Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa ya kusimama leo kuweza kuchangia katika Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Maafisa wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Wizara hii ina changamoto nyingi sana lakini lazima tukiri kwamba kuna kazi kubwa inafanyika na lazima tuwapongeze. Nayasema haya kwa sababu Watanzania ni mashahidi wameona kwa kiasi kikubwa kwamba ajali na uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa sana. Zamani tulikuwa tunashuhudia uhalifu unafanyika katikati ya Dar es Salaam pale Kariakoo lakini sasa hivi hali hiyo imepungua. Ni lazima tulipongeze Jeshi la Polisi katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimponeze Waziri, Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa jitihada kubwa ambazo wanachukua kuhakikisha kwamba wanajenga vituo vya polisi pamoja na magereza. Changamoto ni kubwa kila maeneo, hususan wa wilaya mpya. Binafsi nikushukuru Mheshimiwa Waziri, tumepata shilingi milioni 150 kwa ajili ya kujenga nyumba za Polisi Wilaya ya Kilindi. Bado tuna changamoto ya kituo cha kisasa, wilaya ile ni ya muda mrefu, toka 2002 hatuna kituo cha kisasa. Naibu Waziri ni shahidi alifika Kilindi, nikuombe Mheshimiwa Waziri muiangalie Wilaya ya Kilindi tuwe na Kituo cha kisasa cha Polisi, vituo vya kata vilivyobaki tutajenga sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Katika ukurasa wa 57 umezungumzia Vitambulisho vya Taifa. Hapa pana shida kwa sababu zoezi hili linakwenda taratibu sana. Juzi tumepata taarifa kwamba kuanzia tarehe 1 Mei kila aliye na Kitambulisho cha Taifa ndiye atakayesajiliwa laini, sasa hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wizara ya Mambo ya Ndani iliingia mkataba na Kampuni inaitwa Iris Corporation Berhad ya Malaysia, ilisainiwa Septemba, 2014 na ulikuwa unakwenda hadi 2016 lakini wakaongezewa tena mkataba hadi Septemba, 2018. Jambo hili ni lazima tuseme kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani lazima mlifanyie kazi. Vitambulisho vya Taifa ni haki ya msingi na ni lazima muongeze speed mhakikishe kwamba vitambulisho vinapatikana katika ngazi ya vijiji hadi mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu tunapata malalamiko kutoka vijijini huko kwamba vitambulisho hivi bado. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri lisimamie hili ili Watanzania waweze kupata vitambulisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie juu ya ujenzi wa vituo vya polisi. Nimezungumzia Kituo cha Polisi Kilindi hapa lakini kulikuwa na utaratibu au mkataba na Kampuni ya STAKA ambao walitakiwa kujenga vituo vya Polisi Tanzania nzima. Sasa hapa pametokea changamoto japokuwa naipongeza Serikali iliweza kuchukua hatua kwa wale ambao hawakuweza kutekeleza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, moja ya mapungufu makubwa katika mkataba huu ni kwamba ujenzi wa vituo hivi ulikuwa chini ya kiwango lakini pia waliweza kubadili mipango ya ujenzi. Mahali pengine ni kwamba hapakuwa na mikataba ya ujenzi. Nitoe mfano mmoja tu, ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Lushoto kwa Mheshimiwa Shangazi ambao uligharimu takribani milioni 500 haukwenda sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakuamini sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na uongozi mzima pamoja na Katibu Mkuu, nina imani pamoja na mapungufu yote haya yaliyofanyika basi wale ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo lazima wachukuliwe hatua. Fedha za umma lazima zifanyiwe kazi, haiwezekani pesa zitolewe labda na wadau halafu watu wafanye ndivyo sivyo. Mimi naamini kabisa Mheshimiwa Waziri ulishakuwa Polisi, majukumu haya unayajua vizuri na Katibu Mkuu na viongozi wote wataweza kusimamia vizuri eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la kisera zaidi kwa sababu naiona Wizara hii ni kubwa sana. Afisa Masuuli ambaye ndiyo mwenye wajibu wa kusimamia fedha za umma ana maeneo makubwa sana ya kusimamia. Hili siyo la kwako Waziri, ni suala la Serikali kuliangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuchukue mfano mdogo tu, tuichukulie NIDA yenyewe ambayo inasimamia Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Polisi, Katibu Mkuu ni mmoja tu, anaweza vipi ku-manage? Hebu naomba Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla tuangalie namna ya kufanya restructuring ya Wizara hii. Kwa sababu ukiangalia NIDA yenyewe na hizi taasisi ni takribani Wizara tano. Mimi nadhani wakati umefika tukupunguzie lawama na malalamiko ili Serikali iweze kufanya vizuri katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, pengine niseme tu kwamba kuna mambo ambayo kwa kweli si Polisi wote ambao siyo waadilifu. Kuna tukio moja limetokea Wilaya ya Kilindi, nina Mzee wangu mmoja ambaye yeye amenunua gari kupitia mnada na Mheshimiwa Waziri unalifahamu vizuri sana hili. Cha kushangaza ni kwamba baada ya kununua kwenye mnada yule Mzee amenyang’anywa gari. Mzee yule miaka karibia 40 ametafuta pesa kanunua gari lakini amenyang’anywa. Suala hili liko kwenye Wizara yako, nisingependa kutoa maelezo marefu, naomba wale ambao wanashughulikia suala hili walishughulikie kwa dhati kabisa wampe huyu Mzee haki yake kwa sababu kama mtu ni mhalifu lazima afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru sana, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)