Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kuweza kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Naanza na Mitaala ya Elimu. Mitaala yetu ya elimu bado ni tegemezi, haioneshi ni namna gani mwanafunzi anapomaliza shule anaweza kujitegemea mwenyewe kimaisha. Mwanafunzi pengine anamaliza anakuwa na degree ya engineering lakini akitoka pale hana uwezo wa kutengeneza hata baiskeli. Wanafunzi wanakuwa si wabunifu, elimu wanayopata inakuwa ni ya theory zaidi kuliko elimu ya vitendo. Kwa hiyo, nashauri Serikali ihakikishe kuwa, wanafunzi katika vyuo wanapata zaidi elimu ya vitendo kuliko theory ili wanapotoka pale wanafunzi wetu waweze kujitegemea wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea, ilikuwa ikifika time kuna vipindi wanafunzi wanatolewa darasani wanakwenda kufundishwa namna gani ya kulima. Wanafundishwa kutengeneza mbolea, kutengeneza pengine shamba linakuwa kutoka pengine mche wa mgomba mpaka kufikia mwingine pana urefu wa mita ngapi, wanatengeneza mashimo yanakuwa na ukubwa gani, wanaweka mbolea mpaka kima gani, mwanafunzi anapomaliza shule anakuwa ni mkulima mzuri sana na anaweza kujitegemea. Kwa hiyo nashauri tuige mambo ya namna hii ili wanafunzi wetu wanapotoka vyuo waweze kujitegemea wenyewe siyo tena wawe bado ni tegemezi kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka kuchangia kuhusu shule za private. Shule hizi za private tunazipenda sana na zinatusaidia sana lakini kwa kweli baadhi ya shule watoto wengi wanaharibika hasa watoto wadogo. Kunakuwa na ulawiti mkubwa katika shule hizi za private, hasa shule ambazo zinachukua watoto wadogo, watoto wanaharibiana wao wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri awaite hawa walio na shule za private, wamiliki wa shule za private, wawape elimu wajue kama wanafunzi wanaowachukua ni wadogo kwa hiyo watoto wanapokuja pale wengi wao wanakuwa na tabia tofauti katika majumba yao. Baadhi ya wazazi wanakuwa wale watoto wameshawashinda kule nyumbani, kwa hiyo mtu anaamua bora nimpeleke boarding. Anapokwenda kule anakutana na watoto wengine wana tabia nzuri, lakini kwa sababu wale wana tabia mbaya wanaanza kuwaharibu na wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawashauri walio na mashule haya ya private wahakikishe kila bweni, kuwe kuna mtu ambaye analala nao watoto anawaangalia. Watoto wanaharibiwa usiku wanapokwenda chooni, watoto wakubwa wanawasubiri, wanawaharibu wadogo. Tutakuja kuzalisha watoto sisi tunaona watoto wetu wanakwenda kujifunza, kumbe wanajifunza mambo mengine ya ajabu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Elimu awaite watu walio na shule za private wahakikishe watoto wanawawekea ulinzi wa hali ya juu watoto wasiharibiane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitakwenda kwenye mishahara ya Walimu. Mheshimiwa Waziri asishangae kutuona kila anayenyanyuka anazungumzia suala la mishahara ya Walimu. Kama kuna watu ambao wanaishi katika maisha ya umaskini basi ni Walimu, Mwalimu anafikia kustaafu hana pa kukaa. Mwalimu siku zote anakaa katika nyumba ya kupanga, ikikaribia Januari Mwalimu kichwa chake hakifanyi kazi anafikiria ni namna gani atapata hela ya kwenda kulipia kodi ya nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Walimu wetu tukiwaongezea mishahara na stahiki zao tukiwapa, kidogo akili zao zitaweza kutulia kwa sababu atakuwa hana wasiwasi wa mambo mengine, ataweza kusomesha vizuri na tutapata mafanikio mazuri. Walimu wengi ambao wanafanya kazi katika shule za private, wanalipwa vizuri na ndiyo maana tukaona wanafunzi wanaofaulu wengi wanatoka katika shule za binafsi. Kwa hiyo ingawa hawa walio na shule za private isije ikiwa ni ile tunayosema Mgema akisifiwa tembo atalitia maji, wakaja wakaona kama kweli wao wanawalipa vizuri wakawashusha, hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali stahiki za Walimu ziongezwe, tuwaongezee mishahara ili anapokuwa darasani asifikirie watoto wake watakula nini, wala asifikirie mke wake atapata wapi nguo ya kuvaa au atapata wapi fedha ya kwenda kulipia nyumba ili akiwa pale atulie kabisa aweze kutoa elimu nzuri kwa watoto wetu na tupate ufaulu mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa nitajielekeza kuhusu ajira ya Walimu. Katika vyuo vyetu wanamaliza pengine wanafunzi kama elfu thelathini ambao wote wale wanakuwa tayari ni Walimu, lakini kwenye ajira wanaajiriwa pengine elfu kumi, wengine wanabakia mitaani, utamkuta mtu ameshasoma vizuri, ana uwezo wa kufundisha lakini anakwenda kufanya kazi ya majumbani, kwa sababu hana kazi ya kufanya. Kwa hiyo nashauri Serikali iongeze ajira kwa Walimu ili katika madarasa iwe hakuna vipindi ambavyo hakuna Mwalimu wa kusomesha pengine topic fulani, hapana. Kwa hiyo nashauri tuongeze ajira kwa Walimu, watoto waliomaliza vyuo ambao wamesomea elimu waajiriwe ili tupate Walimu wengi katika vyuo na watoto wetu waweze kufanikiwa vizuri katika elimu zao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umekwisha au bado. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako. Nilikuona karibu na eneo la Maganzo juzi, unaimarisha Muungano eeh! Mheshimiwa Rukia. Mmh! Nilikuona eneo la Maganzo.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam!
MWENYEKITI: Maganzo, ulikwenda kufanya nini? Ni kwenu huko, Muungano ule! Haya tunaendelea Mheshimiwa.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Maganzo nilienda kutembea.