Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu wa shukrani za dhati kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wake kwa kuridhia na kuanzisha ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Mtae - Mlalo, Lushoto. Hii ni hatua muhimu kwa ujenzi na utoaji wa haki katika Mhimili huu. Nafarijika sana kuona jambo hili limekamilika na sasa ujenzi upo katika hatua za upauzi na usafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahakama hii itahudumia kata sita za Tarafa ya Mtae na kata za jirani na itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kukosa sehemu sahihi za kutafsiri haki katika ngazi hii ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kutoka katika Idara ya Mahakama kupitia Chuo cha Sheria Lushoto tuweze kupata msaada wa kisheria katika maeneo yetu ya uwakilishi. Tunaamini hili litasaidia sana katika kuwapa uwezo vijana wetu wanaosoma katika chuo hiki, lakini pia kuwasaidia wananchi kwenye mashauri mbalimbali katika maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Law School; kumekuwa na uhitaji mkubwa wa wanafunzi waliomaliza katika vyuo mbalimbali vya hapa nchini katika Shahada ya Sheria, hata hivyo, linapokuja suala la kupata ujuzi wa elimu ya Uwakili Chuo pekee kinachotoa taaluma hii ni University of Dar es Salaam. Tunaomba Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuona namna bora ya kuweza kupanua wigo ili Taaluma hii ya Uwakili iweze kupatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho la ushauri ni kuhusu azma ya mahakama kutaka kujenga mahakama kila kata ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba kushauri jambo hili lipitiwe upya na lifanyiwe utafii wa kina kwani kwa maoni yangu kushusha mhimili wa Mahakama katika ngazi ya kata itakuwa ni mzigo na gharama kubwa kwa mhimili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, napendekeza kwamba ni bora mahakama hizi zikaishia katika ngazi ya tarafa. Yapo maeneo ikiwemo Lushoto eneo la tarafa ni rafiki kufikika kwa urahisi hivyo kutokuwa na uhitaji wa kuweka mahakama katika ngazi ya kila kata. Tunazo tarafa tano zinazounda Halmashauri ya Lushoto, hivyo ni vyema angalau kila tarafa ikapata Mahakama ya Mwanzo ili kuleta ufanisi katika kutafsiri sheria na kutoa haki. Katika Halmashauri ya Bumbuli, Lushoto kwenyewe zipo tarafa tatu lakini kuna Mahakama ya Soni na Bumbuli pekee, Tarafa ya Tamota na Mgwashi hazina mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kupongeza mhimili huu wa Mahakama lakini pia Viongozi Watendaji Wakuu wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa utendaji wao na kuipa heshima Wizara hii, hasa katika eneo hili la usimamizi na utoaji wa haki. Nawasilisha.