Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na leo tuko hapa Bungeni tunachangia hoja za Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, napenda kutoa pongezi kwa wafuatao. Pongezi za kwanza napenda ziende kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuwatumikia Watanzania na kwa moyo wake thabiti ambao umeonesha kubadilisha maisha ya Watanzania na dunia imeona na imekubali kwamba sasa tunaye Rais ambaye atakwenda kubadilisha nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Prof. Ndalichako na Makamu wake Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi nzuri ya kubadilisha elimu yetu nchini kwa kufuatilia mambo mengi ambayo yalikuwa hayaendi vizuri katika Wizara ya Elimu. Nawapongeza sana na ninawaombea Mungu mwendelee kufanya kazi kwa ajili ya maslahi ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kuchangia mawili, matatu kuhusu Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa, Wizara hii ya Elimu imekuwa ikijitahidi sana katika kuboresha elimu, lakini lipo tatizo kubwa ambalo limekuwa tunaenda nalo sasa kwa muda wa miaka mingi. Tatizo hilo ni tatizo la wanafunzi kumaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika. Wengine kwa sababu siku hizi ni multiple choice, wanafikia kwenda sekondari lakini hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili limekuwa ni sugu, linahitaji tulifanyie upembuzi na labda iundwe Tume ambayo itashughulikia tatizo hili. Kama mtakumbuka, hapo nyuma hata Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, alisema iko haja ya kukaa mezani kuangalia matatizo ya elimu nchini Tanzania. Kwa maana hiyo, ni kwamba wale watoto ina maana wanakuwa wamemaliza miaka saba wakitembea pale shuleni lakini hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaweza tukaangalia jinsi ya kutatua hili tatizo. Kwanza, elimu ya watu wazima iboreshwe ili waweze kwenda kule wakajifunze kusoma na kuandika. Zaidi ya kuboresha, vijijini kwetu kuna wananchi wengi sana Watanzania ambao hawajui kusoma na kuandika. Hata unapokwenda kwenye vijiji vya wafugaji, kule mkoani kwangu Katavi kuna wafugaji, kwa hiyo, wale wana tabia ya kuhama hama na majority yao hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kile Kitengo cha Elimu ya Watu Wazima ambacho najua kwamba kipo lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 nimeona hakijaelezea sana. Naomba uangaliwe utaratibu wa kuboresha namna ya wananchi ambao hawajui kusoma na kuandika ili waweze kujiunga na hii elimu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati tunakua, miaka ya 1970 mpaka 1980. Elimu hiyo ilikuwa na mkazo na watu wengi walijua kusoma na kuandika kupitia elimu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la kuboresha maslahi ya walimu. Kwa mfano, kule mkoani kwangu Katavi, Jiografia ya Makao Makuu ya Wilaya ni mbali. Unakuta kuna kilometa kama 150 kutoka kwenye kijiji kwenda kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Mwalimu huyu anapanda basi au bajaji ama kitu chochote, anakuja Makao Makuu ya Wilaya ambayo yapo kilometa 150. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Elimu iangalie utaratibu ambao inaweza ikaboresha maslahi au ikawapa marupurupu walimu wanaofundisha vijijini ili wawe na interest ya kwenda kufundisha vijijini. Tukichukulia tu kwamba mwalimu anayefundisha mjini anapata maslahi sawa na mwalimu anayefundisha vijijini, kwa kweli naona kwamba hii ina-demoralize katika kufundisha. Nafikiri kwamba si vizuri, tujaribu kuangalia tunaongeza marupurupu gani kwa walimu wanaofundisha vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika kuboresha elimu, maana nimesema kwamba wanafunzi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika; hii ni kwa sababu wanajaa darasani. Darasa moja lina watoto 200. Naomba Wizara ya Elimu iangalie ni utaratibu gani tutaufanya kuongeza ujenzi wa madarasa? Kwa sababu kipindi cha kufundisha darasani ni dakika 40. Mwalimu mmoja hawezi akafundisha watoto 200 kwa dakika 40. Ina maana wale ambao ni cream ndio watakaojua kusoma na kuandika, wale wenzangu mie watabaki nyuma, watakuwa wanasindikiza darasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuboreshe pia kwa kuongeza maslahi ya walimu na kwa kujenga madarasa mengine mapya, lakini nguvu hii pia tuwashirikishe wazazi pamoja na TAMISEMI kwa pamoja tunaweza kujenga madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni maabara zilizojengwa. Wananchi walitumia nguvu yao kubwa, walichanga michango mingi, karibuni kila shule imejenga maabara, lakini hizo maabara hazina vifaa. Niiombe Wizara ya Elimu iangalie, hili tatizo italiondoaje? Shule nyingi zina maabara, hata kule Katavi kuna shule zina maabara lakini hazina vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo tulikuwa tunavitumia sisi, unaenda kwenye chumba cha sayansi unakuta kuna Bunsen burner, na kadhalika. Hivyo vifaa ni vigumu kwa shule kuvinunua na kuviweka kwenye maabara. Naomba Serikali iangalie ni jinsi gani itasaidia. Majengo mengi sana yamejengwa kwenye shule, maabara zimejengwa lakini hazina vifaa. Naomba Wizara ya Elimu iingilie kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu shule za ufundi. Naomba ili kutatua suala la ajira nchini, tuongeze shule za ufundi. Pia, kuna zile shule ambazo zilikuwa ni shule za wazazi. Kwa sababu zile shule za wazazi ziko karibu kila mkoa, zingeweza kugeuzwa zikawa Shule za Ufundi ili watoto wetu waweze kujifunza na waweze kutoka wakiwa wameelewa kitu chochote kama ni kujenga, kushona na kadhalika ili waweze kujiajiri kwa sababu Serikali kama ilivyo hatuwezi tukaajiri wanafunzi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la ajira nchini. Tuangalie ni mbinu gani tutazitumia ili kutoa tatizo la ajira nchini kwa kuzitumia shule za wazazi ambazo nafikiri ziko katika kila Mkoa. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho anaweza akaniambia ni shule ngapi za wazazi ambazo ziko. Ninaamini kwamba kila Mkoa una shule za wazazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni watoto wa kike, ambapo kiutaratibu Wizara huwa inapeleka pesa kule za kujikimu watoto. Hizi pesa kwa sababu watoto wa kike wana matatizo yao ya maumbile ya kibaiolojia, naomba sana Mheshimiwa Waziri, lile fungu lisigawiwe sawa na mtoto wa kiume kwa sababu mtoto wa kikeā€¦ (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)