Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. nami naomba kuchangia hii Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Leo nitakuwa nachangia pole pole sana lakini nitamwomba pia Mawaziri watakapokuwa wanahitimisha, nao wajibu pole pole wala wasi-panic na wala wasiwe na mpango wa kuvua nguo kama Waziri mmoja alivyosema atavua nguo. Naamini watajibu vizuri. Nataka twende vizuri kabisa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja ya kwanza kamba wanafunzi wanaohitimu darasa la saba kila mwaka, kwa takwimu ambazo tunazo wanakadiriwa kuwa milioni moja, lakini wanaojiunga kidato cha kwanza kwa maana ya shule za Serikali na shule za private wanakadiriwa kuwa 300,000 tu. Wanafunzi 700,000 na kitu inaonekana wanabaki nje, hawako private wala Government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia wanafunzi 700,000 ni wengi sana na kwa lugha nyepesi uchukulie ule uwanja wa Taifa ambao unajaa watu 60,000 mara 12 hawa watu wote wanabaki nje, hatujui wanakokwenda ni wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo inawezekana na inajulikana kabisa kwamba watoto wanaohitimu darasa la saba wengi wao wana umri mdogo sana. Wengi ni chini ya miaka 14, wengine 12, 13 wakizidi sana ni miaka 14, lakini hawa wengi wanabaki nje kama 700,000 na kitu hivi. Sasa kwa nini Serikali isitafute utaratibu wa hawa angalau waanze kurudia mtihani kwa utaratibu maalum tu, ambao ni maalum kabisa, kwamba waruhusiwe kurudia mtihani wa darasa la saba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini hata hapa wako Wabunge wengi, hata baadhi ya Mawaziri ambao walirudia mtihani wa darasa la saba kwa majina ya watu wengine. Hatuwezi kuwataja majina, lakini wapo kwa utaratibu ambao siyo maalum. Sasa kwa nini Serikali isihalalishe suala hili liwe ni suala ambalo ni maalum kabisa kabisa ili kusudi wanafunzi hawa wengi wasibaki mtaani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunahangaika, kwa mfano, wapo baadhi ya makundi yanaibuka nchini tunasikia panya road, sijui nani; ni watoto wadogo sana hawa. Sasa kwa nini Serikali isianzishe utaratibu ambao ni maalum waweze kurudia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwa sababu idadi hii ni kubwa sana, kwa nini Serikali isianzishe utaratibu waende kwenye Vyuo vya VETA kupata mafunzo ya ufundi umeme, ushonaji na mafunzo mengine ili Serikali iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi hawa kama ambavyo inatoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu? Kwa nini wasifanye hivyo? Kwa sababu tunaamini kwamba vyuo vyetu vya VETA viko vingi sana nchini, kwa hiyo, wanafunzi hawa wanaomaliza darasa la saba wanaweza wakapelekwa huko VETA Serikali ikawapa mikopo na wakalipa, kwa sababu mkopo unalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iweze kuliangalia hili. Mheshimiwa Ndalichako nimekwambia kwamba leo nitakushauri polepole na baadaye ujibu vizuri polepole kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu mishahara pamoja na motisha kwa Wahadhiri pamoja na Wakufunzi wa Vyuo. Juzi wakati nachangia Wizara ya Mambo ya Ndani nilizungumza na leo pia naomba niseme tu kwamba bado Waheshimiwa Wabunge tusiwe na utamaduni wa kulalamika. Yaani wananchi wametupa kura, hiki ndiyo chombo kinachofanya maamuzi, linapokuja suala la kujadili bajeti ya Wizara fulani Wabunge huwa tunajifanya wazalendo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini Wizara hii ya Elimu pamoja na kwamba Wabunge wengine wamechangia na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na ninyi mko wengi sana, anzisheni utaratibu mzuri tu tuweze kuongeza mishahara kwa Wahadhiri wetu. Sisi upande huu tutawaunga mkono. Ninyi ndio wengi. Utaratibu, wakati mwingine Mabunge huko nyuma wamewahi kurudisha bajeti isipitishwe. Bunge limewahi kuamua miaka ya nyuma huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu wakati huu tunapozungumzia bajeti ya Wizara ya Elimu tunazungumzia makusanyo pamoja na matumizi. Kwa hiyo, tunaweza ndio wakati muafaka huu. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi mko wengi sana, ninyi ndio mnaopitisha akidi ya kila kitu. Kwa hiyo, hili pia tunaweza tukalijadili, sisi wa upande huu hatuna shida. Hata nikiwauliza Wabunge wa upande huu nyoosheni mikono ambao mnasema tuongeze mishahara kwa Wahadhiri; wengi sana.
(Hapa baadhi ya Wabunge walinyoosha mikono)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Unaona! Wako wengi sana; lakini nikisema nyoosheni kule, hata mmoja hatanyoosha. Kwa hiyo, niseme tu kwamba hili liko mikononi mwa Wabunge wa CCM na mishahara ya Wahadhiri iweze kuongezwa pamoja na stahiki zao mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninapozungumza na wewe Wahadhiri kwa taarifa tulizozipata, wameanzisha mgomo wa chini chini, kwa sababu hata zile fedha za nyumba ambayo ni stahiki yao hazipelekwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tutaenda kupata wanafunzi wa aina gani? Mhadhiri anaamua kumkamata mwanafunzi...
MWENYEKITI: Acha uchochezi wewe, Mheshimiwa! (Kicheko)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mhadhiri wa leo anaenda kumkamata mwanafunzi wakati mwingine kwa sababu tu yule mtu ana stress, ana msongo wa mawazo kwa sababu hela za nyumba zao hizo hajapewa na ni stahiki yao. Sasa mambo kama hayo Serikali iweze kuangalia. Shida ni nini? Wapeni hela zao, waongezeni mishahara, boresheni mambo yao yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la utegemezi wa miradi ya maendeleo kwenye fedha za wahisani. Imekuwa ni kawaida, Wizara hii ya Elimu kuomba fedha nyingi kutoka kwa wahisani kuliko fedha zaa ndani. Natoa mfano mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018/2019 bajeti hii ambayo tunaimaliza sasa, yaani fedha za maendeleo kati ya shilingi bilioni 502 fedha ambazo tulikuwa tumeomba kwa wahisani ni shilingi bilioni 311 sawa na asilimia 62. Hizo zilikuwa ni fedha za nje. Fedha za ndani zilikuwa ni asilimia 38 tu, ndio zilikuwa za kwetu za ndani. Fedha hizo za wahisani ambazo zilikuja hadi sasa ni shilingi bilioni 111 kati ya shilingi bilioni 311.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niulize. Kwa mfano, unapoenda kuomba fedha aidha kwa mtu mwingine, unataka labda kujenga nyumba au kufanya jambo lolote la maendeleo, unaomba nyingi au unaomba kidogo, au wewe unazo nyingi unatakiwa uongezewe? Sasa Serikali yetu tunaomba kwa wahisani shlingi bilioni 311 sawa na asilimia 62, halafu sisi eti asilimia 38. Hii ni aibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu ndiyo tunaenda kuonesha utegemezi wa hali ya juu sana. Mwaka huu katika fedha za maendeleo shilingi bilioni 413, tunaomba kwa wahisani shilingi bilioni 279 sawa na asilimia 68. Fedha za ndani mwaka huu ni asilimia 32 tu, lakini wakati huo huo hawa wahisani ndio mmekuwa mkiwaita mabeberu. Yaani mnapoomba fedha mnasema ni wahisani, wanapowashauri namna ya kuendesha nchi na mambo kwenda vizuri, mambo demokrasia, mnasema mabeberu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, ukiangalia kule nyuma kabisa ukurasa wa mwisho kabisa kule amewashukuru hawa ambao tunawaita wahisani hawa, lakini wakati mwingine mnawaita mabeberu. Inabidi mwaombe msamaha. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri anasema, napenda pia kushukuru baadhi ya mashirika yaliyochangia kufanikisha Programu za Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ni pamoja na Benki ya Dunia, DFID, SIDA, Umoja wa Nchi za Ulaya, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Jumuiya ya Madola, Global Partnership in education, United Nations, International children’s, (UNICEF)...
WABUNGE FULANI: Mabeberu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani pale mmetaja wengi, UNESCO, USAID...
WABUNGE FULANI: Mabeberu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Sasa wote hawa wanapokuwa wanatuchangia tunasema ni wahisani…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado dakika mbili.
MWENYEKITI: Hapana. Ahsante sana.