Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa Naibu Waziri, viongozi wote katika ofisi kwa hotuba yao nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze Mheshimiwa Waziri kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya nylon ifikapo tarehe 1/6/2019. Kimsingi jambo hili limekuwa ni kubwa kuliko faida ya mapato ya kodi ambayo Serikali imekuwa ikipata kutoka kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uamuzi huu mkubwa wenye manufaa mapana kwa Taifa, binafsi naona kama taarifa ya sitisho la matumizi ya mifuko hii halijatangazwa sana. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri akisema kwamba wamekaa na wadau wa mifuko hii kwa muda mrefu, lakini naamini kutokana na uamuzi huu mzuri wa Serikali, nina ushauri kwamba ofisi yako kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kupitia Watendaji mbalimbali Serikalini hususan katika Halmashauri zetu, nao wawe sehemu ya kusambaza katazo hili kwa sababu siyo wananchi wote wanatazama TVs, wanasikiliza Redio na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani itakuwa ni busara sana kuhakikisha wafanyabiashara wa kada zote pamoja na watumiaji wanapata taarifa hii kwani ni takribani miezi miwili tu imebaki kufikia mwisho wa matumizi ya mifuko ya plasitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha katazo hili muhimu, Mheshimiwa Waziri amesema katika hotuba yake kwamba, baadhi ya bidhaa zitaendelea kutumia mifuko ya nylon, kama vifungashio vya dawa na kadhalika. Nadhani kwa umuhimu siku za usoni kuhakikisha matumizi yote ya plasitiki au nylon yanapigwa kabisa marufuku kwa kuzingatia athari za mazingira na hata uzalishaji wa mazao umepungua kwa sababu ya ardhi imeathirika kwa matumizi ya mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa za ofisi yako kwa namna inavyokabiliana na uharibifu wa mazingira hususan ukataji wa miti ovyo. Naiomba ofisi yako pia itoe katazo la wananchi wote kulima kwenye milima. Kama ambavyo katazo la kufanya shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji, pia kulima kwenye milima kumekuwa na athari za kuleta mabadilikoo ya tabia nchi hususan kwa mvua kupungua, pia tumeshuhudia kuona vyanzo vyote vya maji vinachafuliwa na maji ya mvua yanayochanganyika na udongo kutoka milimani. Naiomba sana Serikali itazame katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la mazingira ni suala mtambuka, napongeza maelezo ya Mheshimiwa Waziri kusema Halmashauri zetu zina wajibu mkubwa wa kusimamia suala la mazingira. Swali hapa ni je, Halmashauri zetu zina watumishi wa kutosha kusimamia mazingira? Je, Serikali inajipangaje kuhakikisha Halmashauri zinapeleka watumishi wenye elimu na weledi wa kutosha juu ya mazingira? Ni vyema tukajipanga katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.