Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hoja iliyopo mbele ya Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuanza na nukuu ya Katiba kwenye Ibara ya 18 ambayo ndio inayoleta mjadala mpana humu ndani kuhusu haki na uhuru wa mawazo. Hata hivyo, Wabunge wengi wakisoma kipengele hicho hawaendi kwenye Ibara ya 30(1) ambayo naomba niisome; haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatambuliwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine kwa maslahi ya umma.

Mheshimiwa Spika, sasa ndugu zangu ni sahihi kabisa kwamba tunao uhuru lakini uhuru wetu una mipaka na mipaka yenyewe ni pale uhuru wa kwako unapoanzia kuna mahali unaishia na uhuru wa mtu mwingine unaendelea. Kwa hiyo, ni lazima tunapolizungumza hili tujielekeze katika ibara zote mbili za Katiba.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo huo, naomba nianze na suala hili la vyombo vya habari kuishauri Serikali kwamba ni kweli tulipitisha sheria ndani ya Bunge letu Tukufu lakini jukumu la kutengeneza kanuni tumeliacha kwa Waziri mwenye dhamana tukiamini kwamba atawashirikisha wadau wote katika kutengeneza kanuni. Sasa kwa kuwa sheria kidogo ni ngumu kurudisha mara kwa mara lakini tunaamini kwamba kanuni zikionekana kwamba kwa nyakati tofauti haziendani na sheria tuliyopitisha, basi nimwombe Waziri kwamba sio vibaya kuitisha tena vikao na wadau kuweza kujadili ili kuondoa hizi sintofahamu ambazo tunaziona na zinazungumzwa.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya hili lote ni kwamba sasa hivi karibu kila Mtanzania ni mwanahabari kwa sababu ya mitandao hii ya kijamii Instagram, WhatsApp na Facebook, chochote mtu anachofanya ana-post matokeo yake baadaye kinaenda kwenye jamii na tunaona kwamba ni jambo la kawaida. Ni vizuri sana hasa kwa kuwa tumeanzisha maudhui ya hizi online broadcast, tuwe makini sana katika eneo hili la kila Mtanzania kuwa Mwanahabari.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ni lazima pia hawa Waandishi wa Habari wanaandaliwa kwa namna gani, hili nalo ni jambo la msingi sana. Tumeona vyuo vyetu vingi vya habari vinavyoandaa Waandishi wa Habari ni vya kawaida sana mtaani, ni vya kawaida mno kiasi kwamba hatutarajii kwamba vyuo hivi vije kutengeneza Wanahabari mahiri. Kwa hiyo na lazima hili nalo Serikali ilione kwa sababu yenyewe ndio yenye jukumu la kuhakikisha kwamba tunapata habari ambazo zinalinda mila na desturi zetu kama Watanzania lakini pia zinazingatia uhuru wa Taifa letu na pia kuzingatia usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, sasa leo inawezekana ukakutana na mwandishi wa habari hata hizo sheria zinazoongoza mambo ya usalama wa Taifa hazijui, lakini ni kwa namna ambavyo vyuo vinavyowaandaa ndio ambavyo nadhani tatizo linaanzia hapo. Kwa hiyo, ni vyema Serikali ikatengeneza mitaala kwa kushirikiana na wadau, lakini pia kuboresha vyuo vile ambavyo vinatoa maudhui ya habari ili tuweze kupata Waandishi ambao ni mahiri katika nyanja mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, juzi tulipata wageni kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Duniani (IPI) na nilipata bahati ya kuzungumza nao. Wakati tunazungumza walikuwa wamejaribu kulishwa hii dhana kwamba Tanzania hakuna uhuru wa vyombo vya habari, wakaeleza baadhi ya maeneo. Nami katika kujadili tukawa tunazungumza mmojawapo alikuwa anatoka India, nikamuuliza kwamba kwa mfano sasa hivi India ina mgogoro mkubwa sana na Pakistan, nikamwambia inawezekana kweli Mwandishi wa Habari wa India aka-side na Pakistan akiwa ndani ya India kuhusu labda ule mgogoro unaoendelea pale katika eneo la Kashmir. Alivyonijibu tu akasema hiyo wala inawezekana kama yupo kwenye chombo cha habari wala hatatoka hata ndani ya chombo cha habari.

Mheshimiwa Spika, hii ina maana kwamba sisi tunadhani kwamba uhuru wa habari ni kila kitu unaweza ukaandika, lakini hawa wenzetu ambao tunatoa mifano kwao na wao wana miiko. Mwingine alikuwa anatoka Ujerumani, wakati tunazungumza naye akasema hivyo hivyo kwamba hata kule Ujerumani kuna mwandishi mmoja aliwahi kuandika habari akatoa picha ambayo inaonesha kifaru cha Ujerumani jinsi ambavyo kilikuwa kimechakaa kwamba je, ikitokea sasa hivi wanagombana na nchi fulani, kwa kifaru hiki tunaweza tukashinda vita? Basi mwandishi yule wala hakuweza kuonekana tena, alikuja kuonekana baada ya mwezi mmoja. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba sio kwamba hakuna uhuru ambao hauna mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine kwa uchache sana nielezee habari ya michezo kwamba kwenye michezo nako kuna tatizo. Ni kweli kwamba tumefuzu kwenda AFCON 2019, lakini lazima tujione kwamba kwanza nchi zimeongezwa ambazo zinashindana, zamani zilikuwa 16 sasa hivi zimefika 24. Kwa hiyo, inawezekana labda ni baada ya kutanua goli ndio tukapata nafasi. Jambo la msingi hapa ni kwamba lazima tuwe na mikakati ya dhati kabisa ya kukuza michezo. Chuo cha Michezo kule Malya ni kwa kiasi gani kinasaidia kutengeneza kama sio Walimu wa michezo kwenye shule lakini hata Makocha ambao wanakuja kufundisha vilabu vyetu.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwa mfano nchi jirani ya Burundi hapa ina Makocha kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara karibu sita kutoka Burundi na wote ni wa kizazi ambacho kinalingana. Kina Ndailagije, Masoud Juma kuna yule Ramadhan wa Mbeya City lakini hapa kwetu Tanzania kuna programu gani ya kupeleka Makocha wetu hawa au vijana wakapate exposure ya kujifunza mbinu/medani mbalimbali nje ya nchi. Kwa hiyo, nadhani hili ni eneo ambalo linatakiwa lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia michezo shuleni, bado michezo shuleni haifanyiki kwa kiwango kile ambacho tulikitarajia na vile ambavyo huko nyuma kilikuwa kinafanyika. Mheshimiwa Mwakyembe amesoma Shule ya Wavulana Tabora na ameona ni shule ambayo ilikuwa imejiimarisha kwenye kila aina ya mchezo, alikuwepo pale, nadhani mchezo pekee ambao haukuwepo pale ni netball. Hivi leo katika tasnia hii ya michezo, hapa mpira wa pete huuoni ukifanya vizuri, kurusha tufe na mkuki hatuoni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaona michezo ile ile ambayo jamii imeikubali ndiyo ambayo tunaiona lakini bado kuna michezo mingi ya kukimbia na kadhalika hatuoni ikipewa kipaumbele sana na Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba sana, nimeuliza swali wakati mmoja kuhusu Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa, hebu tupitie hii sera kwa uharaka ili tuweze kutengeneza sera nzuri ambayo pamoja na kushirikisha sekta binafsi, lakini pia Serikali itachukua jukumu lake la msingi la kuhakikisha kwamba sio tu kwamba michezo inakuwa ni sehemu ya burudani, lakini pia michezo inakuwa ni sehemu ya ajira kama ambavyo sasa hivi tumeona duniani kote michezo inaajiri watu wengi sana.

Mheshimiwa Spika, la mwisho lakini sio kwa umuhimu, ni vifaa duni vya TBC. Ni kweli shirika letu la Utangazaji TBC linafanya kazi nzuri sana sasa hivi na limezidi kujenga imani kwa Watanzania, lakini vifaa hawana. Mfano mzuri upo hapa hapa ndani ya Bunge, ukienda kwenye Studio ya Bunge ile ambayo TBC wanarekodi ile mic lazima wanapokezana, kuna wakati mwingine imefungwa na rubber band.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana kwamba ili tuweze kuwa na shirika ambalo linalofanana na Taifa letu kwamba Taifa linapiga hatua, lakini pia Shirika la Utangazaji la Taifa tulione kwamba ni shirika ambalo linaweza kushindana na vyombo vingine vya Kimataifa lakini pia na vyombo binafsi ambavyo tunaona vinafanya vizuri katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)