Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami kuchangia hii hoja iliyopo mbele yetu. Naomba nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Watendaji wote kwa kuandaa hotuba hii ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii pia kuungana mkono na Wabunge wote wa chama tawala na watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi hii kwa kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure ambayo pia ni lengo namba nne la maendeleo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilichangia bajeti ya elimu, naomba nichukue fursa hii kuishukuru sana Serikali yangu kwa kutekeleza baadhi ya maombi ambayo sisi kama Wabunge tuliomba Serikali hii iyafanye. Nikichukulia mfano katika Mkoa wa Dodoma, mazingira ya utendaji kazi katika udhibiti wa elimu kwamba Wizara imetoa kiasi cha milioni 152 kwa ajili ya Wilaya za Chemba, Bahi, Chamwino na Jiji kwa ajili ya kujenga Ofisi za Wadhibiti Ubora wa Elimu, pongezi sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, pia zimetolewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi za Udhibiti Ubora wa Elimu katika Wilaya za Kongwa na Mpwapwa. Naomba niwatie shime, niwatie shime watendaji wa Wizara chini ya uongozi wa Waziri, pamoja na kelele zote ambazo mnaambiwa kwamba Serikali haijafanya kitu kwenye suala la elimu naomba mtembee kifua mbele watanzania tuko pamoja na ninyi, mnafanya kazi nzuri sana pamoja na ufinyu wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambayo nilikuwa naomba niishauri Wizara ijaribu kuona inaifanyia kazi, hasa kwa suala la watumishi wa walimu waliopo Wizara ya Elimu, wengi wamekuwa wakicheleweshewa kupandishiwa madaraja kwa muda mrefu. Nikichukulia kwa mfano, mwalimu aliyeanza kazi TAMISEMI mwaka mmoja pamoja na mwalimu aliyeanza kazi Wizara ya Elimu ngazi zao za mishahara zinatofautiana. Kwamba huyu wa TAMISEMI yuko TGTS I, wakati wa Wizara ya Elimu TGTS G, hii inapunguza sana ari ya utendaji wa kazi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri hili mlione ili kusudi sasa muweze kuwapandisha waalimu hawa madaraja kwa muda ambao unaotakiwa. Kwa sababu imetokea pia kuna baadhi hata wakati wa kustaafu wamekuwa wakitofautiana kupata yale mafao kwa hiyo hii inakuwa inawakatisha sana tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nilipenda kufahamu kwanini Wadhibiti Ubora wa Elimu hawapati posho ya madaraka? Kwa sababu wao ndiyo wanaokuwa wakiwakagua hawa waalimu katika shule lakini cha kushangaza ni Waalimu Wakuu, Waratibu Elimu Kata ndiyo wanaopata posho. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake, nilikuwa naomba ajaribu kunieleza, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora katika ngazi ya wilaya na ngazi ya kanda nao wanaweza kupata fursa ya kuweza kupata posho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 129 hadi 130 ya hotuba hii amezungumzia kuhusiana na suala la elimu ya ufundi, kwamba Wizara ina mpango wa uendelezaji wa elimu ya fundi study kwa muda mrefu ambao watatoa washiriki 10000 lakini kwa muda mfupi watakuwepo washiriki 24000. Ushauri wangu kwa Wizara, kwa kuwa kuna baadhi ya shule za msingi zina vituo vya ufundi study, hebu Wizara ione kwamba vituo hivi vifufuliwe wapewe walimu wawepo, vifaa viwepo pamoja na bajeti iandaliwe ili kusudi vituo hivi viweze kufanya kazi kwani vina msaada mkubwa sana katika maeneo ya vijijini. Kutokana na vituo hivi tunaweza tukapata mafundi mbalimbali kutoka hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 25 wa hotuba hii pia Waziri amezungumzia kuhusu suala la kuimarisha study za utoaji ushauri na unasihi kwamba kuna waalimu 300 watapewa mafunzo hayo. Nilikuwa naomba niishauri Serikali kwamba hawa walimu wawe wengi zaidi kwa sababu suala la ushauri na unasihi linahitajika sana kuanzia shule za msingi hadi shule za sekondari na hadi vyuo. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali iangalie kwa upya zaidi na kuongeza bajeti katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nilikuwa naomba nizungumzie kuhusu elimu maalum. Sisi katika Mkoa wa Dodoma tuna Shule ya Buigiri, wasiiona. Nilikuwa niiombe Wizara waone sasa umuhimu wa kuweza kutupatia vitabu vya kutosha hasa vile vya nukta nundu kwa sababu bado kuna upungufu wa vitabu hivi ili watoto wetu waweze kupata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa waalimu wengi wamelizungumzia, na mimi naomba nilizungumzie…

MWENYEKITI: Kengele ya pili tayari, malizia.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Hili ni tatizo la kitaifa, lakini pia upatikanaji wa fedha za kutosheleza. Baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)