Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kukushukuru wewe na Mwenyezi Mungu, Mungu muweza wa yote kwa kuniwezesha kusimama na kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu ya elimu, sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono kwa sababu Waziri Profesa, Mama Ndalichako, Naibu Waziri Olenasha, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ave Maria, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Wahadhiri, walimu na wafanyakazi mnaofanya kazi nzuri sana kwa bidii na maarifa, wavumilivu, waaminifu na kwa uadilifu mkubwa na pia taarifa imeandaliwa vizuri, ina data za kutosha zinatuonyesha wapi tulikotoka na wapi tulipo na wapi tunakwenda, ninawapongeza sana. Naomba tuendelee kuwatia moyo, niendelee kuwatia moyo, endeleeni kuchapakazi, tuna imani kubwa nanyi na Mungu atawabariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Wizara ya Elimu; Utekelezaji wa Fedha za Miradi ya Maendeleo ya Matumizi ya Kawaida; pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kupeleka fedha za mishahara, matumizi mengineyo ya fedha na miradi ya maendeleo kwa kiwango cha asilimia 60 ya Fungu Namba 46, naungana na uchambuzi wa Kamati kuwa lipo tatizo la upelekaji wa Fedha za miradi ya maendeleo ya fedha za matumizi ya kwaida.

Mfano, asilimia 37 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya Wizara ya Fedha ambayo haikidhi kutekeleza kazi zilizopangwa na asilimia 62.8 haitoshi kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa na hivyo basi kusababisha kushindwa kulipa fedha za nyumba za Wahadhiri, kukamilisha miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa. Mfano, Chuo Kikuu Kishiriki cha DUCE na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kama ambavyo taarifa ya Kamati imeeleza. Ushauri:-

(a) Upelekaji wa fedha; naomba niungane na maoni yaliyotolewa na Kamati kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya sekta hii zipelekwe zote kama zilivyopitishwa na Bunge kabla ya mwaka wa fedha haujamalizika.

(b) Kubuni vyanzo vya mapato; pia nichukue nafasi kushauri Taasisi za Wizara hizi kuendelea kubuni vyanzo vya ndani ili kutekeleza miradi ya maendeleo na shughuli za uendeshaji kama ilivyofanyika katika vyuo vya DUCE na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kama ambavyo Wajumbe wa Kamati tulijionea na leo taarifa imewasilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Sayansi ya Kilimo na Tekonolijia; ilani ya CCM, ukurasa wa …. Ibara ya 52, Kifungu cha (k)(2) imetamka bayana kuwa katika kipindi cha 2015-2020, Serikali ya CCM itakamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi Shirikishi cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Butiama) lengo ikiwa ni kuenzi wazo la Baba wa Taifa ambaye yeye siyo kutoa wazo yeye na Ndugu zake, Watima walitoa eneo tena bure wakaanza kujenga miundombinu ya maji, Bwawa la Kialano n.k.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupongeza Serikali kwa kazi zinazoendelea kama ambavyo Waziri ameeleza kwenye ukurasa wa 85 wa hotuba yake.

Mheshimiwa Mwenyakiti, maswali - Hati ya Kiwanja; hati ya kiwanja inapatikana lini? Na kiasi cha fedha kilitengwa na ujenzi unaanza lini? Naomba Waziri utakapokuwa unajibu tusaidie kujua ili wananchi wa Wilaya ya Butiama (Mara) na Watanzania kwa ujumla wasikie kwa sababu lengo la CCM la kuanzisha Chuo hiki siyo tu ni kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu pia ni kuongeza wataalam katika sekta ya Kilimo na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bila malipo; napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya wanawake ninaowaalika kuleta shukurani nyingi kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za zaidi ya kiasi cha milioni 23 kwa ajili ya kugharamia elimu na kuwezesha watoto wa familia za wanawake na watanzania wanyonge, watoto hao kupata fursa ya kusoma bila vikwazo. Pamoja na pongezi hizo, naomba kushauri yafuatayo:-

(a) Mpango endelevu wa elimu bila malipo - Serikali tubuni chanzo cha mapato cha uhakika cha kutekeleza mpango huu kama ilivyo kwenye umeme vijiji na kwenye barabara.

(b) Ujenzi wa miundombinu; Serikali ishirikiane na wananchi kujenga miundombinu kama vile madarasa, mabweni, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia na vya kujifunzia, kuendelea kuongeza walimu hasa walimu wa masomo ya sayansi, upatikanaji wa madawati n.k kwa sababu kwa sasa kuna baadhi ya shule darasa moja na wanafunzi 60 mpaka 200.

(c) Vyuo vya VETA; naipongeza Serikali kwa kuendelea kujenga vyuo vya VETA katika Mikoa na Wilaya mbalimbali hapa nchini. Nashauri tuendelee kuongeza miundombinu ya vyuo vya VETA ili viwe na uwezo wa kuwapokea vijana wengi zaidi kuliko ilivyo sasa.

(d) Serikali iendelee kukamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya zote hapa nchini na kuanzia tuanze na wilaya zenye miundombinu ya majengo, vilivyokuwa vyuo vya wananchi kama vile Wilaya ya Bunda, Kisangwa, Chuo cha Wananchi-Bweri, Musoma Mjini n.k.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoro shuleni na mimba za utotoni; pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Bunge kutunga Sheria kali kwa wale wote watakaomzuia mtoto kusoma kwa namna yoyote, hili tatizo la utoro limeendelea kuwa kubwa sana pamoja na mimba za utotoni. Ili kupunguza utoro shuleni, suala la chakula kwa watoto liwekewe mpango maalum unaotekelezaka. Ushauri wangu kwa Serikali, naomba suala hili la utoro mashuleni Serikali na jamii tulivalie njuga kwa kutumia Sheria hiyo tukakomesha utoro na mimba shuleni kwa sababu upo ulegevu wa utekelezaji wa Sheria hiyo kwa kisingizo hakuna ushahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Bodi ya Mikopo; naomba kumshukuru Rais wetu kipenzi cha Watanzania kwa kutambua changamoto ya fedha za mikopo na kufanya suaa la kutoa fedha za mikopo kuwa ni mambo ya vipaumbele katika mipango ya Serikali ya kugawa rasilimali ya Taifa. Jambo ambalo limewezesha sasa Bodi ya mikopo kutoa mikopo kwa vijana wetu 1,227,583 mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 424,758,636,617.00, kukusanya madeni ya shilingi 128,076,510,388.48 sawa na asilimia 81.2, kati ya fedha 1577 zilizokuwa zinadaiwa. Pongezi nyingi sana. Pamoja na pongezi naomba kushauri yafuatayo:-

(a) Naomba Serikali iwe na mipango mizuri hata ya kujidhamini katika Mabenki kupitia mtaji tulionao ambao Serikali imekwishautoa ili suala la mkopo liwe kwa vijana na watoto wetu wote wenye uhitaji.

(b) Utaratibu wa elimu za ujazaji fomu ya maombi ya mikopo itolewe kwa watoto wote waliopo kwenye shule za sekondari na elimu kupitia mitandao mbalimbali ili kutoa fursa kwa vijana na wazi kuwa na uelewa wa pamoja juu ya vigezo vya kupata mikopo na utaratibu wa kujaza fomu na kuzifikisha katika Taasisi kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu katika vyuo vikuu; pamoja na kazi nzuri inayofanyika ya kujenga miundombinu katika vyuo vyetu hapa nchini. Ningependa kujua Je, Serikali imejipangaje kujenga Mabweni katika vyuo vya ufundi vya Vyuo Vikuu ili kuondokana na changamoto inayokabili vijana wetu hasa wasichana kushindwa kulipa kodi katika nyumba wanazopanga, kutembea umbali mrefu n.k. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga miundombinu, barabara na majengo yenye hadhi ya jina la Chuo – Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.