Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa natoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pia napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napongeza kwa kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Ombi langu ni kwa ajili ya angalizo kwa wanafunzi waliotokea kwenye shule za private. Kigezo cha kutowapatia mikopo wanafunzi waliopitia shule za private, kuwanyima mikopo, nashauri lifanyiwe kazi. Wananchi siku hizi wamepata mwanga na wanapenda watoto wao wasome kwa hali yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wazazi wengine wanasomesha kwenye hali ngumu, hasa wenye mlezi mmoja kama mtoto wa mama ntilie au akina mama wengine wanadunduliza hela ili mtoto wake asome. Mimi ni shahidi Morogoro na mikoa mingine kuna akina mama wanasomesha watoto wao kwa kupitia kulima na kuuza mchicha au kwa kupika maandazi au chapati. Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana kigezo cha wanafunzi kusoma private kifanyiwe uchunguzi wa ndani, watoto wengine waliopitia mkondo huu wanapaswa kukopeshwa asilimia kubwa kwani hali yao ni duni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika kwa ukaguzi na kubaini vyuo vikuu venye upungufu kwa ubora wake kama Chuo Kikuu. Namshauri sana Mheshimiwa Waziri kuhusu ufuatiliaji wa mienendo ya vyuo hivi, ni muhimu kuliko kwenda kama zimamoto na kuvifunga vyuo (baadhi) kwa kutokuwa na ubora. Ni bora vyuo vikafuatiliwa na kupewa ushauri. Vyuo hivyo vikijirekebisha kufuatana na upungufu, viendelee na kutoa elimu kama kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo hivi hasa ni vya binafsi vikiwepo vingi vya dini. Vinapofungwa ghafla wanafunzi wanapata shida kwa kubadilishwa na kupelekwa vyuo vingine. Walimu waliokuwa wanafundisha vyuo hivyo wanapoteza ajira zao na mpaka sasa hawajui kinachoendelea. Naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuahirisha, nipate ufafanuzi kuhusu hatima ya wanafunzi na walimu waliokuwa kwenye vyuo hivi, hasa walimu na wafanyakazi, hatima yao ya ajira ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kitengo hiki cha ukaguzi kipewe fedha zote zilizotengwa pamoja na miundombinu kama magari. Ili kuboresha elimu yetu, ni muhimu kuboresha kitengo hiki cha ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuna kanda ambazo hakuna technical college hata moja. Vyuo hivi vinasaidia sana wahitimu kujiajiri hasa wale waliomaliza Form IV na Form VI. Mheshimiwa Waziri, Kanda wa Ziwa wanaomba angalau chuo cha ufundi kimoja. Ni mengi mazuri yanayofanywa na Serikali yangu ya Awamu ya Tano, naomba nishauri hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bila utafiti na pia walimu wa sayansi ni tatizo. Nashauri fedha inayotengwa kwenye utafiti na hasa vyuo vikuu zitolewe zote ili utafiti uendelee. Ni muhimu sana kuendelea kupunguza hili tatizo la walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Kila Wilaya Kuwa na Chuo cha VETA na hasa wilaya za pembezoni lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.