Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kupata nafasi. Nianze kwa pongezi kwa hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri. Pia niipongeze kama walivyosema wenzangu wengine; Mheshimiwa Mwamoto, na Mheshimiwa Ngeleja, kwamba umekuwa ni mwaka wenye mafanikio katika soka letu na katika michezo kwa ujumla. Tukianza na Taifa Stars kufuzu kwenda AFCON, hatujawahi kufanya hivyo karibu miaka 40. Ni jambo la kujipongeza na sasa tuelekeze nguvu katika maandalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile haitoshi, tumekuwa waandaaji wa Under Seventeen ya AFCON. Ile kuandaa, pamoja na matokeo ambayo hayaridhishi katika Timu yetu ya Serengeti, lakini kule kuweza kuandaa mashindano haya maana yake ni kwamba kama tunavyosema michezo ni ajira, michezo ni biashara, wakati ujao tunaweza tukaandaa pia mashindano makubwa zaidi. Kwa hiyo, ni kama lesson ya sisi kujiandaa katika kufanya maandalizi ya kufanya mashindano haya makubwa ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitakuwa siyo mwingi wa fadhila kama sitapongeza Bunge Sports Club, tulikwenda pale Burundi wote kuanzia wavuta kamba, soka, riadha, wavu na netball. Kwa kweli kwa sababu mimi nacheza soka kama kiungo mchezeshaji, napenda pia kutoa pongezi za pekee kwa Walimu wetu Mheshimiwa Venance Mwamoto na Mheshimiwa Ahmed Ngwali, walitufundisha na tulicheza mchezo wa kuvutia mpaka walikuwa wanashangaa, ninyi kweli ni Wabunge? Kwa hiyo, pongezi sana kwao na kwa timu nzima ya Bunge Sports Club, lakini kwa uongozi mzima kuanzia Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Sekretarieti kwa maana ya Katibu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niseme kuhusu Simba Sports Club, wamefika robo fainali, ni hatua kubwa katika mashindano ya Vilabu katika Bara la Afrika, nayo imetusaidia sisi kutubeba kama ambavyo wamesema wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mara zote nimesema michezo inaenda na hamasa. Pia nitakuwa siyo mwingi wa fadhila nisipowataja baadhi ya wasemaji wa Vilabu ambao kwa kweli wanatia chachu na hamasa kubwa sana. Mtu kama Masau Bwire, nadhani kuna watu hawamjui kwa sura lakini wanamjua kwa kumsikia; mtu kama Thobias Kifaru wa Mtibwa, Masau Bwire yuko Ruvu; mtu kama Haji Manara; watu kama kina Jafar Idd Maganga; watu hawa wanaleta hamasa ya kuwezesha watu kwenda viwanjani, lakini kama ambavyo tuliona tulipokwenda Burundi, Bunge tulikuwa kitu kimoja. Michezo inaweza kuleta umoja, michezo inaweza kuleta mshikamano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema pongezi hizi, niseme kwamba michezo, sanaa na burudani ni biashara. Kwa takwimu nilizonazo, nchi kama kama Nigeria na Marekani, yaani baada ya ajira inayotolewa na Serikali, inayofuatia ni ile inayotolewa na Sekta ya Michezo, Sanaa na Burudani. Watafiti wamekadiria kwamba, kufikia mwaka 2020, mapato katika Sekta hizi za Michezo, Sanaa na Burudani yatafikia shilingi trilioni 2.2 dola za Kimarekani. Unaweza ukaona ni fedha kiasi gani. Kwa hiyo, nasi hapa nchini ili tuweze kunufaika, vyombo vinavyohusika kama walivyosema wenzangu, viweze kusimamia ipasavyo kutengeneza mazingira bora ili sanaa, michezo na burudani iweze kuwa chanzo cha mapato lakini kama ambavyo sasa ni chanzo cha ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo hivi ni pamoja na BASATA, TFF, Bodi ya Filamu, Shirikisho la Riadha na kadhalika, wajielekze kutengeneza mazingira bora ya kuvutia pia hata wadhamini. Kwa sababu, kwa mfano mchezo wa soka leo hii hatujapata wadhamini kwenye ligi kuu yetu. Kwa sababu gani? Inawezekana mdhamini anakuja mahali ambapo anaona kuna umakini na usimamizi bora. Leo hii ligi yetu ukianzia waamuzi, ni mambo ambayo kwa kweli yako shaghalabaghala.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilienda kuangalia mchezo wa Panama na Baobab hapa katika uwanja wa Jamhuri, hakuna hata huduma ya kwanza. Kuna mambo yanahitaji fedha. Mchezaji kaumia, nimeona amebebwa mgongoni. Kuna mambo ni management, ni usimamizi tu wa kawaida ambao unaongea na Mganga Mkuu wa eneo husika, tunaomba huduma ya kwanza, anawasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bila kuwa na usimamizi ambao ni madhubuti katika michezo, naamini kabisa hatuwezi kuvutia wadhamini; na ile dhana ya kwamba michezo, sanaa na burudani ni sehemu ya ajira na ni chanzo cha mapato, hatutaweza kuifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati tunajielekeza kutafuta fedha, lakini wale wanaohusika na dhamana ya michezo tuhakikishe kwamba tunasimamia kwa ufasaha ili kusudi makampuni yaweze kuwekeza fedha zao. Leo hii tunapozungumza ligi kama ya Uingereza, Champions Leage, inakuwa na mvuto. Wadhamini wanapigana vikumbo kutia fedha zao, kwa sababu iko well organized. Kwa hiyo, kuna mambo yanataka tu usimamizi, kuna mambo tu yanataka management.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, nami nimpongeze pia mwamuzi pekee anayechezesha kwenye AFCON ambaye ni mwana mama Jonesia Rukyaa Kabakama. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule AFCON Mheshimiwa Waziri kati ya waamuzi 56, hakuna hata mmoja ambaye anatoka Tanzania. Hii nayo ni sekta ambayo tunatakiwa kuiangalia, tulee waamuzi, tuwasaidie, walipwe vizuri. Kwa sababu kama tunasema ni chanzo cha ajiria, pia tunapopata waamuzi wanaokwenda kuchezesha michezo ya Kimataifa, kwanza tunatangaza Taifa letu, lakini wanachopata wanakuja kuwekeza hapa nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, nami naomba kuunga mkono hoja. Naomba tujielekeze sasa kuishangilia Serengeti. Pamoja na yanayotukuta, lakini tusikate tamaa, hakuna mwanzo mwepesi, mwanzo daima ni mgumu. Ahsante sana. (Makofi)