Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nishukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu. Awali kabisa niseme naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niwapongeze viongozi; Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya. Pongezi hizi msingi wake mkubwa ni kwamba watu wengi tunasema hakuna amani lakini ukilala ukiamka salama maana yake amani ipo, hiyo ndiyo tafsiri yake kubwa. Sasa twende kwenye issues useme wapi umekwazwa au wapi hapaendi sawa, lakini ukitoa statement ya generalization haileti afya kwa Taifa hili wala haileti afya kwa Polisi wetu ambao wanatulinda mchana na usiku. Tukitoka hapa tunakwenda kuchoma nyama hapo Chako ni Chako baadaye tunakwenda kulala halafu unasema Polisi hawakulindi. Sasa sisi tutoke wenyewe tuanze kujilinda kama ni hivyo. Kwa hiyo, kazi ya Polisi ni ya kutukuka na tunawapongeza na tunaomba waendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni pongezi kwa Polisi wote lakini pongezi kwa Polisi wa Usalama Barabarani. Taarifa yetu imetuonesha ajali na vifo vinapungua. Tumekuwa tukiwalaumu sana Polisi wetu wa Usalama Barabarani kwa kutubana sisi madereva maana yake sisi wenyewe Wabunge hapa wote ni madereva, sasa lazima tufike mahali tufuate sheria za barabarani, tusiendeshe sisi kama wafalme. Sheria tumetunga inauma kotokote, huwezi kuwatungia sheria watu ambao wako nje ya Bunge, sheria ikitungwa na sisi inatugusa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nichangie hoja hii ya Waziri. Jambo la kwanza, amezungumza mzungumzaji aliyepita suala la kisera. Mimi niko Kamati ya PAC, katika hoja zetu nyingi ambazo tumekuwa tukizipitia tumekuwa tukimpa taabu sana Afisa Masuuli. Tulichogundua ni kwamba Afisa Masuuli ana kazi kubwa sana na ana risk kubwa sana kwa maamuzi yote na vitu vyote vinavyopita mezani kwake. Asimamie Fungu 14, Fungu 28, Fungu 29, Fungu 51, Fungu 93; inakuwa ni kazi kubwa sana. Tunashauri Wizara iangalie namna bora ya kupunguza risk hii kwa Afisa Masuuli mmoja anayesimamia mafungu matano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo nafikiri Wizara ya Fedha inahusika, wataliangalia waone ufanisi unapatikana vipi katika mazingira kama hayo. Hata changamoto za mikataba mbalimbali iliyoingiwa na ufuatiliaji wake, tumeona kwamba mwisho wa yote ufanisi unapungua kwa sababu Afisa Masuuli ana kazi kubwa, anatakiwa awe na jicho kama la mwewe, yaani awe anaona kila sehemu. Kwa hiyo, hilo ni jambo muhimu, liweze kuangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala zima la NIDA. NIDA sasa hivi ndiyo habari ya mjini wanasema, kwa sababu Serikali imeamua kila Mtanzania apate kitambulisho. Kama kila Mtanzania inabidi apate kitambulisho basi Wizara inatakiwa isimamie jambo hili na tuhakikishie wote wamepata vitambulisho. Huko vijijini tumeona ofisi zimefunguliwa, Maafisa wa NIDA wamekwenda hawana vitendeakazi, wamepiga watu picha huko kwenye kata, watu wanauliza vitambulisho lakini vitambulisho havionekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuangalie tatizo limeanzia wapi, ni kwenye mkataba wa uzalishaji vitambulisho. Tunaomba Waziri atakapokuja hapa atuambie mwarobaini wa vitambulisho ni upi? Watanzania wote watakuwa wamepata lini vitambulisho, tupate commitment ya Wizara. Hilo ni jambo muhimu sana na sasa hivi tumeona transactions zote zinazofanyika ukifika kitu cha kwanza unaulizwa Kitambulisho cha Taifa, kwa hiyo, hii ni agenda kubwa na ni agenda ambayo inatakiwa iwe katika boardroom, viongozi wetu wa juu wasimamie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vituo vya Polisi. Nimeona kwenye hotuba ya Waziri amehamasisha wananchi kujitolea kujenga vituo. Pamoja na wananchi kujenga vituo na sisi tunawahamasisha huko kwenye mikutano yetu na kwenye kazi tunazofanya, isipokuwa bado upo ule Mkataba wa STAKA, hatujapata majibu yake ndani na nje ya Bunge, naomba tupate majibu. Maana kuna vituo vimejengwa vimeachwa, kama Mkalama kituo pale kinaanza kuoza sasa, kilikuwa cha ghorofa, kinaharibika, pesa nyingi zimeshawekwa. Manyoni kuna kituo, kilikuwa kijengwe kituo kingine Ikungi na maeneo mengine mbalimbali, Lushoto imetajwa kama mfano. Hilo ni jambo kubwa na vile vituo umefika wakati wake vimalizike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali au Wizara utuambie ni lini vituo hivyo vitakamilika na ituambie kwa uhakika kabisa na usahihi. Kwa sababu hiyo inakuwa ni pesa iliyotupwa. Hata kama ilikuwa ni pesa ya kimkataba lakini ni pesa ambayo inatakiwa iwe accounted for, tujue kwamba vituo hivyo vitamalizika lini, pamoja na kuhamasisha kwamba bajeti zaidi itengwe kwa ajili ya kujenga vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo ambalo wananchi nalo wanataka wajue, yaani kuna wingu zito. Limezungumzwa ndani na nje ya Bunge na kwenye vyombo vya habari nalo ni suala zima la mikataba ya Lugumi, mkataba wa AFIS, tupate kauli ya Wizara, inasemaje, hilo jambo limeishia wapi? Kwa sababu zipo fununu pia kwenye Jeshi la Magereza ipo mikataba mingi inayomhusu Lugumi ambayo na yenyewe ni mikataba tata. Tunaomba Wizara itueleze hapa ili wote tuwe kwenye ukurasa mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa suala la malipo yasiyo na nyaraka timilifu. Hata hoja nyingi za Mkaguzi Mkuu wa Serikali zinaibuliwa kwa sababu ya ukosefu wa nyaraka, unaanza kutafuta waraka mmojammoja. Limezungumzwa suala la sare hewa, sisi tunaamini katika mazingira ya kawaida Jeshi la Polisi siyo eneo la kujifichia, siyo kichaka pale. Kwa hiyo, tunaamini kwamba hizo sare zilinunuliwa na hili suala la nyaraka hewa, mafunzo hewa, sare hewa, Waziri utatuambia ufafanuzi tuweze kujua kinachoendelea ni kitu gani. Jeshi kwa ujumla wake lina nidhamu ya hali ya juu, tunatarajia kwamba nidhamu ianzie jeshini. Kwa hiyo, nidhamu ikiwa nzuri huko hata Wizara zingine na maeneo mengine watainga mfano huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala vitendea kazi tupongeze Wizara, wameleta magari na mimi Mkalama nimepata gari la polisi japo tunahitaji magari zaidi lakini tunashukuru kwa hicho tulichopata. Nimshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Masauni alifika kule na aliongea na wananchi na walifurahia sana kwa hiyo, tunapongeza sana kwa kazi hiyo kubwa inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira, tumeona humu ndani askari wataajiriwa, tunaamini kwamba mnawapeleka mikoani, Mkoa ma-RPC wanawapangia vituo kulingana na uhitaji. Tumeona Wizara ya Elimu wamechukuwa hatua nzuri sana kujua mahitaji ya ualimu kwa kila shule kwa hiyo wanapanga huku walimu wanakwenda moja kwa moja kwenye shule husika. Sasa nafikiri na hata jeshi la polisi liige mfano huo na magereza wawe wanapanga wafanyakazi kutoka huku huku. Kwa sababu wakienda tunawaachia ma- RPC wanapanga siyo kwamba hatuwahamini wakati mwingine tunaona kuna baadhi ya wilaya au kuna baadhi ya maeneo yanahitaji polisi wengi zaidi alafu wanakuwa hawapatikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za askari kuna pesa ambazo zimetolewa za kujenga nyumba za askari, tunaomba hizo pesa nazo mgao wake usimamiwe kutoka Makao Makuu. Tunatambua kwamba mmekasimu madaraka hayo kwa ma-RPC mikoani, lakini mjaribu kuangalia kwa sababu zipo wilaya ikiwepo Mkalama, hakuna hata nyumba moja ya askari. Sasa hizo pesa na zenyewe zinufaishe maeneo kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja tena ahsante. (Makofi)