Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote kwa kuandaa hotuba hii na kuleta hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri ya kupunguza ajali za barabarani hapa nchini bado ajali za pikipiki zinatishia uwepo wa vijana na nguvukazi ya Taifa. Kwa takwimu zilizopo kwa miaka 10 tu, watu waliopoteza maisha kwa bodaboda ni 8,000, bado majeruhi, walemavu, yatima, wajane, wagane na jamii inayozunguka. Lazima Serikali kuja na mkakati mahsusi wa kupunguza/ kuondoa ajali za bodaboda zaidi ya mafunzo na elimu wanayotoa.
Mheshimiwa Spika, fedha inayotengwa kwenye vituo vya polisi kwenye wilaya zetu kuendesha shughuli za kila siku ni ndogo sana na kusababisha polisi kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Polisi wanapewa lita tano za mafuta kwa siku kwa patrol kwenye eneo kubwa kama Kaliua haiwezi kukidhi kabisa kazi zao kwa siku – matokeo yake matukio ya uhalifu yanatokea pembezoni, taarifa zinafika kituoni kwa muda lakini askari hawawezi kwenda kufuatilia kwa sababu hawana mafuta. Polisi wanaomba mafuta kwa watu binafsi au kwenye ofisi za halmashauri, wakipata waende, wakikosa wakae kimya. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mafuta yapo?
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto kwenye wilaya nyingi hawana ofisi wala magari ya zimamoto, hawapo kabisa. Matukio ya moto yanatokea mara kwa mara nyumba zinateketea bila msaada wowote. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha wilaya zote zina ofisi za zimamoto na magari ya zimamoto yapo?
Mheshimiwa Spika, Wilayani Kaliua Jeshi la Magereza limechukua eneo la kujenga gereza la ekari 12 katika Kata ya Ushokora, Kijiji cha Pozamoyo kwa miaka sita sasa hakuna chochote pale kilichofanyika, hata watu waliohamishwa kwenye maeneo yao na kuacha mashamba yao hawajui hatma yao. Serikali ina mpango gani kuhusu eneo hili lililotengwa tangu 2012? Wananchi waliohamishwa maeneo yao nini hatma yao mpaka leo hawajui/ hawana pa kuishi, lini watalipwa fidia za maeneo yao?
Mheshimiwa Spika, spidi ya utoaji wa vitambulisho vya uraia inakwenda taratibu sana na gharama za utekelezaji wa mradi huu zinaongezeka kila mwaka kwa namna ambayo muda unakuwa mrefu. Kwa kuwa mradi huu ulitengewa fedha nyingi tangu mwaka 2012 kwa sababu ya umuhimu wake na kuhakikisha Watanzania wanapata vitambulisho vya uraia. Serikali ieleze Bunge time limit/ time frame ya zoezi hili muhimu kwa usalama na haki za raia wote wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi pekee ambayo mipaka yake mingi iko wazi na watu wa nje wanaingia kinyemela na wengi wanaishi humu ndani kama raia bila vyeti vya uraia. Wengine wamegombea nafasi za uongozi ndani ya nchi na wanaongoza watu leo. Vitambulisho vya uraia ndiyo mwarobaini wa tatizo hili, kila Mtanzania apate kitambulisho cha uraia.