Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi sina budi kuungana na wachangiaji wa awali kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa kazi nzuri. Ni pacha wangu kabisa lakini pia ni mwanangu, kwa lugha ya upendeleo naona kwamba tuna sababu sasa baada ya kuangalia andiko lake hili, ni kwamba kweli tunaingia katika awamu ya viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kusema kwamba mpango uliopo mbele yetu ukitekelezwa na ninaona kila nia ya kuutekeleza, utatupeleka mbele. Napenda tu nisimame hapa kuchangia kwa kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini na ninafahamu kabisa kinadharia kama mwanauchumi kwamba ili uwe na viwanda na Mheshimiwa Waziri analijua na atakaposimama kujibu atueleze, ni lazima viwanda vinaendana na kilimo, maana yake wanasema ni Agricultural Development na industrialization, hivi vina kwenda pamoja. Huwezi kuendeleza viwanda kama hujaendeleza kilimo. Hutapata malighafi ya ku-feed hivyo viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wachangiaji wengine, na mimi naomba nisisitize kwamba ni lazima tuwe na malighafi. Sasa mazao ambayo unayo, kwa mfano zao la sukari, mchele na alizeti; ukiniuliza mimi kwa uelewa wangu wa mambo kama mchumi, nitasema kwamba Taifa hili halina sababu yoyote isipokuwa katika hali ya dharura kukubali kuingiza sukari, mchele au alizeti kutoka nje. Kwa sababu mafuta, kama unataka industrialization na hii inaitwa nascent industrial development. Lazima uwe na mkakati wa kulinda viwanda. Kila nchi zimelinda, Marekani, Uingereza na Ulaya imelinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha zaidi sasa, Jumuiya ya Kimataifa katika WTO inatulinda sisi tulinde mazao haya. Mheshimiwa Waziri utakaposimama, una mwambata wako yuko Geneva ambaye anafuatilia mambo haya katika World Trade Organisation, under special and differential treatment for least developed countries. Mazao haya yamelindwa na Sheria za Kimataifa. World Bank wanapokuja hapa kutuambia tufungue milango, wanakuwa wanatuonea.
Kwa hiyo, katika zana ya biashara, hili nalo naomba lieleweke na Mheshimiwa Waziri utufafanulie utakavyofuatilia sasa na waambata wako wa biashara walioko Geneva ambao wanafuatilia mazungumzo ya Kimataifa kuhusu biashara duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri jambo hili litatusaidia sisi, kwa mfano mimi nasimama hapa kuzungumzia viwanda na biashara nikitoka pembezoni, Mkoa wa Kagera. Nadhani alikuwa Mheshimiwa Kubenea. Hapa ni lazima niseme kwamba na-declare interest nakubaliana na Mheshimiwa Kubenea kabisa kwamba sikuona mkakati wako kwa mikoa ya pembezoni. Watu wanasema Rwanda ni nchi ambayo haina bandari, lakini Kagera, Kigoma na Katavi ni mikoa ambayo haina bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwe na mkakati wa kusaidia mikoa ya mbali kuweza kufika bandarini. Mimi nafikiria suala ambalo Mheshimiwa Rais amelitilia mkazo na tunashukuru kumuunga mkono kwa nia yote, ni suala la hii standard gauge na reli inajengwa. Na mimi naomba niseme, reli hiyo ni lazima pia iwe na spur au mikondo inayoingia mikoa mingine ya pembezoni itakapokuwa inapita kusudi wote tuweze kuzifikia bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima hapa nikiri kwamba, Rais Museveni nataka nimpongeze kabisa, hatua hii tuliyofikia kwamba bomba la gesi sasa litapita Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua na naweza nikatoa taarifa kabisa kwamba Rais Museveni ilikuwa ni azma yake kwa sababu alikaa hapa Tanzania kama mkimbizi, alikaa Muleba pale kwako Mheshimiwa Waziri, Muleba Kaskazini, ndiye alikuwa anakaa pale anapigania uhuru. Sasa unaona kwamba ametoa shukrani, anatukumbuka na katika hilo lazima tumpongeze na tujipongeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali hiyo, tujipange sasa. Sisi walio wengi ni wakulima, wavuvi na wafugaji, na sisi ndio viwanda. Hivyo viwanda vitahitaji malighafi. Sasa mnatuwezeshaje? Mnatuwezesha kwa miundombinu, lakini pia mnatuwezesha kwa mifumo ya kuweza kuwafanya waingie kwenye uzalishaji wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema sukari isiingie, sukari ikiingia itaua viwanda vya sukari. Hata mtoto wa shule anajua hilo. Ili kusudi Watanzania wapate sukari ni lazima Wizara ya Kilimo iwe na utaratibu wa kuingiza sukari, lakini siyo kutumia wafanyabiashara. Wafanyabiashara wale ukiwapa nafasi wataingiza sukari ya zaidi na viwanda vyetu ndani vitakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa kwa mfano kiwanda cha Kagera sasa hivi hakizalishi kwa sababu mvua ni nyingi, mashine haziwezi kuvuna muwa, vitu kama hivyo.
Kwa hiyo, nataka kusema kwamba itatosha kabisa kwa sisi kuwasaidia wavuvi wetu wapate viwanda. Wavuvi sasa hivi wanahangaika kwa sababu ya nyavu, lakini pia na viwanda vya samaki vingi viko katika mikono ya watu binafsi. Mheshimiwa Waziri naomba uviangalie pia viwanda vya samaki, vinawezeshaje wavuvi? Viwanda vya samaki wenyewe havina utaratibu wowote wa kusaidia wavuvi, lakini utakuta hawapati bei wanayostahili na wakati mwingine mauzo hayaendi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishajipanga ndani, sasa tunajipanga nje; na dunia ya Kimataifa inatusubiri. Nimeona Mheshimiwa Waziri umezungumzia vizuri AGOA (African Growth Opportunity Act), lakini kama unavyojua, Tanzania inasuasua na AGOA. Hatupati faida yoyote. Ninaweza nikasema kabisa, nilipokuwa bado Umoja wa Mataifa kwenye Shirika la Biashara nilipoanzia kazi, Ulaya wametupa pia, AGOA ya Ulaya inaitwa ABA (All But Arms), unaweza ukaingiza kitu chochote Ulaya isipokuwa silaha. Hii ni trade offer waliyotupa, lakini kwa sababau hatujajiandaa…
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kengele ya kwanza eeh? (Makofi)
Sasa nataka kusema hivi, vijana wetu sasa; trade presupposes exchange of goods and services, yaani ni lazima muwe mnabadilishana kitu. Sasa vijana wetu wanapokuja kufanya biashara, tumewawezeshaje vijana wetu?
Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, naomba nisikie mkakati wako wa kuwasaidia vijana waanze kufanya biashara. Wale ambao wamemaliza darasa la saba lakini wana ujanja unaweza wakapewa hata tuition ya kuzungumza kiingereza kusudi waweze kwenda kufanya biashara, maana yake huwezi kufanya biashara za Kimataifa na wewe hujui lugha. Hiyo nayo tusidanganyane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina hawa sasa hivi wanajifundisha kiingereza kila mahali. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba kwa upande wa biashara, tujue yaani tunajiandaaje na masoko? Vijana wetu wanapomaliza form four, form six, chuo kikuu, napenda kuona mkakati Mheshimiwa Waziri unaposimama hapa kujibu, utuambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kabla kengele haijanigongea, Mkoa wa Kagera sisi tuko mbali; nimeshangaa kuona kwamba Omukajunguti haijatajwa hapa. Pale Mheshimiwa Rais Magufuli, alituahidi kwamba ataweka Export Processing Zone.
Sasa napenda kujua kwamba hii Export Processing Zone ambayo itatukomboa sisi Wanakagera kuweza kuingia kwenye horticulture kwenda kuuza mboga (vegetables), kama huna ndege huwezi. Kule Kilimanjaro wanafanya kwasababu kule kuna airport. Sasa kule Bukoba, huwezi. Hata ukienda kule kila kitu kwetu ni green lakini hamna miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huo ndiyo mchango wangu. Tunapozungumzia viwanda na biashara, Serikali hii imejipanga, napongeza sana juhudi za Serikali, naunga mkono hoja, lakini na mimi nimechangia kinadharia kwa kusema kwamba inaendana na sekta nyingine. Huwezi kuzungumza viwanda na biashara in a vacuum, lazima uangalie kwamba itakwendaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, naunga mkono hoja na kumpongeza mwanangu Mheshimiwa Mwijage, amefanya kazi nzuri.