Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwako bado na tatizo la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu hasa watoto wanaotoka katika familia duni ambapo hawana uwezo wa kufuatilia na hawana watu wanaoweza kuwasemea. Nina mfano wa wanafunzi ambao ni wa kike na walifaulu masomo yao ya sayansi na mmoja alikuwa ni mwenye ulemavu, lakini ameomba mkopo mfululizo kwa miaka mitatu hakufanikiwa hadi alipokuja kwangu na kuomba nimsaidie kwa sababu awali shirika langu la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na yatima lilimsaidia toka shule ya msingi hadi sekondari. Baadaye shirika likawaachia ndugu waendelee kumhudumia lakini hatimaye huyu alikatishwa tamaa na kukosa mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifuatailie hasa watoto yatima na wanaoishi maisha hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu kufungia Vyuo vya Dini. Kumekuwa na ufungaji wa Vyuo Vikuu kiholela. Kwa kuwa vyuo hivi vimesajiliwa na Serikali, basi wapate maelekezo na kukaguliwa mara kwa mara; na kunapokuwa na upungufu warekebishwe badala ya kuwafungia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi zisaidiwe kulipia mitihani. Kwa kuwa elimu bila malipo ni kuwa Watanzania wote, basi naomba watoto wanaosoma kwenye shule binafsi wapewe pia ruzuku kwa ajili ya mitihani na hasa kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wanaotoka katika mazingira hatarishi na yatima ambao wamesaidiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, wamefaulu kwenda VETA za Serikali, wamefukuzwa. Wanadai mashirika hayo yawalipie wakati mashirika hayo yamekuwa yakijitolea tu. Matokeo yake vijana hawa wanakatishwa tamaa na kuacha vyuo. Nina mfano halisi wa kijana ambaye amefukuzwa kule Chuo cha VETA cha Morogoro, anaitwa John Mwingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkanganyiko mkubwa sana wa mitaala ya shule za msingi. Kulitoka mtaala wa shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita na kwamba watoto wataishia darasa la sita na kujiunga na sekondari. Hadi sasa hivi wanafunzi wanaendelea kufundishwa kwa mtaala huo ambapo hata vitabu vyake havipo. Hivyo walimu wanafundisha katika mazingira magumu. Naomba Mheshimiwa Waziri atoe mwelekeo wa nini kifanyike ili kurekebisha mkanganyiko huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni tatizo la uhamisho wa walimu. kuna walimu wanakaa shule za vijijini kwa muda mrefu hadi wanazeeka huko vijijini. Wanaishi katika mazingira magumu bila hata motisha. Naomba wakikaa miaka kadhaa wahamishiwe maeneo ambayo yana unafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kupungua kwa bajeti ya elimu. Bajeti ya Wizara ya elimu pekee imepungua kutoka shilingi trilioni 1.408 kwa mkwa 2018/2019 hadi shilingi trilioni 1.357 kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Upungufu huu ni wa shilingi bilioni 51. Elimu haiwezi kuwa bora kwa mfumo huo. Naomba pesa zinazotakiwa kwenye Wizara hii ya Elimu ziende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.