Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba nimepata nafasi ya kuchangia kama Mbunge kwa kuwa maoni yetu kama Kambi Rasmi ya Upinzani yameshindikana, tutayatumia kwa kuongea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani - Fungu 28 tunalolizungumza leo ikiwepo Polisi na wenzao kuna upungufu mwingi sana unaotokea katika Wizara hii. Nikianza kwanza na suala la wakimbizi. Kuna sare za kijeshi zilikamatwa kwenye mipaka, zile sare zilienda zikachomwa, nakubali, lakini najiuliza wafanyakazi wetu wa Uhamiaji waliachaje zile sare zikaingia katika nchi yetu. Nataka kujua, mambo yapo mawili; kama Taifa la Tanzania tulikuwa na utaratibu wa kutoa taarifa tunapokuwa na watu wasiofaa katika jamii inayotuzunguka na kama kuna kitu kibaya kinatokea, sisi kama Watanzania na Jeshi la Polisi likiwemo na Immigration walikuwa wanapewa taarifa na wananchi, je, mahusiano yetu kama Jeshi la Uhamiaji yapo sawasawa na wananchi, ilikuwaje hizo sare zikapita?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi imekuwa ni chama kingine cha siasa, kimejificha nyuma ya Chama Tawala Chama cha Mapinduzi. Sisi kama chama kilichosajiliwa CHADEMA na wenzetu wa CUF, ACT na vyama vingine tunahitaji kufanya siasa kwa ajili ya kuongeza wanachama na ni wajibu wa kikanuni na Kikatiba kwa sisi kufanya kazi ya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana neno wanatumia intelijensia. Intelijensia ipo kwa Wapinzani na wala sio kwa Chama Tawala. Nataka niwakumbushe Jeshi la Polisi, Tanzania hii amani iliyopo sio kwa sababu tuna jeshi kubwa, sio kwa sababu tuna siasa nyingi, lakini kwa sababu watu wote tumeamua kuipenda nchi yetu na tumeamua kukataza watu wetu watulie na siku ikibidi polisi hawawezi kutushinda kwa maana Watanzania pia ni wengi kama vile Polisi wanafikiri wao wanatuweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafanya mkutano Area A, Area D CCM inafanya mkutano, unakujaje kwenye ofisi yangu kwenye mkutano wa ndani umeshika tear gas kuja kunizuia na CCM hujawazuia? Polisi tunawaonya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua mnatumika kwenye chaguzi kuja kubandika matokeo ambayo siyo kazi yenu. Mheshimiwa Siro nakuheshimu, naomba simamia taaluma ili uweze kuwazuia askari wako kwa sababu mwisho wa siku hawa ni ndugu zetu, tunaishi nao uswahilini, tunasoma nao na tunakwenda nao sokoni. Naomba tusifike tukagombana kwa sababu ya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linazuia Wabunge wenye majimbo kufanya siasa. Mheshimiwa Kubenea wiki mbili zilizopita kazuiwa kwa kitu kinaitwa intelijensiia lakini Mheshimiwa Mchengerwa anafanya mkutano intelijensia haipo. Nchi yetu ni ya umoja, tumeishi kama ndugu, msitutenge. Kama mnataka siasa vueni vyeo ingieni kwenye siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitambulisho vya Taifa. Walioandikishwa ni 19,000 mpaka sasa ni milioni nne tu ndiyo wamepata vitambulisho hivyo na hawa watu wameshindwa kwa sababu hawana pesa, wanadaiwa na mkandarasi. Serikali haijatoa hela, uzalishaji wa vitambulisho ni kidogo, leo hii mnalazimisha matumizi ya Kitambulisho cha Taifa wakati wajibu wa Serikali kutoa pesa hamfanyi. Serikali yako iseme hapa tarehe hiyo 1 Mei waliyoweka ya matumizi ya kitambulisho wazuie mpaka haki ya Watanzania ya kupata vitambulisho ipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni iliyochukua tenda ya kutengeneza mashine za hivyo vitambuliso kutoka Malaysia wameleta mashine ambayo uzalishaji wake ni mdogo na mpaka leo kuna watu waliwekwa ndani, sina uhakika kesi zinakwendaje. Mheshimiwa Waziri akija kujibu atuambie hatua zilizochukuliwa, pesa za Watanzania zilizopotea na wale waliosababisha ufanisi mbovu wamechukuliwa hatua gani mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi tena kwenye Polisi maana yake hawa ndiyo cancer ya Taifa. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni kanuni ipi na ni njia gani inayotumika Polisi ambao wanajua kazi yao ni kulinda mali za Watanzania lakini Polisi hao hao wanakwenda kuwagawa Watanzania kwa itikadi za kisiasa. Ma-OCD, ma-RPC, wote wanasimamia kazi za kiasiasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Wabunge wote wa Upinzani wakitembelea majimbo yao OCD yuko mgongoni. Tunakubali, tunahitaji ulinzi, tunafanya kazi kwa sheria na sisi tumejipanga kuwa waaminifu lakini wanatuchokoza na muda mwingi sana tumewavumilia. Tunafanya mikutano wanashinda na kamera kuturekodi, mikutano ya CCM mbona hawarekodi? Tunawatangazia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji na Uchaguzi Mkuu, tunajua kuna maelezo toka juu kama yapo na sisi tutayafanyia kazi maelezo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku Jeshi la Polisi litueleze shilingi bilioni 16 za sare za Polisi ambapo pesa zilitolewa na mwisho wa siku kuna uniform hewa, ziko wapi? Hii ni kwa mujibu wa CAG.

Naomba kujua matumizi ya fedha hizo na ambazo walipata kutoka kwa wahisani ili kujenga vituo vya mifano ambapo Polisi imeshindwa kufanya. Tunaoma watuambie na hasa Mheshimiwa Kangi Lugola, uje utupe majibu sio ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kangi Lugola ni Mbunge mwenzetu lakini toka ameingia Jeshi la Polisi amekuwa na matamko zaidi ya 20 hata moja hakuna lililotekelezeka. Kuna wakati anatoa matamko kumbe amekosea, sijamuona akirudi hadharani na kuomba msamaha. (Makofi)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Kangi hajaingia Jeshi la Polisi, ameingiaje Jeshi la Polisi?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kangi mara nyingi ameonekana akishusha watu vyeo labda huyo mtu kakosea lakini si haki kwa Jeshi la Polisi kumdhalilisha hadharani, kuna njia sahihi za kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiongelea habari ya Magereza, Magereza kuna msongamano mkubwa na kibaya zaidi magereza ya wanawake wafungwa maeneo ya kuwahifadhi na kujihifadhi nayo ni madogo na wanapata shida sana. Tunaomba Magereza watazamwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jengo la Mchicha kwa Zimamoto, nimelizungumzia mara nyingi. Ni kitu kibaya kutumia pesa za Watanzania tukazi-dump pale Mchicha halafu tunashindwa kufanya mipango ya miaka mingi, tunatumia akili zetu nyingi kuzuia Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea suala la uniform za wafungwa. Uniform ni haki kwa mfungwa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)