Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia hoja ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Nataka nianze na hoja ya vijana wa bodaboda wa pale Mchinga kutakiwa kuwa na kitambulisho cha Sh.20,000, hivi vitambulisho vilivyotolewa na Mheshimiwa Rais. Nataka kupata majibu kwamba huu ndio utaratibu? Mimi nimesoma ule Waraka unaoainisha ni watu gani wanapaswa wachangie ile Sh.20,000, sijaona sehemu ya bodaboda. Kwa Mchinga pekee bodaboda baada ya kuwa na leseni wanatakiwa pia wawe na kitambulisho cha Sh.20,000.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri akija aje atueleze kwamba haya ni maelekezo yanafanyika kwa ajili ya kukusanya kodi na ikiwa kama bodaboda wanatakiwa wachangie Sh.20,000, je, madereva wa gari taxi kwa nini nao wasilipe? Kwa hiyo, hili jambo nataka nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nakubali kama wenzangu wanavyokubali kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri na kubwa ya kulinda raia na mali zetu tulizonazo lakini yapo mapungufu lazima tuyaseme na Jeshi la Polisi wayachukue waweze kuyafanyia kazi yabadilike. Dhamira ya mtu inapimwa kwa maneno na vitendo, wakati mwingine unaweza ukachafuka kwa ajili ya maneno yako tu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano anapotokea Polisi akasema nitawapiga na kuwachakaza, hili neno linaudhi lakini pia halina tafsiri njema kwa raia ambao umeapa utakwenda kuwalinda wao na mali zao. Kwa nini usitumie lugha nyingine ambayo inaweza ikatumika kuzuia lakini pia wewe ukaonekana kwamba dhamira yako ni njema katika kulifanikisha jambo lile.
SPIKA: Kwa mfano Bobali, hebu mfundishe lugha ya kutumia, asemeje?
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, kwa mfano tu aseme maandamano haya yamezuiwa na msiandamane, inatosha. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Aaaaa.
SPIKA: Sasa huyo anayesema hivyo ni Mwenyekiti wa Mtaa au askari huyo? (Kicheko)
Endelea Mheshimiwa Bobali.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
SPIKA: Askari ni askari tu, kama umepita JKT hutashangaa hivi vitu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru lakini katika tamaduni za kawaida kabisa Polisi walioapa kulinda raia na mali zao si vyema kuwatisha kwamba watawapiga na watawachakaza, si vyema kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi yako mambo Jeshi la Polisi lazima tuyaseme wamefanya vizuri. Kwa mfano, katika jambo la kupambana na ujambazi, kiwango cha ujambazi kimepungua, hili ni jambo la kupongeza, wanafanya kazi nzuri sana lakini yako mambo yanatia doa Jeshi la Polisi. Kwa mfano, very recently Jimbo la Mchinga kulikuwa na uchaguzi, Diwani mmoja alikuwa amefariki mwezi Machi, kwa hiyo, uchaguzi ukatangazwa.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi wakiwa kwenye gari ya polisi, wakiwa na silaha zao wamekwenda nyumbani kwa mgombea wa Chama cha CUF kumlazimisha asaini barua kwamba yeye anajitoa. Jeshi la Polisi usiku wamemvamia nyumbani kwake. Bahati nzuri tulijua kabla hawajakwenda tukamwambia toka akakimbia. Sasa Mheshimiwa Waziri, haya ndiyo majukumu ya Jeshi la Polisi? Tena wakiwa wameambatana na msimamizi wa uchaguzi, unakwenda nyumbani unamwambia saini hapa kwamba unajitoa halafu baadaye wanatangaza kwamba wamepita bila kupingwa, this is not fair. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mambo kama haya yanatia doa Jeshi la Polisi. Tukikaa nao hawa Polisi wakati mwingine ni rafiki zetu wanatuambia kabisa jamani eeh sisi tunaambiwa. Sasa ni nani anayewaambia Jeshi la Polisi kufanya kazi hii? Ukija utuambie kwamba wewe Waziri ndiyo umewaambia kwa sababu tunakuona muda wote unashika Ilani ya CCM unatembea nayo …
SPIKA: Mheshimiwa Bobali, tukikutaka utuletee hao Askari waliokwambia haya unayoyasema humu utaweza kuwaleta?
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, mimi natekeleza jukumu langu la kumfahamisha Mheshimiwa Waziri.
WABUNGE FULANI: Aaaaa.
SPIKA: Unatekeleza jukumu lako lakini hupaswi kutudanganya kama Bunge, hili ni Bunge.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, sidanganyi.
SPIKA: Kwa hiyo, kama ulipewa taarifa hizo inconfidence basi ni vizuri ukae nazo inconfidence, as long as unaziweka hapa maana yake uko tayari kutuletea hao Askari waliosema hayo na kama hauko tayari kuleta hao Askari maana yake wewe uko tayari kuwa liable kwa unayoyasema. Yaani lazima upime kama kiongozi kuna habari unapewa kwa matumizi yako mradi umeamua kuyaanika hapa maana yake uko tayari kusimama nayo.
Sikukatazi kusema endelea mradi uwe tayari kwa hayo naku-caution tu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nimekuelewa ila nachosema tunakokwenda kwenye mwaka wa uchaguzi huu Serikali za Mitaa, jeshi letu litumike kwenye kutulinda na kuhakikisha kwamba vyama vyote vinatendewa haki. Hilo ndiyo hoja yangu, nimekuelewa.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni kwenye suala la uhamiaji. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji lakini kuna jambo lina dosari. Kumekuwa na wahubiri especially wa Kiislamu wamekuwa wakija miaka mingi hapa wanapita kwenye maeneo yetu wanakuja kuhubiri hasa karibu na mwezi huu wa Ramadhani. Mheshimiwa Waziri anajua kwamba wako wahubiri mwaka jana waliondolewa hapa nchini kwa kupewa warrant ya saa 24, ikawa shida sana. Sasa hivi kumekuwa na shida nyingine wahubiri wakiomba visa inakuwa shida sana wakati mwingine mpaka hata ule muda wenyewe uliokusudiwa kwamba twende tukaelimishe au tukaseme hili unapita.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili mliangalie. Tunajua kwamba mnaangalia mambo ya ugaidi na kadhalika lakini wako wahubiri mkiangalia records zao wamekuwa wakija kwenye nchi hii miaka yote. Kwa mfano, mimi toka nimekuwa na akili timamu wako watu nimewahi kuwaona wanapita maeneo yetu wanakuja wanahubiri wale Wapakistani lakini sasa hivi wakiomba visa kuja Tanzania inakuwa shida sana. Sasa Mheshimiwa Waziri wakati mwingine mnapozuia watu hebu tazameni na records zao kwamba hawa wana record gani zilizopita?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.