Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza leo, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua na kuendelea kuniamini kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumshukuru Makamu wa Rais, Mama yetu, Mama Samia Suluhu kwa maelekezo na ushauri mzuri ambao amekuwa akiutoa kwenye Wizara na tumekuwa tukiufanyiakazi. Nichukue fursa hii pia kumshukuru Waziri Mkuu wa ushauri ambao ameendelea kutupatia. Nimshukuru pia Waziri wangu Mheshimiwa Januari, amekuwa ni mstari wa mbele sana kunipa mwongozo mzuri wa kuhakikisha natekeleza majukumu yangu, nimshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote katika Wizara yetu, tumefanya kazi kwa pamoja vizuri na hatimaye tunaendelea vuzuri. Vile vile nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote, Mwenyekiti na Wenyeviti wengine kwa kazi kubwa ambayo tumeendelea kuifanya kwa pamoja. Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, niwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Singida Mjini, wamekuwa wavumilivu kwa kipindi chote ambacho nikitekeleza majukumu ya Serikali. Mwisho kabisa niwashukuru pia Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira wametupa ushirikiano mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na wengine wamechangia kwa maandishi, lakini nijikite kwenye maeneo machache hasa yahusuyo mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia hotuba ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa 10 wamegusia suala la Stiegler’s Gorge kwamba misitu inafyekwa sawa na ukubwa wa Dar es Salaam nzima. Jambo hili likisemwa hivi kwa Watanzania linaweza kuleta sura tofauti. Mtanzania anayeifahamu Dar es Salaam anaweza akaona eneo lile linalokatwa miti litabaki kuwa jangwa, lakini ni wajibu wetu sasa kufika mahali kueleza faida ya ule mradi wa Stiegler’s Gorge ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mbuga ya Selou ina kilometa za mraba zaidi ya 50,000 lakini ni asilimia tatu tu ambapo ule mradi unaotarajiwa kujengwa na umekwishaanza ndiyo zitatumika kwa ajili ya kuhakikisha tunapata umeme wa megawatts 2,100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunahitaji umeme na tunahitaji umeme rafiki wa mazingira. Sisi ambao tuko kwenye eneo hili la mazingira, huu umeme kwetu ndiyo umeme rafiki wa mazingira kuliko umeme wa mafuta. Kama umewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakizungumza kwenye bajeti iliyopita ya TAMISEMI wanataka umeme wa REA na mambo mengine yote, lakini umeme ule wanaouhitaji wanahitaji wapate umeme rafiki na hapa nilitarajia na mimi kuona Waheshimiwa Wabunge kwanza wanampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na hatua kubwa ya ujasiri ya kuhakikisha kwanza tunapata umeme rafiki wa mazingira ambao tunapata megawatts 2,100. Eneo hili linahitaji ushirikiano wa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini faida kubwa sana tunaipata. Unapozungumzia tu ile miti ambayo sisi hatukati asilimia 3, ile miti ni kama 1.8 lakini faida ya ule umeme ni kubwa kwa nchi nzima na duniani. Wamezungumzia habari ya mabadiliko ya tabianchi kwamba tuwe na umeme rafiki lakini leo wananchi wetu wanawekewa umeme ama umeme unaofika vijijini unahitaji kuwa wa gharama nafuu ambapo ni lazima tuwe na umeme unaotokana na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la umeme kumekuwa na mambo mengi watu wanayaeleza lakini wanaeleza kwenye eneo la kukata misitu lakini waeleze faida ya kile kinachopatikana pale. Mbali ya faida ya ule mradi kwenye umeme pia kuna ajira, kilimo, ufugaji na mambo mengi ambayo tunahitaji tushirikiane na wenzetu kwa ajili ya kuhakikisha kwanza tunaweza kupata umeme huu ambao utatusaidia kufikia malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mengine wenzetu wamejaribu kuzungumzia lakini nieleze jambo moja kwenye eneo la taka ngumu na taka hatarishi, wakati nafanya ziara kwenye Mikoa sita ya Nyanda za Juu Kusini moja ya hoja ilikuwa ni hiyo ya vyanzo vya maji lakini nyingine ya taka. Vyanzo vya maji Mto Rufiji wenyewe unaunganishwa ama unalishwa na mito mikuu mitatu: Mto Rwengu, Mto Kilombero na Mto Ruaha Mkuu. Nimeenda kuangalia vyanzo vya maji na namna vinavyohifadhiwa, nataka niwahakikishie Watanzania tunayo maji ya kutosha na Watanzania ni waadilifu wametunza vyanzo vya maji na tunahitaji kuendelea kuwapa elimu waendelee kutunza vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeangalia eneo la taka ngumu na taka hatarishi, Kamati yangu imelizungumza vizuri, moja ya eneo ambalo linaleta changamoto ya taka, nimemsikia Mheshimiwa Hawa Mwaifunga pia amezungumza eneo hili la taka, ni eneo ambalo ni vizuri kwa kweli tukashirikiana kwa pamoja. Nimeendelea kutoa elimu kwenye mikoa yote ambayo nimepitia, nimetembelea madampo na kuona namna ambavyo wanateketeza zile taka zinapotoka majumbani na kupelekwa kwenye madampo, eneo lile tumewaomba wenzetu wa Serikali za Mitaa walioko chini viongozi wale tunashirikiana kwa pamoja japo tunajaua kwenye Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2004, Ibara ya 6 kwamba jukumu la usafi ama la utunzaji wa mazingira ni la kila Mtanzania ama ni la kila mwananchi ambaye anaishi Tanzania. Eneo hili niwaombe Waheshimiwa Wabunge tushirikiane pamoja, suala la uhifadhi wa mazingira siyo la Wizara moja ama la Serikali peke yake ni suala la kila Mtanzania na kila kiongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Genzabuke amezungumza vizuri na niseme tu kwamba tumepokea ushauri wake juu ya kushirikiana na wenzetu hasa mashirika yale yanayo-deal na wakimbizi. Nimefika mpaka Kagera Nkanda nimeona uharibifu mkubwa wa miti na maeneo mengine. Nimuahidi Mheshimiwa Genzabuke jambo hili tumelipokea na tutalifanyia kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mtolea nikuahidi tu kwamba baada ya Bunge hili nadhani nitakapokwenda Jimboni sasa niwasalimie wananchi wangu, nitakwenda kufanya ziara Dar es Salaam. Jambo kubwa hapa siyo tu kutoza faini na hili tuliweke wazi, kwanza tunahitaji watu wale wapewe elimu. Kwa sababu kama Watanzania kwenye gereji na maeneo mengine hawajapewa elimu na tukakimbilia faini, hili kwa kweli hatutakubaliana nalo. Nikuahidi kwamba nitafika mwenyewe nifanye ziara na pia tuwashirikishe wananchi ambao wameamua kuwa wajasiliamali kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza suala la elimu, kwa kweli tunakubaliana nalo, suala la elimu halina mwisho hata kama tunaendelea kutoa inawezekana bado elimu inahitajika sana. Nimshukuru sana Mheshimiwa Saada Mkuya amesema elimu ya Muungano inayotakiwa sasa ianzie Bungeni. Hili tunakuunga mkono, tutaanza nalo, najua Mheshimiwa Waziri ataeleza vizuri suala la Muungano.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la elimu ni jambo kubwa sana na siyo jambo la Wizara au Serikali peke yake, kila Mtanzania anayeelewa juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira anapaswa kuwaelimisha na wengine. Pia anayejua umuhimu wa Muungano anapaswa kuwaelimisha na wengine. Sisi tutakuwa mstari wa mbele, tutaendelea na majukumu na mikakati yetu ya kuhakikisha kwamba elimu hii inatolewa kadri inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kuendelea kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kadri ambavyo wametupongeza waendelee kutupa ushirikiano wa dhati na sisi kama ambavyo mnafahamu tunafikika na tuko tayari kufanya kazi wakati wote. Pale tunapobanwa mtuwie radhi inawezekana tusifike kwa wakati lakini tunaweza kushauriana na kusaidiana, majukumu haya yote ni yetu pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nichukue fursa hii kuishukuru sana familia yangu, mke wangu na watoto ambao nao wamenivumilia kwa kipindi chote hiki nimeendelea kutekeleza majukumu yangu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)