Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Kilwa Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha leo kuwa na afya na kuongea katika Bunge lako Tukufu. Pili, nawashukuru wapiga kura na tatu nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na mikutano ya hadhara. Sisi sote pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeapa kuilinda, kuitetea na kuienzi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Cha ajabu Serikali hii ya Awamu ya Tano wanazuia mikutano ya hadhara na maandamano kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hata pale Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Magufuli aliporuhusu kwa kusema kwamba sisi Wabunge tunaruhusiwa kufanya mkutano kwenye majimbo yetu lakini Jeshi la Polisi sisi Wabunge nao wanatuzuia. Mimi mmojawapo nimezuiliwa mikutano na polisi inayofika mitano. Nikiandika barua ya taarifa wao wazuia, mwisho juzi nimeandika barua nikazuiwa kwa kusema kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Mpina amechoma nyavu za wavuvi pale ukifanya mkutano basi hali ya hewa itakuwa siyo nzuri.
Kwa hiyo, mimi naiomba Serikali sikivu, iruhusu mikutano ya hadhara kwa mujibu wa sheria za nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza zaidi ndani ya Bunge hili kuna Kamati ya Katiba na inaona Katiba inasiginwa imekaa kimya. Hatusemi Bunge dhaifu lakini kuna tatizo kidogo kwamba Kamati ya Katiba isimamie jambo hili. Hilo ni jambo la kwanza nililotaka kulizungumzia. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunasema nchi yetu haina matatizo, ina usalama na amani, lakini mimi naona si sahihi. Kwa mfano, tarehe 20 Aprili, 2019, kuna kijana wangu amekamatwa na amepelekwa Mtwara na sijui kama atarudi. Kwa sababu mwaka jana katika Bunge hili hili nilisema kuna vijana wangu watatu walikamatwa Ali Shari, Yusuph Kipuka na Ali Yusuph Kipuka mpaka leo hatujui walipo. Niliomba sana na Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo alikuwa rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba lakini hawajapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa wale wanaosema kwamba kuna utulivu na amani katika nchi hii ni kwa kuwa majimboni kwao hawajapata matukio kama haya. Kwa sisi Wapinzani matukio haya yapo, tunaomba Serikali kijana huyu Rashid Salio Rashid aliyepelekwa Mtwara Mheshimiwa Kangi Lugola leo piga simu Mtwara Mheshimiwa huyu kijana aachiwe asipotee kama waliopotea mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema nchi hii ina matatizo. Katika Uchaguzi Mdogo Kilwa Kivinje walitekwa watu watatu na taarifa tukatoa na Mheshimiwa Kangi Lugola ukanielekeza nikafungue kesi, kesi imefunguliwa KLK RB.397 ya 2014. Cha kusikitisha sana walioteka watu hawa wanajulikana, gari ambayo imewateka ya Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka Liwale inajulikana na kuna gari lingine ambalo lilisaidiana lenye namba T693DDD Toyota Passo ya Mheshimiwa Prosper Rweikiza inajulikana lakini kwa bahati mbaya zaidi…
T A A R I F A
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bungara, nitakulindia dakika zako subiri tusikilize taarifa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji asipotoshe Bunge kwa sababu Bunge ni chombo maalum/mahsusi. Gari analolitaja kwamba ni la Mheshimiwa Kuchauka ndiyo liliteka watu si kweli.
WABUNGE FULANI: Kweli.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, gari yangu mimi ilikuwa na namba T324 na namba ambayo iliingizwa kwenye mtandao kwamba imehusika na utekaji ule ni namba T024. Sasa namba hizo ni tofauti na tofauti.
WABUNGE FULANI: Aaaa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, gari anayoitangaza kwamba ni gari yangu siyo kweli. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Bungara.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachosema taarifa nimetoa Polisi na hiyo gari ilikuwepo Kilwa, haikukamatwa kwa sababu walikuwa wanamlinda huyo Mheshimiwa na kama ingekuwa siyo kweli kwa nini isikamatwe? Hiyo namba anayosema ni kweli ilikuwa namba hiyo na tulivyoipeleka ikaoneka gari ya Scania siyo Toyota Land Cruiser. Kwa hiyo, ile gari namba iliyowekwa ilikuwa ya bandia lakini ile gari ni namba yake na ndiyo maana hawakuikamata kwa sababu ilikuwa na namba ya bandia. Mimi naendelea, taarifa yako sikuipokea, ni gari yako na ushahidi upo na kila kitu kipo sahihi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gari nyingine ni T.693 DDD Toyota Passo ya Mheshimiwa Prosper Rweikiza. Taarifa nilitoa Polisi, gari haikukatwa na watu wamepigwa mapanga na watu wao, hii inaonyesha kwamba amani hakuna. Nakuomba Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola fuatilia jambo hili na barua niliandika kwa RPC na wewe nikakupa nakala na ninayo hapa, barua hii hapa na Mwenyekiti nitakupa nakala. Mimi sisemi maneno kwa ujinga ujinga na uhakika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, tulitoa taarifa kwamba kuna watu walipigwa risasi kule Chumo katika Msikiti na Mheshimiwa Mwingulu aliniambia niende kwa Waziri Mkuu. Kwa Waziri Mkuu nikaeenda na barua niliandika nikampelekea Waziri Mkuu. Yeye aliwaambia wale watu atawaita mpaka leo hajawaita na nakala Mheshimiwa Lugola unayo. Naomba Waislamu wale waliopigwa risasi Chumo muwaite muwape fidia kama sivyo tunasema Serikali ya CCM wauaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tukio la utekaji katika Uchaguzi Mdogo, nakuomba Mheshimiwa Lugola uniambie na ushahidi upo. Kama hiyo gari Mheshimiwa Kuchauka anasema sio yake ailete Toyota Cruiser hiyo Kilwa na kwa nini haikukamatwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuthibitisha kwamba Serikali ya CCM inawalinda majambazi, gari hii inayoteka watu ikamchukua iliyemteka wakampeka Polisi na Polisi wanajua kwamba gari hii ndiyo iliyomteka. Pia kwa ushahidi TAKUKURU wakati anatekwa huyo Juma Gondaye walikuwepo na gari waliiona. Mimi nashangaa sana ninyi mnavyosema nchi hii ina amani wananchi mliwapiga risasi, mmewatoa macho, mmewachoma moto kama nao wasingekubali sasa hivi nchi ingekuwa siyo ya amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Mashekhe wa Uamsho. Mwaka jana alisimama hapa Mheshimiwa Kabudi akasema upelelezi unakamika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WABUNGE FULANI: Aaaa.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Bungara muda wako umeisha.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili la Mashekhe lishughulikiwe.