Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii na naanza kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na kumpongeza mtoa hoja Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri. Nianze kuchangia hotuba hii kwa kurejea kitabu cha hotuba ukurasa wa 50 juu ya mkataba wa Nairobi kuhusu hifadhi, usimamizi na uendelezaji wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi. Mkataba huu unataka kuhakikisha tunalinda na kupambana na uchafuzi wa mazingira ya bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zinaonesha ifikapo mwaka 2035 eneo la pwani ya bahari ya Tanzania litakuwa na mifuko mingi ya plastiki na takataka nyingine kuliko samaki baharini. Nashukuru sana tamko la Mheshimiwa Waziri Mkuu na leo Mheshimiwa Waziri wa Mazingira kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. Hatua hii imekuja wakati muafaka kwani hali ya mazingira ya pwani yetu ni mbaya na inaathiri wananchi hususani sisi tunaoishi kwenye visiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni matumizi ya mkaa, kama lilivyoelezwa kwa uzuri kwenye kitabu cha hotuba ukurasa wa 29, kasi ya ukataji miti kwa uchomaji wa mkaa imekuwa ikiongezeka siku hata siku. Nashauri bei ya gesi ipungue ili wananchi waweze kuacha matumizi ya mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandaji wa miti kama lilivyojadiliwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 37 ni jambo jema. Naishauri Serikali yangu iongeze fedha kwenye kampeni za upandaji miti. Ni ukweli usio na shaka kasi ya ukataji miti imekuwa kubwa sana hivyo ipo haja ya kuongeza fedha kwa ajili ya kampeni za upandaji miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuharibika kwa ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu kama lilivyoelezwa kwenye kitabu cha hotuba ukurasa wa 50. Ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu ndiyo inayotiririsha maji kwenye Mto Rufiji na hatimaye maji hayo ndiyo tegemeo kwenye uzalishaji wa umeme kwenye mradi wa Rufiji Hydro Project. Kwa msingi huu, ni muhimu ikolojia hii kutunzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.