Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza ni-declare interest, mimi ni mwalimu na mdau wa shule binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa maamuzi ya kutoa elimu bure nchini, na sisi tunaona na kama walimu tunaona kabisa namna ambavyo hali ni nzuri sana kwenye shule za msingi vijijini huko, wilayani, mkoani, mambo ni mazuri sana. Na hii inasababisha hata kuongezeka kwa uandikishaji na namna ambavyo Form One wanakuwa wengi, Form Five, kwa kweli hali ni znuri sasa tumebaki tu kwenye ule ubora wa elimu (quality education) ndilo tatizo ambalo kidogo naomba Serikali niweze kuingia kuwashauri katika upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, dada yangu na rafiki yangu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako, kwa kweli ni mtu ambaye ukienda kwenye dawati lake ukimueleza jambo anashaurika, pamoja na Naibu Waziri, na inatusaidia sana kupunguza baadhi ya kero. Ukienda ukimwambia Mheshimiwa kuna hiki na hiki kwa kweli anafuatilia na mambo yanakwenda vizuri, na ndiyo maana mmeona hata kelele zimepungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani siku kama ya leo wamiliki wa shule binafsi wangekuwa Dodoma hapa zaidi ya mia wanalalamikia mambo yanayoendelea kutokea huko, lakini baada ya kuingia Waziri huyu na Naibu wake wameweka dawati maalum pale Wizarani, pamoja na Katibu Akwilapo, wameweka baadhi ya viongozi, kamishna wanakaa pamoja wanajadili mambo ya kero zinazoendelea kutokea kwenye shule binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwaka jana kwamba elimu ni ya wote, Serikali ina shule, Wizara ya Elimu ina shule, shule za mazoezi za sekondari na za primary, lakini TAMISEMI ina shule nyingi sana kwenye halmashauri huko na wadau; TAPIE, TAMONGSCO nao wana shule. Kwa hiyo, kwa pamoja nikawa nimeshauri kwamba tupate chombo fulani hapa juu kitakachokuwa kinamulika hizi shule zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani nilitoa hilo wazo mwaka juzi, mwaka jana nikarudia, na mwaka huu naendelea kushauri. Tupate chombo kitakachokuwa kinaangalia mifumo ya elimu nchini, kwamba shule za TAMISEMI zikaguliwe na chombo hicho, shule za Serikali zikaguliwe na chombo hicho na shule za binafsi zikaguliwe na chombo hicho kuliko kuacha Serikali yenyewe inajikagua yenyewe inafanya kila kitu yenyewe halafu inakwenda na kuwakagua wenzao, wakiharibu ndiyo wanawafungia, hii sio sawa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kuendelea kumshauri Waziri, pamoja na hizi changamoto ambazo zipo za kitaaluma, za ubora wa elimu nchini, hebu tupeni nafasi na sisi tuwe tunawashauri mambo yatakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Elimu Nchini. Kwa kweli Idara ya Ukaguzi – sasa hivi wanaita Udhibiti. Sasa hivi kwa kweli nimeona kwenye bajeti ya Waziri mtajenga ofisi, mtaongeza na magari, nimefarijika sana kwa sababu hii idara naifahamu vizuri sana, bila ukaguzi shuleni huko hakuna kitakachokuwa kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wenzetu hapa, hata Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kuhusu walimu wa Sayansi. Ni kweli kabisa huko shuleni, kwa sababu wanaotakiwa wakaone walimu wa Sayansi hawapo, vipindi vinafundishwa, lesson plans zinaandaliwa, ni wakaguzi ambao ndio wadhibiti ubora, naomba muwawezeshe wafike katika shule, wafike vijijini muwape wagari wakakague shule halafu walete ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndicho nilichokuwa nasema, kwamba hiyo ripoti kwa sababu wewe ni Serikali unajikagua mwenyewe ripoti unapeleka wapi? Tupate chombo ambacho hicho sasa ndiyo mtakuwa mnapeleka hizo ripoti ili hiyo ripoti inakuja inawasema jamani hapa ni pabaya, hapa ni pazuri, ndiyo hasa hoja yangu ya kusema kwamba tutafute chombo ambacho kitakuwa kinaangalia hizi shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti VETA; miaka minne iliyopita tulikuwa tuna mpango wa kujenga VETA kila wilaya, na wakati ule ikiwa Wilaya ya Chunya tulichagua mahali fulani tujenge VETA, panaitwa Mkwajuni ambapo sasa hivi ndiyo Jimbo la Songwe. Sasa hii hoja sijui imekimbilia wapi, naona wanatangaza vyuo vya VETA 16 hapa lakini ile Mkwajuni haipo, Wilaya ya Songwe sasa sijui imetupiliwa mbali, sijajua. Kwa hiyo, ninaomba tayari tulishatafuta uwanja, hatimiliki tayari ipo ekari 100, mtuletee VETA pale Songwe, wilaya mpya kwa sababu kitika vigezo ilikuwa inakubalika, kwamba kuna migodi, kuna Ziwa Rukwa, kuna kilimo, kuna misitu ambavyo ndiyo vitu hasa vinavyosababisha tuweze kupata VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shangazi kidogo amejaribu kutafuna zile points ambazo nilikuwa nimeziandaa, lakini ntazirudia tu katika ubora wa kiualimu kwa sababu yeye sio mwalimu, mimi ngoja nizirudie upya. Kuhusu TET, Taasisi ya Elimu Tanzania, wanaochapisha vitabu; kwa kweli naweza nikasema, nitumie neno kwamba majanga bado ni makubwa, Mheshimiwa Waziri naomba tupia jicho pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu nitoe mfano mdogo tu; mwaka juzi Bunge tuliamua, na Mheshimiwa Waziri alitamka, vitabu vyote ambavyo vilikuwa vimeletwa shuleni vimesambaa vilikuwa vibovu vikatolewa, aidha kama mmechoma, hamkutuambia mmepeleka wapi, mlivitoa, na sisi shule za private na sisi tukavitoa tukawa tumekula hasara kwa sababu sisi tulinunua, shule za Serikali waligawiwa bure ila sisi tulinunua kwa fedha zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikawa nimemwambia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati ule alikuwa bwana nani yule, nikataka kuandika barua, wenzangu walisema kwamba tuandike barua tuiambie Serikali na sisi watugawie bure kwa sababu makosa waliyafanya wao na sisi tulinunua kwao. Kwa hiyo, naomba hoja hii niilete tena mwaka huu, na leo nitashika shilingi kwenye kipengele cha Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vitabu vyote ambavyo shule za private tulinunua vikaonekana ni vibovu tukavitoa, shule za Serikali zimeshagawiwa tayari bure na sisi tupewe bure kwa sababu tuligharamia aidha, mturudishie fedha zetu kwa sababu tulinunua kwenu ninyi wenyewe na mkaviharibu ninyi wenyewe, kwa hiyo naomba baadaye nitashika shilingi, leo nina shilingi kama tatu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyosema Darasa la Kwanza hadi la Tatu hakuna vitabu vya lugha ya kiingereza kwenye shule za English Medium, amesema Mheshimiwa Shangazi hapa. Na Waheshimiwa Wabunge mjue watoto wenu wengi, asilimia 80 ya Wabunge mnasomesha watoto huko, hata Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wengine pale Wizarani, mnasomesha watoto huko; hatuna vitabu. Wanachofanya walimu wa shule za private ni kuchukua kitabu kilichaondikwa Kiswahili Histori wanakwenda kufanya translation. Sasa mwalimu wa History hajui kiingereza ila anajua History, anajua content ya Somo la History kwa kiingereza lakini hajui Lugha ya kiingereza kwa hiyo tunawapotosha watoto kule shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hii Taasisi ya Elimu kama imeshindwa kazi warudishe kama mfumo wa zamani kuwapa ma-publishers private ili mambo yaweze kwenda vizuri. Naongea kama mwalimu na kama nina shule ambaye naona kule tunahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jamaa mmoja yuko pale Iringa ni muuzaji wa vitabu vizuri sana, nimemsahau jina lake. Anasema tuna miaka miwili tunatafuta vitabu havipo, na Serikali ilitoa mwongozo na waraka tuwe na text mode moja tu, yaani tuwe na kitabu kimoja nchi nzima tukitumie kama text book. Sasa umetu-limit tusinunue kwa publishers wengine, tunununue TIE, TIE huna sasa tufanyeje? Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri, fanya ziara pale TIE uhakikishe vitabu vinatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi Serikali ilifuta baadhi ya tozo kwenye shule za private, ilifuta tozo ya kodi ya zimamoto (fire) na ikafuata na SDL na kodi ya mabango, lakini bado watumishi wa Serikali wa halmashauri wanakuja kwenye shule kuwasumbua wamiliki na wengine mpaka wanawaweka na ndani, na Mheshimiwa Waziri ntakupa ushahidi, wanasumbuliwa sana. Hebu tupeni basi tamko leo, tupeni waraka – hili na lenyewe ntashika shilingi – mtupe waraka unaosema mwaka 2017 Waziri wa Fedha alifuta tozo hizi na hizi kwenye shule za private. Kwa nini halmashauri kule wanasumbua, ndiyo maana nimesema kuna disorganization kati ya halmashauri, wizara na wamiliki, tukae pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ungeweka dawati la dialogue au wewe mwenyewe na Katibu Mkuu. Kama tulivyokaa siku moja Serena pale; mimi, wewe, Mheshimiwa Rweikiza, Mheshimiwa Esther na wadau mbalimbali, tukakaa tukaongea mambo yakaenda vizuri. Tuwe tunakaa angalau mara mbili kwa mwaka mambo yatakwenda vizuri sana. Kwa hiyo, ninashauri Mheshimiwa Waziri tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine naomba niishauri Serikali, mpaka hivi ninavyoongea – na hii ntashika shilingi baadaye…

WABUNGE FULANI: Ziko kumi.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: …kabisa, ntashika shilingi. (Makofi)

MWENYEKITI: Unashika shilingi eeh!

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna chuo chochote cha Serikali kinachotoa mafunzo ya walimu au kuna mtaala wa shule binafsi kwa English Medium. Labda nirudie tena; Waheshimiwa Wabunge naomba mnielewe, nimetoka kwenye field najua; hakuna chuo chochote chenye mtaala wa English Medium hapa Tanzania na Serikali haijajenga chuo hata kimoja, ila vipo vyuo vinafundisha mtaala huo kwa Lugha ya Kiswahili lakini hakuna kwa English Medium, ndiyo tukiwachukua walimu Kenya tunakuja tunakumbana na matatizo makubwa sana ya namna ya immigration hapa Tanzania.

Naomba Serikali, katika hivyo vyuo Mheshimiwa Prof. Ndalichako unavyovikarabati tenga kimoja TET watengeneze mtaala wa kufundishia masomo ya English Medium kwenye shule za private, mtakuwa mmetuokoa. Nasema hayo kwa sababu najua shule zinahangaika namna ya kutafsiri… tunatasiri na mitihani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Unga mkono hoja basi. (Makofi)

Mheshimiwa, unga mkono hoja.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini nitashika shilingi kesho. (Makofi/ Kicheko)