Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii adhimu. Awali ya yote, nawapa pole wanawake wote waliodhalilishwa jana, maana pande zote walidhalilika; wanawake hawana chama; kudhalilishwa hakuangalii chama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwanza nijue suala la viwanda kama ni vision ya nchi au ni vision ya Mheshimiwa Rais? Mheshimiwa Waziri baadaye akija atusaidie, atuambie kama ni ya Mheshimiwa Rais atusaidie. Atakapovianzisha, hawataviuza wengine? Maana vilikuwepo, wakauza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri, kama inawezekana, kwa baadhi ya vitu tunavyoanzisha tuwe tunatunga sheria ya kuvilinda hivyo tulivyovianzisha. Yaani siyo tunaanzisha, anakuja mtu mwingine baada ya miaka mitano, naye anabadilisha anakuja na mambo mapya mengine kabisa, kama vile hatukuwahi kuwa na kitu chochote hapa nchini. Kwa hiyo, hata hiki kitu kama kingefanikiwa, kitungiwe sheria ya kudhibiti, atakayekuja asikiharibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa nchi zilizoendelea, waliouza viwanda vyetu wangekuwa ndani, jela! Walitakiwa wawe jela, maana mlijua kabisa ili twende kwenye uchumi imara wa nchi hii ni kuwa na viwanda na lilijulikana mapema, lakini sasa hivi ndiyo linatokea, linashamiri baada ya kuwa tumeviuza vile tulivyokuwanavyo. Maana yake nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wale walioviuza ndio wametufikisha kwenye uchumi mbovu tulionao! Kwa hiyo, nchi za wenzetu zilizoendelea, hawa walitakiwa watangulie Segerea ili watusaidie kujibu kwa nini wameifanya nchi kuwa maskini kwa kuuza viwanda ambavyo vingetupeleka mahali pazuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze mambo madogo kabisa yanayohusiana na viwanda. Wala tusiende kwenye viwanda vikubwa sana vya mtani wangu Mheshimiwa Mwijage, akiyaeleza unaweza ukadhani kesho asubuhi hii nchi inakuwa mbinguni. Hii nchi ni Tanzania ile ile, hii hii! Haiwezi kubadilika katika wiki moja, mbili, miaka mitano au kumi, haiwezekani! Atusaidie! Tena nimshauri, ni mtani wangu, aongee machache, atende mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni hii hii ambayo machungwa yanaoza, hakuna anayeshituka; maembe ya wakulima yanaoza, hakuna anayeshituka; nyanya za Watanzania zinaoza, mnaagiza tomato sauce Ulaya na mko hapa hapa! Nanasi zinazooza ni nyingi! Nani kiongozi wa Serikali anaona uchungu kwa mazao yanayoweza kufanyiwa process ya viwanda na akashituka akasema hapa tuweke kiwanda? Tunaangalia tu! Wala havihitajiki viwanda vikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kawaida sana vingeweza kututoa hapa tulipo kwenda mbele zaidi. Tunafikiria makubwa wakati uwezo wa makubwa hatuna. Hii bajeti ya Mheshimiwa Waziri haiwezi kutengeneza hayo yote tuliyoyasema na wafadhili tunaowategemea, Mheshimiwa Waziri atuambie, walikaa mkutano wapi, kwamba watakuja waweke viwanda Tanzania? Watakuja wawekeze viwanda vyetu Tanzania; uwekezaji Tanzania sasa hivi nao unaanza kuwa shida na unaanza kuwa taabu! Masharti lundo! Kwa hiyo, tungeanza na vitu vya kawaida, vya chini mno! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za wenzetu; nimeona Uingereza, mwananchi mkulima wa kawaida mazao yakiharibika, Serikali ina-compensate.
Sisi hapa halipo! Tunaliona la kawaida tu! Tena mazao yakiharibika ndiyo mnakwenda, jamani poleni, zile nyanya vipi, zimeharibika? Yaani ni jambo la kawaida tu, lakini hatujui nguvu aliyotumia, familia yake itaishije kwa taabu kabisa katika mazingira kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumzia viwanda Kigoma kwenye swali asubuhi. Mpango ule wa Kiwanda cha miwa na sukari Kigoma kilianza Bunge la Kumi. Mpaka leo hakuna muwa hata mmoja pale Kigoma! Kwenye kitabu chako hiki, hakuna hata ukurasa uliotaja ile miwa ya Kigoma, hakuna! Sasa watakujaje humu hawamo? Hata hao wawekezaji wenyewe ambao wangekuja! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli tunahitaji kukaa vizuri na hili suala la viwanda. Tusiwaaminishe sana Watanzania, baadaye watatuuliza maswali haya haya, humu humu kwamba hivi mlisema viwanda yaani kwa mbwembwe kwa mkwara kweli kweli, mmefika wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo naona linaleta shida, ni biashara ambayo iko chini ya Waziri mwenyewe. Nchi hii kufanya biashara ni risk yaani owners risk. Hakuna mazingira rafiki ya kufanya biashara katika nchi hii. Wakati wa uchaguzi mimi huwa naupenda sana, ni kwa sababu tu unakuwa ni muda mfupi. Watu wanafaidika na mambo yote mabaya yanasimama ili watu wapate kura, baada ya hapo yanarudi yale yale mabaya waliotendewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna watu wanateseka nchi hii kama bodaboda! Wanakimbizwa na polisi kila asubuhi! Tujiulize, wale watu wa bodaboda wangekuwa hawana hizo bodaboda, nani angekuta side mirror kwenye gari lake? Ujambazi ungekuwa mkubwa kiasi gani? Watu wametafuta ajira binafisi, lakini wanakimbizana na polisi kila asubuhi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu, Wilayani kwangu Kakonko ili uweze kupata TIN Number unakwenda kilometa 300 za barabara zisizo na lami, kuifuata Kigoma Mjini. Unamwambia mtoto wa watu afuate hiyo TIN Number, halafu afuate na leseni, sijui na vidude gani, kilometa 300, anakimbizana na oolisi tu! Bodaboda wangapi wamekufa wakiwa wanakimbizwa na polisi ili wawakamate tu wachukue fedha? Matokeo yake sasa umekuwa ni mradi wa polisi na mwenye bodaboda. Bwana eeh, una leseni? Wewe unaniulizaje leseni na jana sikuwanayo, unaniuliza leo tena? Anachukua fedha zake, anaweka mfukoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawakatisha tamaa wafanyabiashara wa nchi hii. Biashara ya maduka, VAT inasema hivi ili uweze kulipa VAT TRA, mwenye biashara awe na bidhaa inayozalisha shilingi milioni nne kwa mwaka. Wanakimbizana na wauza soda vikreti viwili, anakuja anampigia hesabu mtu wa TRA, wewe unauza soda, eeh, kreti tano kwa siku mara siku 30 mara mwaka mzima, anamtoza kodi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana!