Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Catherine Nyakao Ruge

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia. Tunaitazama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na mafungu yake yote kwa maana ya Fungu la 93 ambalo ni Uhamiaji, Fungu 29 Jeshi la Magereza, Fungu 28 Jeshi la Polisi, Fungu 51 Makao Makuu ya Wizara na Fungu 14 Jeshi la Uokoaji na Zima moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka miwili mfululizo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali alipata fursa ya kukagua wizara hii pamoja na mafungu yake yote. Mwaka 2016/2017 CAG aliibua hoja kumi za ukaguzi kutoka kwenye wizara hii ambazo zilikuwa na thamani ya shiilingi bilioni 128.6. Ukaguzi wa mwaka 2017/2018 CAG aliibua hoja 12 za ukaguzi zilizokuwa na thamani ya shilingi bilioni 180.2. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 40 ya thamani ya hoja zote za ukaguzi kwa maana ya total value of audit queries.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara hii imekuja mbele ya Bunge lako tukufu kuomba tena kuidhinishiwa bajeti kwa ajili ya matumizi kwa mwaka ujao. Ninashangaa wizara hii bila woga imeweza kufanya hivyo wakati ikiwa na hoja lukuki za ukaguzi ambazo hazijapatiwa majibu kwa kipindi cha miaka miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwaka 2017/18 Bunge hili lilipitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya shilingi bilioni 930. Lakini shilingi bilioni 180.2 zinahojiwa najiuliza wanapata wapi confidence ya kusogea mbele ya Bunge hili na kuomba tena fedha kwa ajili ya matumizi ikiwa kuna hoja nzito sana za ukaguzi ambazo zimekosa majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kama hii wizara ina hadhi ya kuja kuomba pesa tena wakati imeshindwa kujibu ufisadi na pesa nyingi za walipa kodi wanyonge Watanzania zimetumika kwa ubadhirifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mifano michache, ufisadi wa kutisha kwenye ununuzi wa mfumo wa utambuzi wa alama za vidole au afisi katika jeshi la polisi. Kulikuwa na manunuzi ya mtambo wa utambuzi wa gharama kwa alama za vidole. Kwanza jeshi la polisi halikuwa na bajeti, lakini hazina ilichepusha kinyemela shilingi bilioni 40.3 kwenda jeshi la polisi kwa kutumia fomu ambazo hazikuwa halisia, afisa aliyehamisha hizo fedha alikuwa hausiki, sasa basi sawa zimekwenda basi zitumike vizuri, maajabu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni 1.7 ambazo zilikuwa zitumike kufunga vifaa vya utambuzi kwenye magereza 35 hayakufanyika. Malipo hewa ya huduma ya matengenezo na uwezeshaji shilingi bilioni 3.3, malipo ya mafunzo hewa shilingi milioni 600.4, malipo ya vifaa hewa shilingi milioni 594 kulikuwa na vifaa vyenye uwezo sawa, mahitaji sawa na sifa sawa lakini zilikuwa quoted kwa gharama tofauti, kwa bei tofauti na hii ikapelekea jeshi la polisi kulipa zaidi ya shilingi milioni 556. Huku ni kupoteza na ni matumizi mabaya ya pesa za walipa kodi. Wote tunafahamu na tunatambua mkandarasi au mzabuni alikuwa ni nani? Alikuwa ni Lugumi enterprises. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nashangaa mpaka leo sioni hatua zilizochukuliwa dhidi ya Lugumi. Nakumbuka mwaka jana Mheshimiwa Kangi ulivyoteuliwa kuwa Waziri ulikuja na kauli nzito na mkwara mzito kweli kuhusu Lugumi na ulim-summon kuja ofisi kwako within 24 hour. Lakini baada ya wiki mbili kuna kitu gani, who is behind Lugumi, tunataka Serikali ituambie mmechukua hatua gani dhidi ya Lugumi na maafisa wote wa Jeshi la Polisi waliohusika na huu ubadhirifu tunataka majibu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, nasema hivi kwa sababu Serikali hii imekuwa ikijipambanua kwamba ni Serikali ya kupinga ufisadi ya kutetea wanyonge hivi ni ufisadi gani sasa ambao mnaupinga huu sio ufisadi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye hoja nyingine, hoja ya Idara ya Uhamiaji. Idara ya Uhamiaji imekuwa ikipata hati zenye mashaka kwa miaka miwili mfululizo. Mwaka huu hati yenye mashaka imesababishwa na Idara ya Uhamiaji kutokurekodi thamani ya ule mfumo ulionunua waki-electronic wa e-migration.

Tunatambua mfumo huu ulinunuliwa, manunuzi yalifanyika kwenye ofisi ya Rais, nashangaa manunuzi makubwa siku hizi yanafanyika kwenye Ofisi ya Rais. Rais amekuwa ndio afisa manunuzi mkuu wa taifa au procurer in chief wakati tunafahamu hatuwezi… [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunafahamu mambo yafuatayo kwa mujibu wa kanuni ya 61(1)(e) lakini kwa mujibu pia wa kanuni ya 61(1)(a). Jambo la kwanza ninalotaka kusema manunuzi ya umma yana sheria yake na yanafata taratibu za kisheria zilizowekwa na Serikali hii. Taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya 34 inampa mamlaka Rais ya uteuzi wa viongozi watakaowajibika na kusimamia majukumu mbalimbali ya Serikali. Lakini Kanuni ya kwanza, Kanuni ndogo niliyoisema ya (e) inayovunjwa na Mheshimiwa Mbunge anapoleta tuhuma nzito ndani ya Bunge hili, kwamba Rais wetu sasa amekuwa Afisa Manunuzi na anasimamia manunuzi ndani ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halivumiliki, siyo jambo la kweli, ni uongo uliopitiliza. Namwomba Mheshimiwa Mbunge athibitishe wapi? Lini? Kwa namna gani? Kwa vigezo vipi Mheshimiwa Rais amefanya hivyo? Ninao ushahidi kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri na ninafahamu Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akizingatia taratibu na sheria na kuzisimamia sheria za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba mjumbe afute kauli yake, kama hataki kufuta kauli hii, alete vielelezo vya kuthibitisha kwamba Mheshimiwa Rais sasa amekuwa Afisa Manunuzi Mkuu na amekuwa akisimamia na kufanya manunuzi yeye mwenyewe. (Makofi)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge,…

MBUNGE FULANI: Kanuni zinasema athibitishe mwenyewe.

MWENYEKITI: Hapana.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, mimi ndio naongoza shughuli na Kanuni ndiyo zenyewe.

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kasimama vizuri sana kwenye point ya utaratibu na ametaja hizo Kanuni ambazo kwa sababu ya muda sitachukua, niseme tu moja ili mjue yeye yuko katika nafasi ya Waziri na kwa mujibu wa nafasi hiyo, ana nafasi pana sana na uwanja mpana sana wa kupata taarifa na ndiyo maana amelielezea Bunge hili taratibu ambazo zinatumika kwa upande wa manunuzi, kwamba haiwezekani hata siku moja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania afanye shughuli za manunuzi kama inavyodaiwa. (Makofi)

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa Kanuni hiyo ya 63 ambayo ndiyo inahamisha jukumu sasa, mimi naridhika kabisa kwamba kwa maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Chief Whip wa upande wa Serikali, yanalifanya Bunge liamini kwamba ana taarifa za uhakika. Sasa Mheshimiwa Ruge Catherine una option mbili, na mimi kama Presiding Officer nakupa option ya kufuta kauli yako ili twende mbele au sasa tuingie hatua ya kukutaka uthibitishe.

Nakupa option ya kufuta kauli.

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta kauli. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, endelea.

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuchangia. Kwa sababu mtambo huu wa kielektroniki wa e-Immigration haukuwa kwenye hesabu za Idara ya Uhamiaji, ilimnyima nafasi Mkaguzi kuweza kukagua manunuzi ya mtambo huu na hivyo kupelekea Idara ya Uhamiaji kupata hati yenye mashaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anakuja ku-wind up atueleze ni kwa nini fedha hizi au thamani ya mtambo huu ambao ulinunuliwa kwa shilingi bilioni 127 haukuweza kuonekana kwenye hesabu za Idara ya Uhamiaji kwa sababu hilo ni takwa la kisheria la IPSAS 31. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2018 hapa, tuliambiwa e-Immigration ilikuwa na component nyingi sana zaidi ya nne ikiwemo e-passport, e-border, e-gate na vitu vingine. Ningependa kufahamu mchakato huu umefikia wapi? Baada ya e-passport zile components nyingine ziko katika hatua gani kwenye mchakato? Kwa sababu nimejaribu kupitia kitabu chake na sijaona amelizungumzia suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzingumzia manunuzi ya sare hewa ya Jeshi la Polisi ya shilingi bilioni 16. Naitaka Serikali iweze kutoa majibu juu ya suala hili. Pia kuna fedha shilingi milioni 800 ambazo zilitoka Jeshi la Polisi zikawalipa watu ambao siyo Polisi. Tunataka tuambiwe watu hao ni akina nani kama siyo Polisi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)