Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kabla ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri, Katibu Mkuu na Majaji wote wanaotoa haki katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianzie hapa, Mheshimiwa Balozi kabla hujateuliwa kuwa Waziri katika eneo hilo alikuwepo Waziri mmoja anaitwa Mheshimiwa Kabudi. Mheshimiwa Kabudi nilimuuliza kuhusu Mahakama ya Wilaya ya Misenyi. Wilaya ya Misenyi ina miaka zaidi ya 25, ipo boarder na ina kesi nyingi, nikaambiwa bajeti inayokuja Misenyi itakuwepo, kitabu chako hakina Misenyi. Mahakama ya Wilaya haionekani ndani ya kitabu hiki. Sitaki kusema sana Mwanasheria na Waziri tukitoka tuongee kidogo ili mjue utaratibu mtaufanyaje wa Mahakama ya Wilaya ya Misenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Mahakimu wetu wa Mahakama za Mwanzo. Ni kweli tunajenga Mahakama za Mwanzo, tunarekebisha na kadhalika lakini haki inaanzia chini, hawa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo maisha yao mnayajua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Mahakimu wetu wa Mahakama za Mwanzo. Ni kweli tunajenga Mahakama za Mwanzo, tunarekebisha, tunafanya nini, lakini haki inaanzia chini. Hawa Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo maisha yao mnayajua; ambao wanaanza na kesi ili mtu akate rufaa mpaka Mahakama Kuu, mazingira waliyonayo mnayaona?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, hebu nafasi, wapeni haki ili haki itendeke na watu waweze kuona kwamba haki inaonekana. Maisha yao jamani yanatisha. Sitaki kuingia sana kwa undani lakini naomba Mheshimiwa Waziri pale alipo, hebu akakae na Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo aone wanaishije na wanafananaje ili haki ipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni wasaidizi wa Majaji. Hawa nao wana haki sawa na Mahakimu. Hivi hawa stahili zao ni zipi jamani? Ndio wanamsaidia Jaji kuandaa, kuandika na kadhalika. Hali zao ni dhofulhali, samahani nitumie kauli hiyo. Hebu wapeni value na wao, maana wakitoka pale mnawateua kuwapa nafasi za juu, lakini kazi zao ni ngumu na maisha yao ni magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu cha bajeti humu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika bajeti ya maendeleo haina hata shilingi, lakini ofisi hii ndiyo inafanya kesi zote za nje, ndiyo inasafiri, tunaenda kushindwa. Kuna nini hapa? Kesi za Kimataifa ziko kwenye ofisi yake, hamkumpa hela ya maendeleo hata shilingi moja, atafanyaje kazi? Au tumemaliza kesi za Kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuna Mahakama kama za rafiki zangu akina Mheshimiwa Bashe hawa. Wamejenga wenyewe, wamejenga maboma, wanatakiwa kumaliziwa, kwa nini msingekuwa mnaenda kwa hawa watu ambao wameshaturahisishia kazi ili wakapata huduma hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nampongeza Mheshimiwa Waziri, najua ameingia hivi karibuni bado ana siku chache, lakini hayo machache yanamtosha. Mwakani tutakuwa na mengi sana ya kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.