Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba kuleta mchango wangu kwa maandishi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza pongezi zangu kwa Waziri na Naibu kwa kazi kubwa mnazofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yetu ya CCM, lazima tujikite katika kuandaa mitaala ambayo itawapa fursa wanafunzi wanaohitimu waweze kuwa na skills ambazo zitawafanya waweze kujiajiri au kumudu kuendesha maisha yao binafsi katika mazingira ya sasa ya ushindani. Wanafunzi wengi wanaomaliza vyuo na elimu za kawaida za sekondari, wamekuwa wakitegemea sana kupata ajira rasmi kutoka katika taasisi za Serikali na binafsi. Jambo hili limepelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la nguvu kazi mtaani ambayo haitumiki kwa maana ya kwamba hawana ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufike wakati muafaka sasa Serikali yetu iandae mitaala ya namna ya kuwapa elimu ya kujitegemea wahitimu wetu ili wapate technical skill ambazo zitawasaidia kujiajiri au kujitegemea. Hapa tunaweza kupata wahitimu wakaandaliwa katika vikundi mbalimbali tukawapa mikopo ya mitaji hawa ambao tumewaandaa vema ili waweze kuanzisha miradi ya kujiajiri na kujitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulimaliza shule za msingi na kulikuwa na mafunzo ya elimu ya kujitegemea kama vile uselemara, umeme, ufundi wa magari na kadhalika. Naishauri Serikali yangu kuhakikisha watoto wetu wanaohitimu wanapata skills ambazo zitawasaidia kujiajiri na nchi pia kupata wataalamu ambao tutaweza kuwatumia katika viwanda ambavyo tunavihamasisha vijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naishauri Serikali kupitia mfumo wa kuhakiki vyeti vya wanafunzi wanaoomba mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ambapo kwa sasa utaratibu umetolewa kwa waombaji wanaoomba kupitia online kulazimika kuhakiki vyeti jambo ambalo naona ni kuwapotezea muda na gharama watoto wa Kitanzania. Nashauri Serikali irudishe jukumu la kuhakiki vyeti lifanywe na Bodi ya Mikopo yenyewe na liwe well-coordinated. Wanafunzi wanapoomba mikopo wanaambatanisha na vyeti vyao vya kuzaliwa moja kwa moja, Bodi ichambue na kupeleka majina na nakala za vyeti viweze kuhakikiwa na hivyo kuwasaidia watoto wetu kupunguza gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya ya Ikungi, sisi ni wazalishaji wakubwa sana wa alizeti hivyo uhitaji wa ujenzi wa vyuo vya ufundi hauepukiki ili kupata vijana wenye technical skills watakaojiajiri katika usindikaji wa mazao ya kilimo yanayopatikana katika Wilaya yetu. Naomba sasa ujenzi wa VETA utekelezwe katika Kata ya Minyughe, Wilaya ya Ikungi, mahali ambapo tayari tumeandaa eneo la ujenzi wa chuo hiki ambacho kitakuwa chachu ya maendeleo katika kuwasaidia vijana wa Kitanzania watakaokuwa na uwezo wa kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, natoa rai kwa Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuja na mkakati madhubuti wa namna ya kuandaa mkakati wa ujenzi wa nyumba za walimu nchini. Walimu wetu wanateseka sana katika kupata makazi ya kuishi hivyo kuathiri taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante.