Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa namna ya pekee, naomba nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya na ma-RPC wakiwakilishwa na Bwana Mroto – RPC wa Dodona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wanawalaumu Polisi wakati sisi usiku tumelala na wake zetu tunapata joto wenyewe wamekumbatia bunduki wanapata ubaridi kwa ajili ya kuhakikisha sisi tunalala salama mpaka asubuhi. Inasikitisha kuona sisi Wabunge kama wawakilishi tukitumia Bunge kama jukwaa kwa ajili ya kuwapiga na kupambana na Jeshi la Polisi, hiyo haipendezi kabisa.

Mheshimiwa Spika, watu wanashindwa kutofautisha kati ya Polisi na Afisa Maendeleo ya Jamii. Polisi siyo Afisa Maendeleo ya Jamii ndiyo maana imeitwa Police Force, sawa? IGP Siro kama upo humu ndani wewe siyo Kamishna wa Maendeleo ya Jamii, kwa hiyo, asikuchezee mtu, umepewa nguvu kwa mujibu wa Katiba, kwa hiyo komaa! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wanalalamika kuhusu shughuli za kisiasa, hao wanaolalamika ni wale waliovamia treni kwa mbele. Kwa wanasiasa sisi wenyewe wakongwe wa siasa ambao tunaijua alichofanya Nyalandu kutoka CCM kwenda CHADEMA ile ni siasa siyo mpaka ufanye mkutano wa hadhara, alichofanya Maalim Seif kutoka CUF kwenda ACT ile ni siasa kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata anachofanya Lipumba kuondoa wasaliti ndani ya CUF ile ni siasa tosha siyo mpaka mikutano ya hadhara. Wanachofanya akina Zitto Kabwe, wale wanaoongea na waandishi wa habari, ile ni siasa kubwa sana katika nchi siyo mpaka mfanye mikutano ya hadhara, hizo ni siasa za zamani na zinaharibu maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, naomba Jeshi la Polisi likomae.

Mheshimiwa Spika, pia mnaozuiliwa siyo ninyi tu, kwa mfano mimi Ulanga niligundua ufisadi wa shilingi bilioni 2.9, wananchi wangu waliandaa mkutano mkubwa na mapokezi ya kunipokea mimi. Polisi waliniambia Mheshimiwa Mlinga utakapofanya hilo, kuna wahalifu wako ndani ambao wanaumia na ule ufisadi uliougundua kwa hiyo usifanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, siyo wao tu, siyo kila kitu lazima tuseme na siyo kila barua unayopewa na Polisi lazima uweke katika vyombo vya habari, hiyo haiwezekani. Kwa hiyo, Polisi wanawazuia siyo ninyi tu hata sisi sehemu yoyote, sasa mkiachiwa mkadhurika mtasema Polisi hawafanyi kazi. Kwa mfano, Mheshimiwa Tundu Lissu alipopigwa risasi angepewa tahadhari tangu mwanzo mngesema kaonewa. Kwa hiyo, muwe mnawasikiliza, hawa wanafanya kazi kwa taaluma, wameenda wamesomea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote, kuna matatizo katika Jeshi la Polisi la nyumba za askari. Sisi Morogoro pale tumeanza mkoani tunajenga nyumba kwa ajili ya maaskari wetu.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la uniform kwa Polisi. Juzi wakati tunaangalia Ripoti ya CAG shilingi bilioni 16 za uniform za polisi ni hewa, wanasema nyaraka hazionekani lakini hata nilipopita karibu na IGP nikagundua hata ile uniform yake bado ni ya zamani. Kwa hiyo, najua kabisa hii bilioni 16 hakuna uniform hata moja iliyonunuliwa na Polisi hawawezi kusema wao wenyewe kwa sababu mfumo wao wa chini hawezi kumhoji wa juu. Kwa hiyo, uniform Polisi mpaka wanaokwenda kucheza gwaride tena katika sherehe kama za Uhuru yaani mtu baada ya miaka mitano ndiyo anapata uniform, kwa hiyo, bado hatuwatendei haki.

Mheshimiwa Spika, suala la vitendea kazi, siku moja nilishuhudia askari anaenda kuchukua maiti hawana hata ile mifuko ya kuwekea maiti kwa hiyo hawana vitendea kazi. Kwa mfano, camera, posho, mtu anapewa kazi akachunguze kesi ya mauaji hapewi hata shilingi 10, unategemea nini kitakachotokea? Yule anayetuhumiwa si anamhonga hela kiasi tu anaachana nayo?

Mheshimiwa Spika, mafunzo kwa Jeshi la Polisi bado yanatolewa kwa upendeleo yaani mtu mpaka awe anamjua mtu wa juu ndiyo anapewa nafasi kwa upendeleo. Hilo hamuwatendei haki polisi wetu.

Mheshimiwa Spika, bado kuna mapungufu mengine kwa mfano, Dar es Salaam, eti unakuta katikati ya Mji Dar es Salaam kuna tochi yaani askari anakaa anapiga tochi katikati ya Da es Salaam. Kwa mfano, maeneo ya Tegeta, Mbezi, Oysterbay kuna tochi, hivi tochi Dar es Salaam inafanya kazi gani? Tunajua Sheria za Usalama Barabarani hazihitaji gari moja kukaa mbele ya lingine mita tatu, sasa Dar es Salaam hiyo mita tatu unaitolea wapi, Askari anakukamata. Eti Dar es Salaam umekanyaga Zebra askari anakukamata. Kwa hiyo, hapa naomba muwe mnaangalia hizi sheria zenu ziwe zinaendana na mazingira.

Mheshimiwa Spika, lingine ni ulevi, sizungumzii askari wote. Ulevi unaruhusiwa lakini mahali pa kazi hauruhusiwi. Siku moja nilikuwa naongea na Mheshimiwa Waziri nampa taarifa na yeye akanipa kesi yake siku moja na yeye alilindwa na askari ambaye amelewa, nikamwambia wasiwe wanapewa silaha, wawe wanachunguzwa kwanza kama wamelewa au la.

Mheshimiwa Spika, lingine ni counseling, askari kabla hawajapewa silaha wawe wanafanyiwa counseling kwa sababu hujui mtu ametoka katika mazingira gani huko alipotoka. Ndiyo maana ukichunguza wako maaskari wanaua wenzao maeneo ya kazi, wako maaskari akipewa silaha baada ya saa mbili anajipiga risasi. Kwa hiyo, muwe mnawafanyia counseling mgundue wana shida gani kwa sababu hata mishahara yenyewe ni midogo.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine tena nilipewa na askari. Kuna maaskari mwaka 2013 walilipa fedha kwa ajili ya kupatiwa viwanja Chalinze Mzee na kampuni moja inaitwa Ardhi Plan International, askari zaidi ya 1,000 na wamelipa hiyo hela ikiwa ni pamoja na hati lakini hakuna hata askari mmoja aliyepewa hati. Naambiwa hizo pesa zimepigwa na viongozi wa Polisi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri unapo-wind up tafadhali nahitaji majibu, hawa askari wanapata lini hati zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Uhamiaji, ameongea Mheshimiwa mwenzangu Bashe. Uhamiaji ndiyo jeshi ambalo linafanya vibaya kwa sasa hivi. Uhamiaji mmegeuza watu kuwa mitaji yenu. Mtu akigundua kijana anatembea na mke wake anaenda kuongea na watu wa Uhamiaji wanampa nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, leo hii wanakukamata wanakwambia wewe siyo raia wa Tanzania na ni wengi. Kuna kesi moja nilipeleka mimi kwa Mheshimiwa Waziri na hata Kamishna wa Uhamiaji nimemwaambia, kwa hiyo, Uhamiaji imegeuzwa silaha kwa ajili ya kuwapigia watu. Kama alivyoongea Mheshimiwa Bashe, tukianza kuchokonoana kutafutana uraia tutakaobaki raia halali wa nchi hii ni Wapogoro na Wazaramo peke yetu, wengine wote ni wahamiaji. (Kicheko)

WABUNGE FULANI: Aaaa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Ndiyo! Kwa sababu Wangoni tunajua mmetoa Afrika Kusini, Wachaga ninyi ni Wasomali, kwa hiyo, tutakaobaki ni sisi peke yetu. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Mlinga, taarifa. Watakaobaki ni Wagogo peke yake maana ndiyo wa katikati. (Makofi/ Kicheko)

Endelea Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Uhamiaji imegeuka fimbo kwa wananchi wetu wa Tanzania. Pia Uhamiaji wamewageuza hawa watu wanaoishi sasa hivi, kwa mfano, watu wa Congo wa Dar es Salaam ndiyo mitaji yao. Leo Afisa Uhamiaji akiona mambo yake magumu anamtafuta mtu mmoja wa Congo anampiga blahblah pale anachukua hela, watu wa Uhamiaji.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la zimamoto. Tunashukuru kwa kutupa Maaskari wa Zimamoto hata Ulanga tumepata. Hata hivyo, unatuletea Askari wa Zimamoto Ulanga hata koleo la kubebea mchanga hana, gari hana, anafanyaje kazi? Ina maana moto unapowaka naye anasaidia kuja kutuangalia? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la NIDA kuhusu vitambulisho. Leo miaka minne NIDA wametengeneza vitambulisho milioni nne. Sasa hata tukiwapa huo mwezi Novemba bado hawatakuwa na uwezo wa kutengeneza hivyo vitambulisho kwa Watanzania. Watanzania tuko zaidi ya milioni 50, kwa hiyo, muda tuliowapa ni mdogo na kazi yao wanayoifanya ina changamoto nyingi.

Mheshimiwa Spika, la mwisho nimalizie na suala la kupata uraia. Kuna shida kubwa, watu wana muda mrefu hawajapata uraia. Mtu ameomba uraia miaka 10/15 iliyopita hajapewa mpaka leo, hili linatengeneza mazingira ya rushwa. Wako hata hapa Wabunge wana wake ambao siyo raia lakini wameshughulika sana na imeshindikana. Kwa hiyo, hili linachangia kuleta rushwa katika kitengo hicho cha kuwapa watu uraia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)