Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha nami kufika mahali hapa na kuchangia Hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2019/2020. Hotuba hiii inakwenda kutekeleza Ilani a Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoelekeza hususani katika kukuza sekta ya elimu kwa kutoa elimu bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu na masuala mazima ya teknolojia. Halikadhalika nitumie nafasi hii kwa mara nyingine tena kumpongeza Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa hatua kubwa ilizofikia katika sekta ya elimu, uandikishwaji wa wanafunzi wapya katika mfumo rasmi wa elimu nchini unaonesha kuwa hadi Machi, 2019 wanafunzi wa elimu ya awali walioandikishwa ni 1,278.816 sawa na asilimia 92.48 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,382,761.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kati ya hao walioandikishwa wanafunzi 1372 ni wenye mahitaji maaulum. Vilevile wanafunzi wapya walioandikishwa kuanza darasa la kwanza ni 1,670,919. Kati ya hao wanafunzi wenye mahitahi maalum walioandiishwa ni 3028, hatua nzuri na ya kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naipongeza Wizara pamoja na ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa kuendelea kushirikiana na wananchi na wadau wa maendeleo katika kuboresha miundombinu ya shule za awali na msingi. Takwimu zinaonyesha hadi februari 2019 ujenzi wa vyumba vya madarasa 2840 kwa shule za msingi umefanyika na kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa 2637 viko katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti vilevile jumla ya matundu ya vyoo 7067 vyoo vya wanafunzi matundu 6445 na vyoo vya walimu matundu 622 yamejengwa katika shule za msingi na kuongeza matundu ya vyoo kutoka 190,674 yaliyokuwepo Machi, 2018 hadi kufikia matundu ya vyoo 197,741 mwezi Februari 2019 hili ni ongezeko la asilimia 3.5. Aidha, matundu ya vyoo kutoka 3004 yanaendelea kujengwa na yanatarajiwa kukamilika kabla ya Juni, 2019 ni mwanzo mzuri ambao mwelekeo wake ni kuhakikisha changamotoo zilizokuwepo zinakwenda kuisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali imeendelea kufanya kazi nyingine za uboreshaji miundombinu ya elimu zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu 720 na kuongeza idadi ya nyumba hizo kutoka 44320 mwaka 2018 hadi nyumba 45040 Februari, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, jambo lingine la kupongeza ni idadi ya madawati ya wanafunzi watatu watatu kuongeza kutoka madawati 2,858,982 yaliyokuwepo Machi,2018 hadi madawati 2,994,266 Februari 2019 sawa na ongezeko la madawati 135,284. Aidha, kupitia programu ya Equip-T, Serikali imetoa jumla ya vyumba vya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi yametekelezwa katika mikoa tisa yenye halmashauri 63. Yapo mengi sana yaliyofanywa na yanayoendelea kutekelezwa na Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi katika sekta hii ya elimu, naishauri Serikali kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali kwenye sekta ya elimu, hii ni kutokana na umuhimu wake hasa katika maendeleo endelevu ya kiuchumi na mapinduzi ya nchi ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kugusia sasa changamoto zinazohusu sekta ya elimu katika Jimbo la Kibaha Vijijini, ni mdau mkubwa wa sekta hii ya elimu, nimekuwa nikihamasisha wananchi wangu kuhakikisha wanachangia sekta ya elimu, halikadhalika na mwenyewe nikishiriki kama mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejitahidi kufanya mengi sana kwenye sekta hii na mengi hayo ni mazuri yenye tija, lakini bado Kibaha Vijijini tuna changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu, tuna changamto ya upungufu wa nyumba za walimu 342, upungufu wa vyumba vya madarasa 140, matundu ya vyoo 483 nadawati, ofisi za walimu 27 pamoja na samani za ofisi, naiomba Serikali katika bajeti hii kuliangalia hili na kuongeza fedha kwenye bajeti hii hasa katika halmashauri yangu ili kutatua changamoto katika jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, fedha husika zifike kwa wakati ili ziende moja kwa moja katika changamoto husika na kuzitatua. Aidha, tuna changamoto ya mabweni ya shule ya Magindu na bwalo la Shule ya Sekondari ya Soga na kupanda madaraja kwa walimu wetu, pamoja na walimu kupanda madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika bado pia kuna changamoto kubwa jimboni kwangu ya ucheleweshaji wa fedha za uhamisho wa walimu wetu pindi wanapopata uhamisho, hali hiyo imekuwa ikirudisha nyuma hamasa kwa walimu kwani fedha hizo za uhamisho zinapochelewa husababisha walimu kutokufika katika vituo vyao vya kazi kwa wakati,naiomba wizara kuifanyia kazi changamoto hii, na kwenye majumuisho ya majibu wakati wizara itakapotoa majumuisho naomba kupata majibu ya changamoto hii, ni lini walimu wangu wanaodai fedha za uhamisho watapatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.