Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza Waziri pamoja na Naibu wake wakiwemo Katibu Mkuu na Naibu wake pamoja na timu yote ya wataalam wa Wizara hii. Kwa kweli hotuba ni nzuri kwani imesheheni mambo mazuri ambayo yanaeleweka na sisi kama Wabunge kazi yetu ni kushauri pale ambapo kuna mapungufu na ndivyo ambavyo nitafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nitakuwa sijatenda haki kama sitampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya ya kusimamia Serikali. Kama tunavyoona leo hii wanafunzi wanasoma bure kutoka shule ya msingi mpaka sekondari. Vilevile tunaona kuna utaratibu mzuri wa kutoa mikopo hata kama mapungufu yapo bado tutaendelea kushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanikiwa kwa wananchi ni kufanikiwa kwa taifa lakini kuwa na elimu pekee bila ujuzi bado siyo suluhisho la kufanikiwa kwa wasomi wa Kitanzania. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuishauri Wizara kuhakikisha kwamba inaweka mikakati ya kupitia mitaala iliyopo ili kuweza kutoa fursa kwa wanafunzi ambao wapo mashuleni kushiriki katika michezo lakini katika mafunzo ya kazi za mikono kama ushonaji, ufinyanzi pamoja na ujasiriamali. Kwa upande wa michezo nipongeze Wizara kwa kurudisha michezo ya UMISETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini nashauri hivi? Ni kwa sababu ni wakati wa nchi yetu kujitafakari na kuhakikisha kwamba tunaanza kutengeneza wasomi wasio na fikra ya kuajiriwa tu ila wasomi wenye fikra ya kujiajiri na kuweza kutengeneza ajira kwa wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu katika kipindi cha Ubunge wangu ndani ya miaka hii michache nimeweza kutembelea shule kadhaa kwa nia mbalimbali. Naipongeza Shule ya Sekondari ya Misungwi kwa sababu kwa kweli imekuwa ni ya mfano mzuri na ningetamani sana siku moja Mheshimiwa Waziri atakapokanyaga Mkoa wa Mwanza aweze kufika pale ili aone. Kwa kweli shule hii imekuwa ikitoa mwongozo mzuri kwa wanafunzi wake vilevile imekuwa ikiwaandaa kwa ajili ya maisha baada ya masomo chini ya Mwalimu Mkuu Mr. Mbando kwa kweli ni mbunifu na anahitaji pongezi na shule ile inahitaji motisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ile ina club ya ujasiriamali, wanatengeneza sabuni za maji na mbolea za maji na wanafundisha wanafunzi ujenzi wa nyumba za machupa ya plastiki. Kama haitoshi wanawafundisha wanafunzi wao wa jinsia ya kike kuweza kutengeneza taulo za kike ili waweze kujisitiri katika siku zao. Vilevile kama haitoshi kupongeza kwa hayo imekuwa na Fema Club ambayo imeongoza nchini kwa miaka kadhaa. Kwa hiyo, tunahitaji walimu wabunifu kama hawa na ni mategemeo yetu kwamba hata pale ambapo promotion zinatokea kutoka kwenye ualimu kwenda kwenye Uafisa Elimu, walimu kama hawa akina mwalimu Mbando ndiyo wanaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu kwa walemavu, kwa kweli bado haliridhishi, wanafunzi wenye changamoto ya ulemavu ni wengi, shule hizi zimekuwa ni chache mno. Kwa mfano kwa Mkoa wa Mwanza zipo shule tatu tu ambayo ni Shule ya Mitindo iliyoko katika Wilaya ya Miswungwi, kuna shule mbili za Wita na Itumbili katika Wilaya ya Magu. Kwa kweli shule hizi ni chache kulingana na mahitaji. Na uchache huo unalazimisha wanafunzi ambao wana changamoto ya ulemavu kwenda kwenye shule za kawaida ambazo hazina miundombinu inayowafaa, lakini vilevile hakuna wataalam wanaoweza kuwaelimisha vizuri kwa kiwango ambacho kinahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile shule hizi pamoja na uchache wake bado kuna upungufu mkubwa wa hostel. Nikitoa mfano wa shule ya Itumbili iliyoko Magu ina wanafunzi 105, lakini katika hao ni 48 tu ambao wanaweza kuwa accommodated katika mabweni. Kwa hiyo, tunaona umuhimu wa kuongeza hostel katika mashule haya, na ukiangalia wanafunzi wengi wanatoka umbali mrefu, wengine ni wa kubebwa, wanapelekwa shule kwa kubebwa, wengine wanatembea kwa shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwa Wizara hii kwamba iweze kuangalia changamoto hiyo. Kama Mbunge wa vijana kwa nafasi yangu nimeweza kuwafikia mpaka sasa wanafunzi 26 ambao nimeweza kuwagawia baiskeli za watu wenye ulemavu ili waweze kufika shuleni. Sasa najiuliza, kama Mbunge nimeweza kufika hao watu, kwa Serikali hii ambayo inatoa elimu bure ni kwanini isiweze kuwafikia wanafunzi hawa ili at least waweze kupata baiskeli za kuwafikisha shuleni. Mheshimiwa Prof. Ndalichako, ni imani yangu unapokuja kuhitimisha nitasikia neno kuhusu hilo, kama tunaweza kutoa elimu bure na kama tunaweza tukatoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ni kwanini tusiweze kuwasaidi wanafunzi hawa ambao wanaenda hata kwenye shule za kawaida kwa mwendo mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia kuhusu mikopo nikakumbuka kwamba lipo suala la kipaumbele katika utoaji wa mikopo. Tumeona wanafunzi ambao wamefaulu kwenda vyuo vikuu ambao wanatoka kwenye mazingira magumu wakipata mikopo, wakipewa kipaumbele, lakini tumeona wanafunzi ambao wanasoma masomo ya ualimu na masomo ya sayansi wakipewa kipaumbele. Ni kwanini wanafunzi hawa wenye ulemavu wasipewe kipaumbele katika utoaji wa mikopo pale ambapo wanafaulu kwenda shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na upungufu wa hostel kama ambavyo nimesema hapo awali, kwa wanafunzi wenye ulemavu bado kumekuwa na upungufu mwingi katika shule hizi. Kwa mfano mashine za kupima usiku, vitabu vya nukta nundu, karatasi za kuandika nukta nundu, vifaa...
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri, mengine utaandika. Mheshimiwa Fatma Toufiq.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja na mengine nitawasilisha kwa maandishi. (Makofi)