Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo kwa namna moja au nyingine imefanyiwa uchambuzi na Serikali na kuondosha aya nyingi ambazo kama Kambi tuliona ni muhimu kutoa maoni yetu, kuishauri na kuihoji Serikali.

Mheshimiwa Spika, napenda kupata majibu ya Serikali kuhusu Polisi kukamata raia na kuwaweka mahabusu ya Polisi muda mrefu hadi miezi sita bila kuwapeleka Mahakamani na wengine kuwaweka mahabusu ya magereza hadi miaka kumi na kuendelea na kusema upelelezi haujakamilika. Naongea haya nina ushahidi kwa Magereza ya Idete, Kiberege, Morogoro Mjini (Manispaa). Hivi kwa nini hii Serikali inawatesa raia/nguvukazi namna hii? Napenda kupata majibu ya Serikali kuhusu uvunjaji huo wa haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, sababu mojawapo inayosababisha mlundikano wa mhabusu magereza ni DPP kuchelewesha uchunguzi kwa kifungu cha 225. Je, lini Serikali itakifuta kifungu hicho ambacho ni cha ukoloni wakati huo kunyanyasa watu weusi? Kifungu hiki kinasababisha mazingira ya rushwa kwa waendesha mashtaka na kuangamiza familia/raia.

Mheshimiwa Spika, mahabusu ya wanawake Gereza la Morogoro Manispaa ina hali mbaya kwa wanawake kutumia choo kimoja ambacho kiko nje ya maselo hayo matatu ambapo kuanzia alasiri wanapofungiwa na ikiwa mahabusu amepata tumbo la kuhara inampasa ajisaidie kwenye ndoo ambayo ni moja (mtondoo) uliopo ndani na kulala nayo hadi asubuhi. Je, huu ni uungwana kwa wanawake kufanyiwa ukatili huo?

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi mahabusu hao wanatumia choo kimoja na maaskari walio zamu na kuhatarisha maisha ya maaskari hao. Je, ni lini Serikali itaboresha selo za gereza hilo? Kibaya zaidi selo hiyo haina bomba la maji ya kunywa, bomba liko moja tu chooni ambako hutumiwa kupata maji ya kunywa, hivi sisi hapa tunakunywa maji ya chooni? Naomba Serikali iweke miundombinu haraka katika gereza/mahabusu hiyo ambayo ina wanawake waliowekwa hapo zaidi ya miaka mitatu hadi mitano bila kesi zao kuisha au wafungwe ama waachiwe.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ipeleke trekta na vifaa vingine vya kilimo Gereza la Idete ili wazalishe kwa tija. Trekta moja walilopewa halitoshi kwa kuwa wana eneo kubwa la kilimo.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mlimba liko kilometa 235 hadi Ifakara ambapo ndipo kilipo Kituo cha Polisi cha Wilaya hivyo kupelekea wananchi wengi kukosa haki zao. Serikali imeomba jengo la TAZARA kuhifadhi askari wachache kujibanza hapo kutokana na kutokuwepo kwa jengo lao.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, pamoja na umbali huo na ukosefu wa barabara ya lami na uwingi wa mvua zilizopo Mlimba, askari hao hawana gari la uhakika. Halmashauri na watu wa Mlimba kwa kuona umuhimu wa uwepo wa Kituo cha Polisi walitoa eneo la ardhi bure ili Serikali ijenge Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itajenga kituo cha kikubwa cha Polisi, Jimbo la Mlimba ili kuepusha usumbufu kwa wananchi? Napenda kupata majibu ya Serikali, je, bajeti hii imetenga kiasi gani cha fedha kuanza ujenzi wa kituo hicho? Kuhusu gari, ni lini Mlimba itapata gari la uhakika kutokana na mazingira yake?

Mheshimiwa Spika, nilishaongea na Waziri, Mheshimiwa Kangi mara nyingi kuhusu matatizo mbalimbali ya rushwa zinazofanywa na baadhi ya maaskari wa barabarani kwa watoa huduma ya usafiri kwa wananchi wa Mlimba ambao ni waendesha Noah, pikipiki na kadhalika. Wao wenyewe wako tayari kumueleza Waziri kuhusu kero hiyo kubwa ya rushwa. Pia nilimwambia kuna rushwa ndani ya Ofisi ya Upelelezi kwa baadhi ya maaskari. Vilevile nilimuomba afanye ziara Jimbo la Mlimba lakini pamoja na ahadi alizonipa hadi leo hajatekeleza. Je, ni lini sasa Mheshimiwa Kangi Lugola, Waziri, atafanya ziara hiyo kama alivyoahidi? Ahsante.