Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Ulimwengu na vilivyomo ndani yake tukiwemo sisi wanadamu. Aidha, napenda tujue kwamba Allah ana sheria zake ambazo tunapaswa tuzitii na kuzifuata. Vilevile na sisi binadamu tumeandaa sheria zetu na kanuni ili kuzifuata na kuzitii ambazo ni sheria za nchi husika zinazotutaka kila raia kuzifuata na hakuna mtu aliye juu ya sheria. Kwa maana nyingine, ndiyo tukatengeneza Katiba ambayo ni Sheria Mama ya nchi yetu Tanzania. Ndiyo maana Bunge na Wabunge wako hapa kuilinda Katiba na hata Kiongozi wa nchi naye huapa kuilinda Katiba hii hii, kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo Wizara nyeti na Wizara ambayo husimamia majukumu ya Katiba, Sheria, Kanuni na utaratibu zilizowekwa na vyombo halali vya maamuzi. Baada ya kutoa ufafanuzi huo, ama utangulizi huu napenda kutoa maoni yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na upotoshaji na uvunjifu wa Sheria na Katiba yetu kwa wananchi na viongozi wa nchi na kuwa juu ya sheria, jambo ambalo siyo zuri na ni baya sana na litapelekea uchafuzi wa demokrasia na amani ya nchi, kwa sababu kuna ambao wako juu ya sheria na kuna ambao wako chini ya sheria; jambo ambalo ni baya sana na nalipinga kwa nguvu zote na naomba Bunge lako lipinge na Wizara husika itoe kauli na kupinga vikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambacho Taifa hili linapitia katika changamoto na ugumu mkubwa ni kipindi hiki. Kumekuwa na changamoto ya kutoheshimu utawala bora wa sheria; ni kipindi ambacho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria mbalimbali za nchi na Kanuni zote hazifuatwi, badala yake kuvunjwa sheria kwa makusudi. Kwa hiyo, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo Wizara yenye jukumu la kuhakikisha kuwa nchi hii inaongozwa kwa kuzingatia Katiba ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na msisitizo huu kuwekwa kwenye maneno ya utangulizi (Preamble) ya Katiba yetu, tangu mwishoni mwa mwaka 2014 mpaka leo, ninapotoa maoni yangu, nchi yetu imekuwa ikipitia katika kipindi kigumu cha janga la Kikatiba ambapo Serikali ya CCM haisimamii misingi ya Katiba ya mwaka 1977 wala haina mpango wowote madhubuti wa kurejesha mchakato wa Katiba pendekezwa ya Jaji Warioba ya mwaka 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inathibitishwa na kauli ya Mheshimiwa Rais kuwa hajawahi kuahidi kuhusu Katiba Mpya na wala haikuwa sehemu ya ahadi zake za Kampeni kauli inayokinzana na Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo katika ukurasa wake wa 206 – 207 kipengele cha 145(e) inasema “ Ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2015 – 2020, CCM itahakikisha kuwa Serikali inatekeleza yafuatayo: (e) Kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.” Mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo leo hii Serikali ya Chama cha Mapinduzi inakana Ilani yake iliyoinadi kwenye uchaguzi na badala yake inaikanyaga Katiba kupitia viongozi wake. Huko ni kuvunja uaminifu na maadili ya Chama na Serikali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na uvunjifu wa sheria na ukiukaji wa Katiba na Utawala Bora kwa mambo ambayo yanaendelea kujitokeza katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Kuna ushahidi wa kimazingira unayoonesha baadhi ya uteuzi kufanyika kwa fadhila baada ya wahusika kufanya vitendo vya kuwanyima haki watu wengine kwa lengo la kutekeleza matakwa ya utawala. Mfano, uteuzi wa Hakimu mmoja kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa Jaji wa Mahakama ya Tanzania, ni miongoni mwa teuzi ambazo zinaonesha ushahidi wa kimazingira kwamba ni fadhila kwake baada ya Hakimu huyo kufuta dhamana ya Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe, pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uteuzi wa Jaji ulikuwa ni fadhila kwake baada ya kutekeleza hila au kile ambacho alielekezwa na mamlaka zilizomtuma ama kujipendekeza. Hali hii haikubaliki kwenye nchi ambayo inasimamia vizuri Demokrasia, Sheria, Kanuni na Utaratibu tuliojiwekea katika Katiba ambayo tuliahidi kuilinda na kuifuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, narudia kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria. Kwa hiyo, ni wakati wa kutenda haki na kusimamia Utawala Bora wa Sheria na kutimiza ahadi zetu tulizoweka mbele ya Mungu kwa kiapo.