Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, nianze kukushukuru wewe na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha 2019/2020 hali ya usalama wa raia na mali zao umeimarika. Pamoja na changamoto zilizojitokeza za mauaji ya watoto na kupotea kwa watoto katika Mikoa ya Njombe na changamoto za hapa na pale ambazo hazijakatisha tamaa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kulinda raia na mali zao na wote tunaotambua na kuthamini kazi kubwa mnayoifanya, tunawatia moyo endeleeni kuchapa kazi. Watanzania walio wengi wanawaunga mkono na kuwaombea dua njema. Taarifa imeandaliwa na Mheshimiwa Waziri na timu yake, wanafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani; pamoja na kuipongeza Serikali kwa kupeleka fedha kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 86, nashauri fedha ya Wizara hii ipelekwe yote na bajeti iongezwe kwa sababu majukumu ya Wizara hii ni muhimu na nyeti kwa usalama wa raia, mali na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, maslahi ya Askari Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu kuhakikisha inaboresha maslahi ya Askari wetu kwa kuwapa mishahara bila kukosa, kuwapa posho ya chakula, nyumba na kadhalika bado tatizo kubwa lililopo ni maslahi ya Askari wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali itazame upya mambo yafuatayo:-

(a) Mishahara ya Askari iongezwe;

(b) Posho ya chakula iongezwe na itolewe kila inapofika tarehe 15 ya kila mwezi kuliko inavyotolewa sasa mwisho wa mwezi;

(c) Posho ya nauli za likizo na safari za kikazi kwa Askari zilipwe kwa wakati kama inavyofanyika kwa watumishi wengine;

(d) Vitendea kazi kwa Askari wetu, mfano, uniform kwa sasa baadhi ya Askari wananunua wenyewe. Hili liangaliwe na zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya kununua nguo za Askari Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto;

(e) Stahiki za Askari wanapostaafu zitolewe mapema ili kuondoa usumbufu kwa Askari wanaokaa muda mrefu bila kulipwa stahiki zao. Napendekeza taratibu za malipo na kila anachostahili Askari kupewa, kiandaliwe mapema kabla ya Askari kutoka kazini;

(f) Askari Polisi anapofiwa na ndugu wa karibu kama vile baba, mama, mke au mume, Askari hapati fedha ya rambirambi kama ilivyo kwa watumishi wengine; na

(g) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa rambirambi kwa Askari anayefiwa na ndugu wa karibu kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine.

Mheshimiwa Spika, makazi ya Askari Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji. Pamoja na kuipongeze Serikali kwa ujenzi wa makazi na vituo vya Polisi na pia kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 7 Aprili, 2018 wakati akizindua nyumba za Askari Mkoani Arusha, alitoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Askari ngazi ya chini ambayo fedha hiyo imesaidia kujenga nyumba 400 katika mikoa mbalimbali kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza kwenye hotuba yake. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, Serikali iandae mpango mkakati wa kujenga nyumba za Askari kwa kutumia rasilimali watu iliyopo katika Taasisi hizi kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo. Serikali ifufue kitengo cha ujenzi kilichopo katika Jeshi la Polisi na Magereza na kuwatumia wataalam wa ujenzi waliosajiliwa na Bodi ya Wahandisi; licha ya uchache wao wangeweza kusaidia kuboresha hali ya majengo kupitia kikosi cha ujenzi cha Polisi au Shirika la Uzalishaji Mali la Polisi; lakini wafungwa wanapangiwa kazi za jumla vituoni (general duties) na Askari wenyewe.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali itoe fedha tuweze kujenga nyumba za Askari kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Askari Polisi na Magereza walijenga nyumba zao wenyewe kwa kutumia rasilimali fedha kidogo na rasilimali watu katika taasisi hizo. Swali, pia ningependa kujua kama Askari analipwa posho ya nyumba; na ni kwa asilimia ngapi?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupongeza utaratibu unaotumika wa kuwapandisha vyeo Askari Polisi, bado lipo tatizo la baadhi ya Askari kutopandishwa vyeo kwa wakati, jambo ambalo linaleta manung’uniko yasiyo ya lazima kwa baadhi ya Askari. PGO ya Jeshi la Polisi inaeleza, Askari atapandishwa Daraja/cheo kila baada ya miaka mitatu endapo Askari anatimiza masharti kwa mujibu wa PGO.

Napenda kujua ni kwa nini wapo Askari ambao wanatimiza masharti ya PGO mpaka sasa wamekaa muda mrefu bila kupandishwa vyeo na wengine wanakaa kwenye cheo kimoja miaka zaidi ya mitatu hadi miaka 10 na wengine mpaka wanastaafu?

Mheshimiwa Spika, pia masharti ya upandishaji wa vyeo yamekuwa yakibadilika tofauti na Uhamiaji na Magereza. Hapa napenda kujua, sababu ni nini?

Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga blocks sita za makazi, ghorofa tatu zinazokaliwa na jumla ya familia za Askari 24 kutoka mikoa ya Mwanza, Bukoba na Musoma bado hazijakamilika toka mwaka 2010. Napenda kujua nyumba hizi zitakamilika lini ili Askari Polisi waweze kuishi humo na hasa kwa kuzingatia kuwa walibomolewa nyumba walizokuwa wakiishi? Pia Jeshi la Polisi lilikuwa na mpango wa kujenga mahanga katika kila Mkoa wa kuishi Askari wapya 96 katika baadhi ya Mikoa michache tu ila mahanga hayajajengwa. Napenda kujua je, mahanga yenye uwezo wa kubeba Askari wapya 96 kila Mkoa yatajengwa lini?

Mheshimiwa Spika, ningependa kujua je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ofisi za Polisi Mkoa na Wilaya ambazo hazijakamilika katika mikoa mbalimbali?

Mheshimiwa Spika, kuna vituo vya Polisi vimejengwa kwa nguvu za wananchi katika maeneo mbalimbali; mfano, Kituo cha mpakani mwa Malawi na Soko la Ileje na Kituo cha Malimbe Mwanzo: Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga mkono nguvu za wananchi ili vituo hivyo viweze kukamilika na kutumika? Jeshi la Polisi lilianzisha mpango wa kujenga nyumba za Askari katika baadhi ya Mikoa na Ofisi za Mikoa na Wilaya. Napenda kujua mpango huu umekwamia wapi?

Mheshimiwa Spika, swali, nyumba za Askari Mkoa wa Mara hazijakamilika na kutumika, tatizo ni nini? Nyumba za Askari Mkoa wa Mwanza hazijakamilika, tatizo ni nini? Ofisi mbalimbali zimeanzishwa, zimeisha kwenye misingi tu kama Manyara na Mara.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.