Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe kwa hotuba yake nzuri na pia taarifa ya Kamati. Nimwambie Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wamefanya vizuri sana kwenye tasnia ya muziki. Watanzania wengi tunawaelewa na tunaamini mnawasimamia vizuri vijana na tunapata burudani za kutosha ikiwemo na hii aliyomaliza kuitoa msanii mkubwa nguli Sugu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitazungumzia sana kipande cha wasanii kwa sababu nimejaribu kumsikiliza Mheshimiwa Sugu kama msanii mkubwa nilitegemea atazungumza matatizo makubwa ya wasanii badala yake Mheshimiwa Sugu leo kageuka kuwa mwanasheria kuzungumzia mambo ya magazeti na vitu vingine.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, wasanii wa muziki kwa nini wanafanikiwa? Wanafanikiwa kwa sababu hawategemei kuuza filamu, wanapotoa nyimbo zao wanachokitegemea wao ni kufanya matamasha na kukodiwa na kuchukua viingilio. Ni lazima Wizara ione huruma kwenye tasnia ya filamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kuangalia kwenye kitabu hiki mipango ya Bodi ya Filamu siamini kama watu waliotengeneza hiki kitabu ni hawa wanaosimamia tasnia ya filamu. Tasnia ya filamu iko hoi bin taaban na ndiyo maana unakuta wasanii wetu wa Bongo Movie hawana kitu, sasa hivi wanategemea misiba wapate michango na kufungua madanguro na kuwa makuadi kwa wanaume. Wako hoi bin taaban, kwa nini? Tumeruhusu vitu vya kijinga ambavyo vimekuja kuuwa kabisa tasnia ya filamu na filamu ndiyo sehemu kubwa ambayo sisi Watanzania ilikuwa inatupa mafunzo ya utamaduni wetu wa kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kuna filamu inaitwa Sultan hakuna Mtanzania ambaye haiangalii na mbaya zaidi imetafsiriwa Kiswahili. Hivi ni nani anaweza kwenda kumuangalia Marehemu Majuto akaacha kwenda kuangalia Sultan? Tunapata faida gani kwenda kuzungumza mambo ya Waturuki tunaacha kukuza utamaduni wetu wa ndani? Hakuna Mtanzania anayeangalia Bongo Movie leo hayupo na hawa hawa watu wanaotafsiri Kiswahili ni wasanii wanatulipa nini kama Serikali? Kwa hiyo, nimwombe Waziri anusuru wasanii wa Tanzania wanamfia mikononi mwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ukitengeneza filamu ya Kibongo ina ukaguzi zaidi ya 1,000 lakini zikija filamu za Kikorea hakuna ukaguzi, nani atakayeenda kuangalia sinema ambayo mmewaambia Watanzania wavae madera na kanzu wakati filamu za Kikorea watu wamepiga miniskirt lazima watu wataenda kwenye miniskirt. Kwa hiyo, niombe sana kama tunaweka ukaguzi wa filamu lazima na filamu zinazotoka nje zikaguliwe ziendane na maadili yetu ya Kitanzania otherwise wasanii wetu wa Kitanzania wote tunaenda kuwapoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitengeneza filamu ya Tanzania unapoitoa inabidi ulipe kodi, mfano iwe shilingi milioni moja na mwakani lazima uilipie shilingi milioni 1, hii kitu siyo sawa. Filamu inaangaliwa mara moja inachuja lakini wewe unamweka kwenye library yako kumtoza shilingi milioni moja kila mwaka. Wasanii wetu wamekata tamaa na Mheshimiwa Waziri naomba sana uitumie kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba chukua maamuzi ya kusafisha hiyo Bodi ya Filamu, wametuulia filamu yetu ya Kibongo na ukitaka nikutajie hata majina ya wanaouwa nitakueleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako vinara Tanzania Bodi ya Filamu inawafahamu wako Kariakoo, hawa watu wanaleta makontena na makontena ya dublicate kazi za Watanzania. Hata Waziri unawafahamu ukitaka nikutajie kwa ruhusa yako nakutajia. Hawakamatiki, wanatengeneza dublicate ya kazi za Kitanzania wanazileta kama export wanazipeleka Kongo na Kenya. Ukifika Kongo leo filamu ya Tanzania inauzwashilingi 500, hivi ni nani atakayeweza kufanya kazi ya kutengeneza filamu hapa Tanzania? Makontena yanaingia kutoka Korea, China na wanaoyaleta wanafahamika. Hata wakikamatwa na hizo dublicate faini yake ni shilingi milioni tano, mtu ana mzigo wa bilioni kumi na makontena yake anarudishiwa. Ni nani atakayeangalia kazi za wasanii wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wewe unatokana na CCM hawa wasanii ni watu wakubwa sana kuanzia mwaka huu mwezi Novemba kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tutawatumia, mwakani tutawatumia, tusipowasaidia hawa wakipotea tutakuja kuchaguana watu wenye sauti nzuri humu tutageuka wasanii na kufurahisha kwenye majukwaa wakati wa uchaguzi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, mimi nalalamika na wewe na nakueleza vizuri kwamba shughulika na wasanii wa Bongo Movie wamepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukiingia Sinza madanguro makubwa yote ni ya wasanii. Ukitokea msiba, watu wanaokwenda kusimamia michango ni wasanii angalau wapige ganji wapate kitu. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, usiopochukua hatua kwenye hili, nami natarajia kuja kushika shilingi, uhakikishe kwamba unanifuata hapa tuongee unieleweshe vizuri vinginevyo nitalia na wewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yanayozungumzwa humu tunakoelekea yatatokea tu, kwa sababu hakuna cha kuzungumza. Sera ya Chama cha Upinzani ilikuwa ni kukosoa; na kweli walikuwa na sababu za msingi, mimi nilikuwa shabiki wao kuwaangalia. Walikuwa wanasema Tanzania hatuna ndege; haya mambo yametengenezwa yote. Sasa hawana cha kuzungumza. Mbunge anasimama anakwambia unaenda na ving’ora. Hiyo ndiyo kazi wamemtuma watu wa Mbeya, wala tusishangae, hakuna kitu cha kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anasimama hapa kwa mujibu wa kitabu chetu tumegaiwa hapa, unamwambia badilisha, anasusa kusoma taarifa nzima ya Kambi ya Upinzani, halafu na wenyewe wanampigia makofi. Naamini ukitamka neno baya kwa mwenzio, utegemee linakurudi wewe. Humu ndani tuliitwa mboyoyo, lakini tumeona leo mboyoyo ni nani; mtu anaacha kusoma taarifa ya Kambi ya Upinzani, watu wanampigia makofi. Kwa hiyo, mboyoyo wanaeleweka kwenye hili Bunge. (Makofi)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.