili kukabiliana na suala hili, nguvu toka pande zote inatakiwa kutumika. Ofisi ya Waziri Mkuu, Fungu 37, miradi inayohusu kujiandaa kwa majanga na mabadiliko ya tabianchi haikupata hata senti moja. Kwa maana hii, nchi yetu ya Tanzania hatuoni kama hili ni tatizo na kama tunaona ni tatizo kwa nini basi tusione ni wakati kama Taifa kuyalinda mambo ya mazingira kwa kutumia fedha zetu ili kuondokana na tatizo la ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchafuzi wa mazingira kutokana na taka ngumu ni changamoto katika maeneo ya mijini kutokana na uwezo mdogo wa Mamlaka za Serikali za Mtaa na miundombinu hafifu ya usimamizi wa taka za aina hii hasa mifuko ya plastiki au rambo. Nchi yetu Tanzania ina Kiwanda cha Karatasi Nyororo Mkoani Iringa, Wilaya ya Mufindi, kinatoa karatasi za kiwango cha juu ambazo zinasafirishwa nchi jirani. Kwa nini Serikali isichukue maamuzi magumu kuwekeza katika utengenezaji wa mifuko ya kaki katika kiwanda hicho na kwa kufanya hivyo mapato ya Serikali yataongezeka, wakati huo matumizi ya mifuko ya plastiki itakoma na hali ya mazingira itakuwa salama. Ni mipango ambayo kama nchi hatupaswi kulialia, hapa ni uamuzi mgumu ambao unatakiwa kufanyika kulinusuru Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sheria ya utunzaji wa vyanzo vya maji ambayo inaelekeza shughuli za kibinadamu zisifanyike kandokando na mito, nashauri sheria hii isimamiwe kwa umakini kwani kuna maeneo mengine wanaambiwa wafanye shughuli zao ndani ya mita 60 na maeneo mengine mita 100. Nashauri watu wote waelekezwe umbali ufanane kama ni mita 60 au mita 100, kauli iwe moja tu kwa kuwa nchi ni moja na watu ni wamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukauka kwa Mto Ruaha Mkoani Iringa kunasababishwa na wakulima wa mpunga Mbarali ambao baada ya kumwagilia mashamba yao wanaacha maji yanatiririka ambapo kungekuwa na usiamamizi mkali wa kuhakikisha kila mwenye shamba baada ya kumaliza kumwagilia maji wanayarudisha kwenye mto. Kadri Mto Ruaha Mkuu unavyozidi kukauka wanyama wa Mbuga ya Ruaha, Mkoani Iringa watahama na mbuga hii ndiyo mbuga kubwa kuliko mbuga zote Tanzania. Nini kauli ya Serikali kuhusu hatma ya mbuga hiyo? Nataka kauli ya Serikali wakati wa kuhitimisha.