Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema, ametujalia na leo tumeiona siku yetu ya Ijumaa, basi azidi kutupa heri na baraka na atuongoze kwa kila jambo lilokuwa na heri na sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbele yetu kuna hoja inayohusu viwanda. Viwanda tunavyovizungumzia tunataka vituletee mabadiliko ambayo tayari Watanzania tulianza kuwanayo katika miaka ya nyuma. Kwenye miaka ya 1970 tulikuwa na viwanda vingi kwenye maeneo mbalimbali. Msimamizi mkuu katika shughuli hizo za viwanda ilikuwa ni NDC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapozungumzia uchumi wa viwanda, nasi Watanzania tuko tayari, tumesema tutaupokea uchumi wa viwanda. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri aliyotuwasilishia; ameyataja maeneo mbalimbali ya Tanzania kwamba tutapata viwanda ikiwemo Mkoa wa Pwani ninakotoka mimi. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kwanza atufufulie viwanda ambavyo vilikuwepo na vimekufa. Viliuzwa kwa watu, iweje mpaka leo hakuna kitu chochote ambacho kimeendelezwa au kimefanyika katika viwanda hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hotuba yake ameelezea kwamba kutakuwa na utaratibu wa viwanda ambapo wenye viwanda watashirikiana na wananchi waliokuwepo katika maeneo yale kwa maana ya kuwa wakulima watakaotumia maeneo yale kwa kilimo na vile viwanda vitatumia mazao yale kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai au ushauri kwake, sasa hivi tumeona kuna viwanda vingi nchini, ikiwemo Mkuranga na Bagamoyo, lakini kwa nini jambo hili la kuchukua wakulima wadogo wadogo wanaozalisha mazao yao wasianze sasa hivi tukaona mfano? Hata sisi Wabunge tutakapokuwa tunazungumzia suala la kuhimiza na kushawishi watu kuja kutengeneza viwanda kwa maeneo yetu, tuwe na mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Arusha kuna maeneo wanazalisha maua, lakini pia kuna wakulima wadogo wadogo ambao wanazalisha yale maua, yanauzwa kwenye viwanda, wao wanasaidia zile mbegu na dawa za kuzuia uharibifu wa mazao kwa maana ya maua. Kwa hiyo, naomba na huku kwetu uwezekano wa wakulima wadogo wadogo waweze kununuliwa mazao yao kwa sababu Mkoa wa Pwani, mfano, tuna machungwa mengi, maembe mengi, na matunda ya aina mbalimbali. (Makofi)
Mhshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuthibitisha hilo, msimu wa matunda pita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani uone mazao yanavyoharibika kwa sababu hakuna pa kuyapeleka. Mkulima hasa mwanamke; asilimia 80 ya wanawake ni wakulima wadogo wadogo. Naomba basi uwezekano Serikali kufikiria ni vipi watakwenda kununua mazao hayo kwa wakulima kuwawezesha na wao wainue kipato chao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapozungumzia viwanda, nilizungunguzia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Kwenye viwanda vyetu vilivyokuwepo sasa hivi nchini, vijana wetu wanatumika vibaya sana. Wao wanaajiriwa kwa mshahara mdogo sana, wakati sisi tunatarajia waajiriwe wapate fedha zitakazowaendesha katika maisha yao, lakini kinyume chake wanapewa mshahara wa shilingi 150,000 kwa mwezi. Shilingi 150,000 kwa mwezi anaifanyia nini kijana yule, mama yule, dada yule, kaka yule? Naomba kama tunakwenda kwenye mtindo wa kuwa na viwanda vingi, basi hata mshahara uwekwe kabisa, aambiwe mwekezaji kwamba mshahara wa kima cha chini isiwe shilingi 5,000 kwa siku.
Mhehimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kama kutakuwa na uwezekano kwa Serikali yetu ichukue hata vile viwanda ambavyo vilikufa, vikawezeshwa na wakachukuliwa akina mama wakapewa kiwanda kile waendeshe wao. Wako ma-engineer, wako wataalam wa aina mbalimbali, iwe mfano wa kiwanda kile tuone uzalishaji utakotoka pale. Akina mama ni wachapakazi! Sisemi kama wanaume hawafanyi kazi, lakini nasema uchumi wa viwanda umkomboe na mwanamke katika viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema viwanda, tuangalie na mazao tunayoyalima katika maeneo yetu. Mkoa wa Pwani tunalima nyanya nyingi sana, lakini mwisho wa siku tunanunua nyanya za kopo, zinazotoka nje ya nchi, haipendezi! Tuwe na viwanda vyetu, tuwe na nyanya tunazotengeneza wenyewe, tuwe na matunda ya aina mbalimbali ambayo akina mama wanaweza wakatengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie na hotuba ya Wapinzani kwenye ukurasa kama sikukosea ni wa 16, waligusia ahadi ya Mheshimiwa Rais, kwamba aliahidi atajenga kiwanda cha Korosho, Mkuranga na Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie neno moja tu, Waswahili wana msemo wao wanasema hivi, tena hata waimbaji waliimba, “mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waje waone wenyewe.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi toka imetolewa hata miezi sita haijakamilika. Subirini muone kazi itakavyokwenda. Nawaomba himizeni wapiga kura wenu, wananchi wetu, wasimamie uzalishaji wa korosho, wasimamie uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali ili tuweze kuhakikisha viwanda vyetu vitakuwa na malighafi, inayotoka ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nasema ahsante sana. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwa ajenda yake ya uchumi wa viwanda. Watanzania na hasa akina mama, tumesimama imara, tutaifanya kazi katika viwanda vitakavyoletwa. Ahsante sana.