Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika suala la kubadilishwa kwa mitaala bila ya kufanya utafiti wa kina na wala kushirikishwa kwa Walimu ambao ni wadau wakubwa sana. Hili ni suala lililozoeleka kwa kipindi sasa, pia mtaala umejikita kuwakaririsha wanafunzi. Kwa mfano kwa upande Zanzibar sidhani kama Walimu wanashirikishwa ipasavyo. Hata hivyo, mitaala ikibadilishwa haipatikani kwa muda muafaka, tukizingatia wanafunzi wa Zanzibar wanafanya mitihani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa form four na form six.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri, Mheshimiwa Ndalichako atuambie hii ni Wizara ya Muungano ama vipi. Kama sio kuna makubaliano yoyote waliyofanya na Wizara ya Elimu ya Zanzibar ama Serikali, ni yapi? Mbona hatuoni ofisi za Wizara ya Elimu ya Muungano kama ilivyo kwa TRA na Wizara ya Mambo ya Ndani. Kama zipo, Unguja ipo wapi na Pemba wapi? Je, Waziri ameshawahi kutembelea mara ngapi? Kwa nini Walimu walipwe na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar badala ya kulipwa na Serikali ya Muungano na kuzingatia wanatumwa na Serikali ya Muungano na kwa utofauti mkubwa wa mshahara wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yote hayo si masuala ya Muungano kwa nini Zanzibar tusiachiwe kuwa na mitaala yetu na kutunga mitihani wenyewe? Naomba Mheshimiwa Waziri anijibu masuala haya ili kuondoa ukakasi uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu waongezwe mishahara na kupandishwa madaraja kwa wakati na kupewa stahiki zao kwa wakati. Hii itasaidia Walimu kufanya kazi kwa ufanisi, tukizingatia wanatuzalishia viongozi. Tusikubali wafanye kazi katika mazingira magumu na msongo wa mawazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa uhaba wa Walimu wa sayansi, hiki ni kilio cha nchi nzima, kwa mfano katika wilaya nzima utakuta Walimu wa sayansi wawili mpaka wanne, hii ni hatari kubwa. Waziri atuambie ana mkakati gani madhubuti wa kupata Walimu wa sayansi. Pia ina mkakati gani wa kuongeza wanafunzi wa kike kwenye masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupatiwa majibu na naomba kuwasilisha.