Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba iende kwenye rekodi pia, hata kukata hotuba za upinzani ni shambulio dhidi ya uhuru wa habari. Ni kuwazuia wananchi kupata mawazo mbadala yanayotoka upande mwingine. Hii inatuharibu sana kama Taifa. Jana nilikuwa naangalia kipindi cha The Stream kwenye Al-jazeera, topic ilikuwa uhuru wa habari na demokrasia Tanzania. Dunia imeanza kutumulika na tunatia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee ku-stress kwamba, kigezo cha kuwa na magazeti sijui 200 plus, kwamba ni uhuru wa habari, hiyo si hoja ni hoja mfu, kwa sababu hatutaki quality tunataka quantity. Haina maana kuwa na magazeti 216 ambayo waziri au Dkt. Abbasi anaweza akaamuka tu asubuhi kwa strike ya pen au penseli akayafuta yote kwa dakika moja tukawa tuko tumerudi kwenye zero. (Makofi)

Kwa hiyo, tatizo la uhuru wa habari katika hii nchi, ni very serious…

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Antony Komu.

T A A R I F A

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa msemaji kwamba ni kweli kuwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari si kigezo peke yake cha kuwa na uhuru wa habari. Hii ni kwa sababu hata kule Zaire wakati Mobutu anatawala na dunia nzima ikipiga kelele kwamba hakuna demokrasia na uhuru wa habari kulikuwa na vyama vingi vya siasa vikifika 400 kuliko mahali pengine popote duniani. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea na ni hatari sana kwa sababu mambo kama haya angalia Zaire walivyofanya na mwisho wao na sasa hivi angalia Sudan na mwisho wa Al-Bashir…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Nakuambia vile. Jana Ali Bashir amehamishwa kutoka house arrest alipokuwa amezuiwa amepelekwa kwenye gereza kuu la Khartoum ambako alikuwa anawafunga wapinzani wa kisiasa. Leaders beware. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana niwapongeze sana MCT, LHRC na THRDC kwa hatua yao ya kupeleka Mahakamani baadhi ya vifungu vibovu vilivyopitishwa vya Sheria ya Habari ya mwaka 2016. Hawa walienda kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki na imetoa hukumu kwamba vifungu vile vinazuia haki ya watu kupata habari au vinazuia uhuru wa habari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tujiulize sisi Wabunge tunakaa humu ndani tunawawakilisha watu, tunatunga sheria inaenda inapingwa Mahakamani halafu inatupiliwa mbali si tunaonekana mapoyoyo. Tunatia aibu kimataifa kwa sababu nchi za East Africa zamani zilikuwa zinaiangalia Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya kidemokrasia na kadhalika, Mheshimiwa Kikwete alituweka vizuri sana lakini leo hii Mahakama za nje zinatengua, zinatuambia kwamba Bunge la Tanzania lilitunga sheria ya kukandamiza uhuru wa habari, hawalaumu hata Serikali, sasa hivi vitu ni vibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mashambulio haya yalianza toka Awamu ya Tano ilivyoingia. Shambulio la kwanza la uhuru wa habari lilikuwa ni kuzuia Bunge live, tena nakumbuka Naibu Spika ndiyo ulikuwa umekalia Kiti siku hiyo, nakumbuka vizuri sana. Sasa unazuia Bunge live kwamba watu wafanye kazi lakini leo Mkuu kila siku yuko kwenye TV asubuhi, mchana, jioni, usiku mbaya zaidi unakuta Wakuu wote wa Taasisi za…

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, kuna kanuni inavunjwa, Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu, ninazo Kanuni mbili ambazo Mheshimiwa Mbunge mchangiaji anakokwenda anakwenda kuzivunja. Kanuni ya kwanza ni Kanuni ya 53(8), inasema, Mbunge yeyote hataruhusiwa kufufua jambo lolote ambalo Bunge lilikwishakuliamulia katika Mkutano huu uliopo ama mikutano iliyokwishakupita. Hiyo ni kanuni ya kwanza ambapo anapoendelea kuzungumza na kuchangia Mheshimiwa Mbunge maamuzi yote ya Bunge live na taratibu nyingine zote zilishafanyiwa maamuzi kwenye mikutano iliyopita na jambo hili lilikwishaondolewa katika mijadala yetu kwa kuwa lilishafanyiwa maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Kanuni nyingine aidha wewe ulikaa kwenye Kiti ama hukukaa kwenye Kiti lakini Bunge lilishakwishafanya maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni nyingine tunaposhughulikia masuala ya utendaji kazi wa Mheshimiwa Rais, kwanza yanasimamiwa na Katiba kama Kiongozi Mkuu wa nchi inamlinda kufanya kazi kwa sheria ambazo zinatumika kusimamia utendaji kazi na mwenendo wa Rais. Kwa hiyo, suala la kujadili mwenendo wa shughuli Rais kwa mujibu wa Katiba, hata akitaka kuwa na TV, akitaka kutangazwa saa 24, hili siyo suala la Bunge ni la Kikatiba na la mhimili wa Urais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye Kanuni yetu ya 64(1)(e) inatukataza pia kuzungumzia mwenendo na utendaji kazi wa viongozi wanaotoa maamuzi na mwenendo hasa wa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, kama mchangiaji ana hoja kuhusu vyombo na uhuru wa habari, uhuru wa habari huo usimwingize Mheshimiwa Rais katika utendaji wake wa kazi kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa Kanuni tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nirudi kusema Kanuni ya 53(8) ni lazima Waheshimiwa Wabunge yale ambayo yalikwishakufanyiwa maamuzi hayatakiwi kuwa tena ni part ya mjadala mpya ndani ya Bunge letu.

Mheshmiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Jenista akiomba kuhusu utaratibu wa Kiti kwa Kanuni ambazo amezirejea kwamba zilikuwa zinavunjwa. Ameanza na Kanuni ya 53(8) inayozungumzia kuhusu jambo ambalo lilikwishaamuliwa na Bunge katika mikutano iliyokwisha ama katika mkutano huo unaohusika. Pia ametupeleka kwenye Kanuni ya 64(1)(e) inayokataza kuzungumzia mwenendo wa Rais.

Waheshimiwa Wabunge, sikusudii kurejea kwenye mchango wa Mheshimiwa Mbilinyi na ambao Mheshimiwa Jenista ameona kwamba unazigusa hizi Kanuni mbili. Huwa siku zote tunakumbushana kufuata utaratibu ule ambao tumejiwekea wenyewe kwa ajili ya majadiliano humu ndani.

Waheshimiwa Wabunge, Kanuni ya 53 inakataza kuzungumzia jambo ambalo lilikuwa limekwishaamuliwa isipokuwa kama unaleta hoja mahsusi ili Bunge liweze kuliangalia upya jambo ambalo liliamuliwa. Jambo ambalo kwa sasa hivi hakuna hoja inayozungumzia Bunge kuliangalia upya jambo ambalo lilikwishaamuliwa. Nadhani kwenye hilo linazungumzia maelezo ya Mheshimiwa Mbilinyi kuhusu uamuzi si hata wa Bunge, uamuzi wa Serikali kutokuonesha tena moja kwa moja mijadala inayoendelea Bungeni.

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, kama Bunge lilihojiwa kuhusu jambo hilo ilikuwa ni hoja ambayo ililetwa ili Bunge lifanye maamuzi. Kwa sababu ililishapita ni vizuri kuzingatia masharti ya Kanuni zetu. Kama jambo hilo bado linaleta tabu miaka mitatu au minne baada ya uamuzi huo, Kanuni zetu zinatoa fursa kwa Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ama mtu mwingine yeyote kufanya hivyo.

Waheshimiwa Wabunge, Kanuni ya 64 kuhusu mchango wa Mheshimiwa Mbilinyi pia ambao Mheshimiwa Jenista ametupeleka kwenye fasili ya (1)(e) kutokuzungumzia mwenendo wa Rais. Ni vizuri kukumbushana kwamba Kanuni hii inazungumzia mambo yasiyoruhusiwa Bungeni na hilo ni mojawapo isipokuwa ikiwa hoja iliyoko Mezani imeletwa mahsusi kwa ajili ya kuzungumzia mwenendo wa Rais, jambo ambalo silo lililoko Mezani sasa. Kwa hiyo, niwaombe tuzingatie Kanuni zetu tulizojiwekea ili majadiliano yetu yawe yanaenda vizuri bila kukatisha kila wakati kwa kuvunja hizi Kanuni.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbilinyi utakuwa umepata mwongozo wa mambo haya yote mawili katika dakika zako zilizobaki uendelee kuchangia hoja iliyoko Mezani na siyo hoja ambayo kwanza ilifanyiwa maamuzi lakini pili usizungumzie mwenendo wa Rais ama mtu mwingine yeyote ambaye siyo hoja iliyoko mezani sasa. Mheshimiwa Mbilinyi.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachogundua watu wamejaa hofu na kujipendekeza, mimi hakuna sehemu hata tukienda kwenye Hansard nimesema Rais, nimesema Mkuu. Sasa haya ndiyo mambo tunayosema mnajiongeza mpaka mnaharibu mpaka Rais anawaambiwa kwamba Watanzania siyo wajinga kwa sababu hata hili watalifuatilia kwenye mitandao na watajua tofauti yangu na yenu katika hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia jambo mnaweza mkawa mmesema ninyi humu ndani kwamba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sugu, kwani Mkuu ni nani? Ni Mheshimiwa Mbowe?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizngumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Siyo nikija Mbeya tu hata sehemu nyingine lakini usiendeleze jambo ambalo nimekwishalitolea ufafanuzi hapa mbele. Malizia mchango wako ukiwa umeondoa hayo ambayo tumesema yanavunja Kanuni.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Katibu, dakika ngapi zimebaki nijue kabisa?

NAIBU SPIKA: Huwezi kumwongelesha Katibu Mheshimiwa Mbilinyi, wewe si ni Mbunge mzoevu, wewe mwenyewe umesimama kwa kuwa mimi nimekuruhusu ili uzungumze. Unapomuuliza Katibu yeye anazungumza humu ndani? Mheshimiwa Mbilinyi, tafadhali.

MBUNGE FULANI: Maliziamalizia Jimbo la Mbeya linaondoka hilo.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua mimi nawaambia, don’t go personal on me, I am just doing the job for this country. Tukiendelea hivi tunakubali kuingizwa kwenye giza, tutajikuta kama North Korea ambapo wameelekezwa mpaka namna ya kupiga makofi. Nchi nzima wanatakiwa kupiga makofi kwa inchi tatu, kutoka hapa kuja hapa, paa, paa, paa, sasa mnataka hili Taifa lifike huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajizuia kwenye kila eneo la uwazi, hebu angalia hivi ni sababu gani iliyofanya tujitoe OGP (Open Government Partnership), huu mkataba wa kimataifa? Mkataba huu unataka nchi wanachama kukuza uwazi katika uwajibikaji na utendaji wa Serikali. Serikali hii inajinasibu kwamba inapenda uwazi, inataka kila kitu kiwe wazi, kwa nini sasa tunajitoa katika vyombo ambavyo vinatu- endorse kwamba sisi ni watu ambao tunataka uwazi. Halafu tukisema mnatutafutia mbinu mbadala, mnatuvizia, matokeo yake mnaleta Taifa katika mtanziko mkubwa kwa kufanya mambo bila kushirikisha Wabunge kama mlivyofanya kwenye vitambulisho vya wajasiriamali. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mmekaa huko wenyewe, mmepeana vitambulisho, Mbeya Mjini mmeleta vitambulisho 45,000 wakati Wamachinga hawafiki hata 3,000. Watendaji wanalia kule na kwa sababu hawana uwazi hawawezi kutoka na kuitisha press kusema hiki kitu hakiwezekani wanalia chinichini, huku ndiko mnakolipeleka Taifa. Uhuru wa habari, uhuru wa kupata taarifa, uhuru wa kutoa taarifa hakuna, wanabaki kunong’ona tu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiriakwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi, muda wako umekwisha.

(Hapa Mhe. Joseph O. Mbilinyi aliendelea kuongea bila kutumia kipaza sauti)