Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Newala Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia hoja hii muhimu sana ya Wizara hii ambayo ni uhai wa Taifa letu. Nataka nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyowezesha Jeshi la Polisi kutekeleza kazi zake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza mdogo wangu Mheshimiwa Kangi Lugola anavyotekeleza majukumu yake kama Waziri wa Mambo ya Ndani. Pia nataka niwapongeze watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kuna majeshi ya kila aina katika Wizara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, nataka kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi katika nchi hii. Nitatoa mifano ya namna gani Jeshi la Polisi limetunusuru katika majanga ambayo tulikuwa nayo katika nchi hii. Tabia ya binadamu ni kusahau, ndiyo maana kila siku tunakwenda Msikitini, tunakwenda Kanisani kukumbushwa mambo. Siyo kama hatujayasikia, lakini kwa sababu tunasahau, ndiyo maana tumepangiwa kila Jumapili na kila Ijumaa twende kusali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge, natoka Mtwara. Ili utoke Mtwara kwenda Dar es Salaam lazima upite Ikwiriri – Kibiti. Tulivamiwa Kibiti - Ikwiriri na watu ambao hatuwajui. Watu wengi wameuawa, usiku kulikuwa hakupitiki, Jeshi la Polisi limepambana, Kibiti kumetulia, Ikwiriri kumetulia, sisi watu tunaotoka Kusini tunapita Ikwiriri - Kibiti hata saa nane usiku, hakuna tatizo. Kazi hiyo imefanywa na Jeshi la Polisi.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, katika nchi yetu hii kuna mapori makubwa yaliyopo katikati ya Mji na Mji; Kasulu, Kibondo, mabasi yakitembea hasa giza likiingia lazima Askari wa Polisi wa-patrol kuhakikisha kwamba tunakuwa salama. Wanafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, wale ambao wanabeza kazi ya Polisi, kaa, tafakari, hebu jiulize itokee siku moja Jiji la Dar es Salaam halina Mapolisi kwa muda wa nusu saa, hakuna Mapolisi wa kuongoza Traffic Dar es Salaam, badala ya kuwa traffic jam itakuwa imesimama kabisa. Polisi wanafanya kazi nzuri. Polisi wamepunguza ajali katika nchi hii. Ajali zimepungua, Mapolisi wanafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa umri wangu, jana nimeumia sana kuona kwamba watu wanasimama hakuna hata ile shukrani. Halafu jambo lingine nimelishangaa kwa utu uzima wangu, watu wameuliza maswali juu ya raia waliokufa ambao hawajulikani waliko; lakini hakuna aliyesimama anasikitika Mapolisi waliouawa wakiwa kazini wakifanya kazi ya kututetea sisi. Kwa mwendo huu mnataka kuwafanya vijana wakati mwingine sasa waseme eeh, kumbe ukienda Jeshi la Polisi wewe ni target? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wetu wengi wamepoteza maisha, siyo kwamba walikuwa wanalinda shamba la baba yao; siyo kwamba walikuwa wanalinda duka lao; walikuwa wanatulinda sisi Watanzania wote bila kubagua wewe umetoka Mtwara, umetoka Lindi, umetoka Kilimanjaro, umetoka Kigoma nakadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Nchi hii bila Polisi; hapa tu jioni magari yajae, maana yake leo watakuwepo watu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kama atapita na Inshallah atapita. Magari yatajaa hapa. Ili tutoke hapa, bado mnataka Askari Polisi kutuondoa tu hapa Ukumbini. Je, Dar es Salaam! Kwa hiyo, nasema Traffic wanafanya kazi nzuri, mimi nimesimama hapa kuwapongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Polisi hawa wanaitwa Askari wa Usalama wa Raia. Usalama wa Raia maana yake wanaangalia usalama wetu sisi. Sasa jana hapa palikuwa na hotuba za lawama tele, Polisi hawafanyi hiki, fulani amepotea hatujui aliko; sijui imekuwaje! Polisi anafanya kazi ya kulinda nchi hii kwa kusaidiwa kupewa taarifa na raia wema ili wafuatilie waweze kubaini ni watu gani wanauchafua usalama wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tunaambiwa na tumepewa namba kwamba bwana una jambo la kuwataarifu Polisi? Piga hiyo namba. Hupigi namba; tangu mwaka 2018 tumemaliza bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, watu wamekaa kimya, hawana mawasiliano na Polisi, hawajawapa taarifa ya Polisi, wanasubiri leo hotuba ya Mheshimiwa Kangi Lugola, waseme tena fulani hatumwoni na fulani ilikuwa hivi; na fulani. Umewapa taarifa Polisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Polisi walivyo wachache, sisi Watanzania tuliobaki milioni 55 ondoa hiyo idadi ya Polisi ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na hao milioni 55, watawezaje kupata taarifa kama sisi wakereketwa wa nchi hii, wenye uchungu wa nchi hii hatuwapi taarifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusisitiza hapa, tuwape taarifa ya ushirikiano Jeshi la Polisi. Polisi pekee hawawezi kufanya yote ya kulinda usalama wa nchi yetu kama sisi hatutawapa taarifa. Kuja hapa na kutoa tu hotuba fulani hatumwoni, fulani kaibiwa, fulani imekuwa hivi, umewapa taarifa Polisi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi sitaki malumbano, nimesimama hapa kueleza kwamba tuna haja ya kushirikiana na Jeshi la Polisi ili nchi yetu izidi kuwa nchi ya amani na usalama. Siyo vizuri kutoa tuhuma humu dani bila kuwapa taarifa Jeshi la Polisi ili waweze kufanya uchunguzi, waweze kufuatilia kwa sababu Polisi kwa kawaida yao, wamesomea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nataka kuzungumza habari ya utawala bora, imegusiwa hapa na pale. Ndugu zangu na Watanzania huko mliko, niwatoe hofu Watanzania wenzangu, Tanzania tuko salama. Nchi yetu, vyombo vya usalama vimedhibiti. Niambieni Afrika Mashariki yote hii leo, nchi gani watu wakipata matatizo ya vita kwao, wakipata civil war, wapi wanakimbilia kama siyo Tanzania? Hivi Tanzania pangekuwa mahali pa vurugu mechi wangekimbilia? Wanakimbilia Tanzania kwa sababu ni nchi ambayo ina amani, tuko shwari, vyombo vyetu vinafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana juzi niliumia hapa, mmoja akataka mjadala, tumjadili CDF kasema hivi. CDF kasema tu jamani eeh, sisi tutawafuatilia wakorofi wote, tukiwapata, tutawashughulikia. Hivi Askari kazi yake nini? Si kughulikia maadui wa nchi? Ukaja mjadala humu, CDF tumjadili; mnajadili nini? Askari tunapoapishwa na Rais, tunakula kiapo cha kulinda nchi yetu. Alichosema yeye na wanajeshi wenzake, wataendelea kulinda nchi yetu ili isichezewe. Ikawa nongwa. Unakuja mjadala humu! He! Freedom ya kukaa tunamjadili CDF aliyesema kwamba tutashughulika na wote wanaoleta chokochoko katika nchi yetu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimalizie, maana dakika kumi naona ni chache. Upande wa utawala bora, nataka kuzitoa takwimu hizi; Watanzania tuna tabia ya kubenza mafanikio yetu. Tuko tayari kusifu mambo ya wenzetu lakini yetu hatusifu. Ndiyo maana hata humu ndani hata wenzangu wale wenye interest za mpira, ukimwambia panga timu ya mpira wa Ureno, atamweka goalkeeper, yote iko kichwani; lakini mwambie Taifa Stars juzi walicheza nani na nani? Hajui. Ndiyo tulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niseme upande wa utawala bora; na hapa uniruhusu kusoma. Nataka kusema, kwa utawala bora sisi katika nchi za Afrika tunang’ara. Maana mengi yaliyokuwa yanazungumzwa hapa ni ya kubeza utawala bora uliopo katika nchi hii. Kiashiria cha transparence International, hili ni NGO moja ya ki-International, inaeleza habari ya utawala bora dunia mzima. Wanasema kwamba Tanzania tunafanya vizuri. Tumepanda katika utawala bora, tulikuwa nafasi ya 193, sasa tuko nafasi ya 99, wanasema kwa utawala bora Tanzania iko juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu wa Afrobarometer hawa wanasema mwaka 2014 ilionesha kuwa asilimia 66 ya waliohojiwa walisema kuwa kiwango cha rushwa kimeongezeka; mwaka 2017 wakasema kiwango cha rushwa kimepungua, watu asilimia 85; TWAWEZA wakasema Tanzania utawala bora umeongezeka, rushwa imepunguza. Wale REPOA wakasema hivyo hivyo. Tungeweza kutoa mifano mingi sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKTI: Nimekuongezea dadika tatu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa huruma yako. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ndugu zangu, Watanzania tujivunie mafanikio tuliyonayo. Tanzania kama isingelikuwa nchi ya amani, mbona tuna wakimbizi hapa? Wamekimbia kwao. Mbona hawajakimbilia nchi fulani, mbona hawajakimbilia na nchi fulani na nchi fulani? Wamekimbilia Tanzania kwa sababu hapa wakija hakuna ile unamwona tu fulani, kabila gani huyuo ua! Kabila gani huyo, ua! Utawala bora nchi hii uko juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na matatizo hapa ya mauaji ya Albino, tumepambana, nchi imetulia; mambo hayo bado wapo mmoja mmoja, lakini na hao mipango tumeiweka kwa usalama wa nchi hii, hatutaki mtu auawe tu kwa sababu ni kilema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono hoja. Nawaomba Wabunge wenzangu, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, Polisi wanafanya kazi nchi hii. Polisi na vyombo vyote vya usalama vinafanya kazi nchi hii, ndiyo maana ukipewa fursa ya kuongea, unaongea jinsi unavyotaka. Nchi nyingine wanavyoongea baadhi ya watu hapa, ilikuwa ukitoka tu hapa tayari anakusubiri pale uende ukakae ndani huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu mnaongea huru hapa, mnaongea mambo mengine ya ajabu ajabu, Mheshimiwa Rais ananunua vitu, amekuwa yeye ndiyo mnunuzi. Mmeambiwa hapa, Mheshimiwa Rais hajaenda shopping hata siku moja kwa ndege za Serikali, wala kwa jambo lolote la Serikali, vitu vyote vimenunuliwa kwa taratibu za manunuzi ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.