Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kusimama katika Bunge hili na kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi lakini nimpongezee Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote katika Wizara hii kwa kazi nzuri wanazofanya. Nimesikiliza vizuri hotuba ya Waziri jinsi gani wamejipanga kuhakikisha wanaweka miundombinu salama kwenye suala la elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze ukurasa wa 8 wa hotuba ya Waziri ambapo amezungumzia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Katika ukurasa huo amezungumzia Chuo cha Mbinga na Chuo cha Nandembo kilicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Kama nitakuwa na kumbukumbu sahihi, Chuo kile cha Nandembo majengo yake yalijengwa mwaka 1947, majengo yale yalikuwa ya mission lakini yalikabidhiwa Serikalini kwa maana ya kuanzisha chuo mwaka 1978.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshawishika kusimama na kukiongelea chuo kile kulingana na mazingira magumu yalikuwepo pale. Waziri amesema kwamba anafikiria kutenga pesa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Nimesimama kwa ajili ya kutaka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba katika mwaka wa fedha 2017/2018 chuo kile walikitengea shilingi milioni 700 kama sijasahau kwa ajili ya kujenga karakana lakini mpaka leo nimesimama hapa pesa zile hazijanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuanzisha vyuo hivi ni kwa sababu siku za nyuma shule za sekondari zilikuwa chache. Watoto wanapomaliza darasa la saba walikuwa wanapelekwa kwenye hivi vyuo kwa ajili ya kupata stadi mbalimbali za kazi ikiwepo useremala, ufundi magari, cherehani, mapishi na mambo mengine mbalimbali. Cha ajabu na ambacho kinachonisikitisha naona sana kipaumbele si kwa vile vyuo, hatuwasaidii watu wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia chuo hiki ambacho nakizungumzia majengo yake ni chakavu. Mheshimiwa Waziri siku za karibu alikuja Mkoa wa Ruvuma kwa ziara Mheshimiwa Rais lakini nimwombe aje rasmi atembelee Halmashauri zetu za Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Halmsahuri ya Wilaya ya Tunduru ili ajionee mazingira yaliyopo. Katika chuo kile walimu wanaotakiwa ni 17 lakini tuna walimu watatu (3), hivi kweli tunakusudia kuwasaidia watoto kwenye lengo letu lile ambalo lilifikiriwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kutaka kuwasaidia watoto wetu kupata stadi mbalimbali ni vizuri tukaona umuhimu wa kutenga hata hao walimu ili kuwapeleka kwenye maeneo haya waendelee kusaidia. Pia itapendeza zaidi kuweka miundombinu na kujenga hizo karakana ambazo zitasaidia sana wanafunzi ambao watakuwa katika shule hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala ambalo wenzangu wamelizungumza la watumishi mbalimbali katika Wizara hii na hususani walimu. Nimeona hivi karibu Mheshimiwa Waziri Jafo akisema kwamba wameajiri walimu na amesisitiza walimu wale waende katika shule zile ambazo wamepangiwa. Sina hakika kama wameangalia matatizo yaliyopo kule. Kama kweli wameangalia matatizo yalipo kule sina shida lakini wamezungumza Wabunge wenzangu kuhusiana na suala la walimu na mimi naomba nisisitize kwamba mpaka hivi tunavyozungumza kwenye shule zetu walimu ni wachache, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaongeza spidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwanza kabla ya kuangalia wale walimu ambao walikuwa na vyeti feki na walimu hewa lakini siku za nyuma pia tulikuwa na upungufu wa walimu, kwa hiyo, tuna mapengo hayo ya kuhakikisha tunayaziba. Kwa hiyo, niiombe hii Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali sikivu kupitia Waziri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako hakikisheni jambo hili la kuajiri walimu linapewa kipaumbele. Hata sisi tulioko humu ndani kama siyo walimu tusingeweza kufika hapa. Kwa hiyo, jambo hili ni jema katika kuhakisha tunapanga walimu katika shule zile. Ukienda kwenye shule nyingine inasikitisha, shule inatakiwa walimu 10, 15 unaweza ukakuta walimu 2, hatuwasaidii watoto. Kwa hiyo, naomba sana tuzingatie hilo kupitia Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie suala nyumba za walimu, wenzangu pia wamesema na mimi naomba niseme walimu wetu walio wengi wanaishi katika mazingira magumu sana. Mazingira pia ya kufundishia yanashawishi pia mwalimu kuwa mzuri katika eneo analofanyia kazi. Niombe sana Mheshimiwa Prof. Ndalichako suala la nyumba za walimu na madarasa lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Ruvuma, sina hakika ns maeneo mengine lakini mpaka hivi ukienda unaweza ukakuta madarasa ambayo yameezekwa kwa nyansi. Ndiyo maana nimemuomba Mheshimiwa Waziri akimaliza bajeti hii afike kule aone hali halisi ili haya tunayozungumza Waheshimwa Wabunge kupitia vikao hivi basi hata yeye ataenda kuona uhalisia. Darasa moja watoto wa darasa la tano wanaangalia ubao upande mwingine, watoto wa darasa la sita wanaangalia upande mwingine. Unaweza ukaona ni kitu cha ajabu lakini hivyo vitu vipo katika maeneo yetu mpaka hapa tunapozungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kuhakikisha tunaondoa hizo changamoto. Yapo mambo mengi mazuri yanafanyika lakini palipo na mambo mengi mzuri lazima kuna changamoto na changamoto lazima kuzibaini na kuzitafutia ufumbuzi wake. Mheshimwa Waziri hali za elimu kule ni ngumu, nasisitiza sana mama yangu mpendwa uje mkoani uone si tu ukikaa pale ukitembelea Kigoma unakuta umemaliza mkoa njoo na Ruvuma uone hali ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Wakaguzi wa Shule. Suala hili Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamelisema na mimi naomba nisisitize jambo hili. Wakaguzi hawa wa Shule wana mazingira magumu. Kwenye Halmashauri zetu sisi Wabunge ni Madiwani unaona jinsi gani Wakaguzi hawaendi kwa mujibu wa ratiba kutembelea zile shule na kuangalia mwenendo mzuri wa elimu yetu. Nikuombe ipo haja sasa ya kuhakisha Wakaguzi wanapatiwa magari, mafuta na wanawezeshwa kwa namna moja au nyingine ili wafike kwenye maeneo mbalimbali ili tupokee taarifa zilizo sahihi vinginevyo tunaendelea kupokea taarifa zinazopikwa kila mwaka kwa sababu hawana uwezo wa kufika kwenye maeneo yale. Nalisisitiza hili naamini kabisa ni sehemu ya kuboresha elimu yetu, elimu ya msingi pia ya sekondari, nasisitiza sana Wakaguzi wana hali ngumu katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kupandishwa vyeo walimu, nina hakika ni haki ya mtumishi kwamba anapostahili apate lakini wengi wamekuwa wakilalamika na hawapati fursa hizo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri toa maagizo katika maeneo yanayohusika inapofika wakati mwalimu anastahili kupandishwa daraja, apandishwe kwa sababu ni haki yake. Katika maeneo mengine walimu wamekuwa wakilalamika kwamba anatakiwa kupandishwa daraja lakini hapandishwi, tunawakatisha tamaa walimu wetu kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la uhamisho wa walimu. Naamini Wizara hii inategemeana na Wizara ya TAMISEMI. Tunalo tatizo, walimu wengine na hasa maeneo ya vijijini wanakaa kule kana kwamba ni adhabu. Mwalimu anamfundisha mama mtu, mtoto mtu, mjukuu mpaka anazeeka kwenye shule ile ile. Inafika mahali inaonekana kama kuna upendeleo fulani katika uhamisho wa walimu. Niombe tuzingatie na tuwaangalie wale walioko vijijini, tutoe motisha kwa walimu wetu ili waendelee kufanya vizuri. Inapoonekana kwamba nay eye anatakiwa apate uhamisho basi ni vizuri ahamishwe aende maeneo mengine lakini anakaa anamfundisha mama/baba mtu, mtoto mpaka mjukuu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga nkono hoja, ahsante sana. (Makofi)