Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na uzima kuweza kufika siku ya leo. Kipekee kabisa, nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wangu, Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe, kwa miongozo mikubwa ambayo amekuwa akinipatia katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitumie fursa hii kuishukuru kwa dhati Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa michango yake mizuri ambayo imekuwa ikitoa kwa Wizara yangu. Vilevile nishukuru pia michango yote ambayo imeweza kutolewa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimepewa muda mchache, nitaomba nijielekeze katika masuala machache, hususan nikianza na hoja ambazo zimeibuliwa na Kamati. Kuna hoja ambayo imetolewa na Kamati ya namna gani sisi kama Wizara tutaboresha suala zima la Chaneli yetu ya Utalii ambayo tumeianzisha mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba sisi kama Wizara tunayo mipango mizuri kabisa ya kuhakikisha kwamba tunaboresha Chaneli yetu hii ya Utalii. Kwa sababu ndiyo tunaanza mwaka wa fedha wa 2019/2020 tumejipanga kushirikiana na wadau wetu kuhakikisha kwamba Chaneli hii ya Utalii inafanyiwa maboresho makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Wajumbe wa Kamati kwamba tunayo mipango mizuri sana ya kuhakikisha kwamba Chaneli hii ya Utalii kwanza inaboreshwa lakini vilevile itakuwa ni chaneli ambayo inaweza kusikika kimataifa. Kwa sababu lengo ni kuhakikisha chaneli hii siyo kwamba inasikika tu ndani ya nchi lakini pia iweze kusikika kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mipango ambayo tunayo mpaka sasa hivi tayari Chaneli hii ya Utalii imekwishaanza kuoneshwa kwenye chaneli mbalimbali za kimataifa ikiwepo kwenye chaneli ya DSTV, Zuku na kwenye chaneli zote ambazo zinatumia mfumo wa satellite. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia mojawapo ya kuweza kusaidia Chaneli yetu ya Utali iweze kutazamwa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, Chaneli yetu hii ya Utalii kwa sababu ni chaneli ambayo iko ndani ya nchi lakini tunajua kwamba kimataifa huko tunazo chaneli nyingi sana ambazo zimebobea katika masuala haya ya utalii, mpango wetu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba tunashirikiana na makampuni mbalimbali ya kimataifa ambayo yamebobea kwenye masuala haya ya utalii kuhakikisha na sisi kama nchi Chaneli yetu ya Utalii inaweza kutazamwa kimataifa. Kwa hiyo, huo mpango tunao na tunaamini kabisa kwamba muda mfupi na ndani ya mwaka wa fedha huu ambao tunauanza wa 2019/2020, mazungumzo hayo yatakuwa tayari yameshakamilika na Chaneli yetu ya Utalii itaanza kuonekana katika hizo chaneli za kimataifa ikiwemo Chaneli ya National Geographic.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ya Kamati ambayo imezungumza kuhusu kuboreshwa Shirika letu la Magazeti (TSN). Nikiri kwamba kumekuwa na changamoto ya muda mrefu hususan katika suala zima la mapato, kwamba mapato mengi hususani suala zima la matangazo katika magazeti haya ya Serikali yamekuwa yakishuka. Changamoto hii ilitokana na kwamba kumekuepo na ukuaji mkubwa sana wa kasi ya teknolojia ambayo kwa namna moja ama nyingine iliathiri upatikanaji wa matangazo katika magazeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba sisi kama Wizara tumeliona hilo na kunapokuwa na changamoto yoyote ile lazima tuangalie namna gani ambavyo tutaitumia hiyo changamoto kama fursa. Sisi kama Wizara kwa kushirikiana na TSN tumekuja na mpango wa kuhakikisha kwamba tunaweza kukabiliana na hiyo changamoto, kwa sababu suala la ukuaji wa teknolojia, pamoja na kwamba inaweza kuwa changamoto kwa namna moja lakini vilevile ni fursa ambayo naamini hata sisi tukiitumia inaweza kusaidia sana katika kuboresha haya Magazeti ya TSN.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba na sisi tunaanzisha chaneli yetu wenyewe ya kimtandao. Televisheni hiyo tayari imekwishaanzishwa ambayo inaitwa Daily News Digitals. Tunashukuru kwa sababu televisheni yetu hiyo ya mtandao inafanya kazi nzuri sana. Ndani ya muda mfupi mafanikio ni makubwa sana kwani watazamaji wameongezeka lakini vilevile imesaidia sana kuweza kuongeza mapato katika Taasisi yetu hii ya TSN.

Mheshimiwa Spika, iko hoja pia ya Kamati ambayo imezungumzwa kuhusu Serikali iangalie namna gani ya kuweza kuongeza fedha katika Chuo chetu cha TaSUBa kwa sababu kumekuwa pia kuna changamoto kwamba chuo kipo kwenye ukingo wa ufukwe wa bahari na mara kwa mara kunatokea mawimbi ambayo yanaathiri miundombinu ya chuo kile. Niseme kwamba ushauri ambao umetolewa na Kamati tumeupokea lakini kwa sababu ni suala la kushauriana na Wizara ya Fedha na uzuri wenzetu wa Wizara ya Fedha wako humu ndani, sisi kama Wizara tunaendelea na mashauriano kuhakikisha kwamba chuo chetu hiki ambacho kimsingi kimetunukiwa kuwa chuo cha ubora uliotukuka katika Afrika Mashariki kwa maana ya center of excellence, kuhakikisha kwamba Serikali inatenga pesa lakini kila mwaka pesa zinatolewa. Hilo likifanyika tutaweza kumaliza changamoto mbalimbali ikiwemo hilo suala la kuweka fensi ili kuweza kuzuia bahari isiweze kuharibu miundombinu ya chuo vilevile kuhakikisha tunajenga na kuboresha madarasa pamoja na kumbi mbalimbali ambazo zipo kwenye hicho chuo.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ambayo pia imetolewa kuhusiana na Kampuni ya Beijing Construction Engineering, kwamba inakwenda kumaliza muda wake mwezi Agosti 2019, itasababisha Uwanja wetu wa Taifa utakosa mdhamini wa kuweza kuukarabati. Nikiri kwamba ni kweli, sisi kama Wizara tunatambua kwamba tuliingia mkataba na Jamhuri ya Watu wa China kupitia hiyo Kampuni ya Beijing Construction Engineering na unakwenda kumalizika Agosti, 2019.

Mheshimiwa Spika, lakini nitumie fursa hii kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi kama Wizara tupo kwenye mazungumzo na kampuni hii ili kuhakikisha tunauhuisha mkataba huu. Niseme kwamba mazungumzo yetu yamefika pazuri na tunaamini kwamba tutakapofikia mwafaka mkataba ule utaweza kuhusihwa ili kuhakikisha kwamba kampuni hii inaendelea kuhudumia Uwanja wetu wa Taifa katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya umeme, maji pamoja na miundombinu mingine.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Kuna hoja ambayo imeibuliwa na Kamati, Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mheshimiwa Shangazi pamoja na Mheshimiwa Juma Nkamia kuhusiana na suala zima la kuboresha mitambo ya TBC. Ni kweli kwamba siku za nyuma tulikuwa tuna tatizo kubwa sana la uchakavu wa mitambo ya TBC. Nikiri kwamba Serikali ya Awamu ya Tano tangia ilipoingia madarakani tumeona bajeti ya uboreshaji wa Shirika letu la TBC ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ukianza bajeti ambayo ilitolewa mwaka 2016/2017 ilikuwa Sh.1,000,000,000; mwaka 2017/2018 ikapanda ikawa Sh.3,000,000,000; na sasa hivi 2019/ 2020 imefika Sh.5,000,000,000. Sasa tunavyoingia kujadili bajeti ya mwaka 2019/2020, bajeti kwa ajili ya kuboresha masuala yote yanayohusiana na TBC imefika Sh.5,000,000,000. Kwa hiyo, Serikali ina nia ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunaboresha mitambo. Hata ukienda kwenye ofisi ambazo ziko pale Mikocheni, Dar es Salaam imefungwa mitambo mipya kabisa ambayo inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, lengo la haya yote ni kuhakikisha kwamba Shirika letu la TBC kwa sababu kazi yake ni kuhabarisha umma, Watanzania waweze kupata habari ambazo ni za ukweli na za uhakika, tunataka shirika hili lifanye kazi yake kwa umakini ili Watanzania waweze kuhabarishwa. Yapo mambo mengi mazuri ambayo yametekelezwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya mambo mazuri sana, ndiyo maana mimi nikisikia humu Bungeni Wabunge wanakuja na hoja kwamba kwa nini TBC inaonesha Live ziara za Mheshimiwa Rais, hilo suala mimi linanipa shida sana kwa sababu kwanza kile ni chombo cha umma lakini vilevile Mheshimiwa Rais anafanya kazi ya Watanzania, hafanyi kazi ya Chama cha Mapinduzi na anapokuwa kwenye ziara anagusa matatizo ya Watanzania wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tutakuwa ni mashahidi namna gani ambavyo kwenye ziara za Mheshimiwa Rais huko mikoani ukipita sehemu zote unakuta Watanzania wametulia wanafuatilia kazi ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya; iwe ni baa, saluni au mabenki kwa sababu Watanzania wanaona namna gani ambavyo Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri. Kwa hiyo, mimi niseme kwamba hatuwezi kuacha kuonesha ziara za Mheshimiwa Rais kwa sababu ni mambo ambayo yanahusu maendeleo na yanawagusa Watanzania na Watanzania ni vitu ambavyo wanapenda kuviona. Sasa kusema kwamba kwa nini tunamuonesha ni hoja haina nguvu wala mashiko. Kwa sababu Mkurugenzi wa TBC yuko humu ndani, mimi nimwambie kwamba aendelee kufanya kazi kuhakikisha kwamba Watanzania wanajua namna gani ambavyo Serikali yao inatekeleza Ilani pamoja na ahadi ambazo ziliahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ambayo imeibuliwa na Mheshimiwa Amina Mollel, amezungumza kuhusiana na maslahi duni ya wafanyakazi wa TBC. Niseme kwamba kwa kipindi kirefu sana sisi kama Wizara tumekuwa tukijitahidi kuhakikisha kwamba maslahi ya watumishi wa TBC yanaboreshwa na tumechukua hatua mbalimbali. Mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunapeleka ombi kwa Msajili Mkuu wa Hazina ili basi aweze kuboresha mishahara ya watumishi wa TBC. Tunaamini kwamba katika mwaka huu wa fedha 2019/2020, maslahi hayo ya watumishi likiwemo suala la kupandishwa mishahara yatazingatiwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, malizia Mheshimiwa Naibu Waziri, tayari muda.

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi kumekuwa kuna changamoto kubwa sana ya malimbikizo ya madeni kwa watumishi wa TBC. Niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu mpaka sasa hivi imekwisha kutoa Sh.3,200,000,000 kwa ajili ya kumaliza madeni yote ya watumishi wa TBC. Kwa hiyo, Serikali ipo makini inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha. (Makofi)